Villa Park, Uingereza
Kama ilivyokuwa msimu uliopita, maswali yanazuka kuhusu Alejandro Garnacho ambapo miezi miwili baada ya kujiunga na Aston Villa kwa mkopo wa awali, winga huyo bado hajathibitisha thamani yake kwa kocha Unai Emery.
Mshambuliaji huyo wa Argentina amecheza dakika 31 pekee akiwa na Villa, akitokea benchi katika mechi tatu tofauti na dakika 15 alizocheza dhidi ya Hull ndio muda mrefu zaidi alioutumia uwanjani katika mechi moja.
Garnacho amekuwa mchezaji wa akiba ambaye hakutumika katika mechi nne zilizopita za Villa, akishuhudia kutoka benchi timu hiyo ikishinda mabao 3-2 dhidi ya Tottenham siku ya Jumamosi.
Goli moja na pasi nne za mabao katika mechi 24 za Ligi Kuu ya England akiwa na Chelsea msimu uliopita, vilikuwa chini ya matarajio ya klabu hiyo kwa mchezaji huyo iliyemsajili kutoka Manchester United kwa pauni milioni 40, hivyo akaruhusiwa kuondoka.
Msimu huu ndio kwanza una mwezi mmoja, lakini Garnacho, mwenye umri wa miaka 22, huenda tayari anajikuta katika njia panda akiwa Villa Park.















