Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea Historia ya Dini ilivyokuwa wakati wa Mapinduzi ya Viwanda (Industrial Revolution) barani Ulaya. Leo tunawaletea Misingi na Haki ya Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa. Sasa endelea…

Mwaka 1967 Papa Paulo VI (1963-1978: wa 262) alitoa barua yake ya Kichungaji “Populorum Progressio,” yaani ‘Maendeleo ya Binadamu’. Licha ya mengine, alisisitiza kwamba hakuna maendeleo ya kweli, kama siyo ya binadamu wote.
Anasisitiza juu ya wajibu wa mataifa tajiri kusaidia yale maskini. Wakati wa kuadhimisha miaka 80 tangu itolewe barua ya Rerum Novarum Mei mwaka 1891, Papa Paulo VI alitoa barua ya Kitume mwezi Mei 1971 “Octogesima Adveniens”, yaani ”Ujio wa Miaka Themanini”.
Katika barua hiyo, aliongelea hasa hali duni katika miji. Tarehe 26 Oktoba 1975 alitoa barua nyingine ya “Evangelii Nuntiandi”, yaani “Utangazaji wa Injili”, ikiadhimisha miaka 10 ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano (1962-1965), alisisitiza kwamba kazi ya Kanisa ni kupigana dhidi ya uonevu na udhalilishaji.
Papa Yohana Paulo II (1978-2005: wa 264) alitoa barua mbili kukazia mafundisho hayo ya Kanisa juu ya jamii. Mwaka 1981 ikiwa miaka 90 tangu barua ya Rerum Novarum, aliandika barua ya kitume ya “Laborem Exercens” akisisitiza kwamba haki binafsi ya kuwa na mali haipashwi kuathiri umma, yaani haki ya wote kuwa na mali au kukiuka haki za jamii.
Papa Yohana Paulo II alirudia mawazo hayo kwa mkazo zaidi, hasa akikosoa ubepari uliopindukia, na ujamaa hasi katika barua yake nyingine ya kitume “Centesimus Annus” ya mwaka 1991, akiadhimisha miaka 100 ya Rerum Novarum.
Kwa namna hii, unaonekana umuhimu wa barua ya Papa Leo XIII (1878-1903: 256) iliyolitoa Kanisa katika makucha ya mabepari bila kuiingiza katika utumwa wa wajamaa hasi, au ukomunisti. Kabla Papa Yohana Paulo II hajafariki mwaka 2005. ulitolewa muhtasari (Compendium) ya Mafundisho ya Kanisa juu ya jamii.
Papa Benedikto XVI (2005 -2013: wa 265) akifuata katika nyayo za watangulizi wake, mwaka 2009 alitoa barua ya Kitume “Caritas in Veritate”, yaani “Upendo katika Ukweli”.
Licha ya kusisitiza yale yaliyosemwa na watangulizi wake, pia aliisifu hasa barua ya kitume ya Papa Paulo VI ya mwaka 1967” Populorum Progressio” kwa kuongelea, siyo tu juu ya maslahi ya wafanyakazi, bali pia juu ya maendeleo ya binadamu mzima (Integral Developoment).
Papa Benedikto XVI alikosoa sana ubepari, akiuona kukosa utu na kuwa na ubinafsi wa kujitafutia faida kutoka kwa wengine bila kuona wajibu wa kurudisha vilevile kwa jamii. Alisisitiza juu ya haki za jamii kuzidi haki za mtu binafsi kupata faida. Alilaumu ubepari kwa madhara ya siki hizi, yakiwemo vilevile balaa la madawa ya kulevya.
Papa Fransisko (wa sasa: 2013: wa 266), mafundisho yake yote ni juu ya upendo na kujali. Mwaka 2016 alitangaza mwaka wa Huruma ya Mungu na Upatanisho. Mafundisho yote ya wakati huo yalikuwa Mungu atakuhurumia, nawe ukiwahurumia wengine.
“Kuweni na Huruma kama Baba yenu wa Mbunguni alivyo na Huruma.” Katika barua yake ya Kitume “Evangelium Gauduim” au “Furaha ya Injili” ya mwaka 2013, anasihi serikali mbalimbali na vyombo vya kimataifa vya fedha kuhakikisha kuwa watu wanapata haki za msingi, yaani kazi, afya na elimu.
Anakubali haki ya serikali kuingilia uchumi kwa wema wa umma. Anapinga utamaduni wa kuabudu fedha na kuacha soko huria kwa faida ya wachache, wakati wengi wanakuwa fukara. Analaami utofauti unaoongezeka kati ya walionacho na wasionacho.
Katika barua nyingine ya Kitume ya mwaka 2015 “Laudato Si”, ambayo ilipokelewa vizuri sana na watu wa rika na Imani mbalimbali, anaongelea siyo tu juu ya haki ya wanyonge, bali na ulazima wa kutunza mazingira, na kulaani matumizi mabaya ya nyenzo za dunia kwa sababu ya ulafi.
Aliongeza barua nyingine mbili akisisitiza juu ya upendo na kujali; “Gaudete et Exultate” yaani “Furahini na Kushangilia” ya mwaka 2018 na “Fratelli Tutti”, yaani “Sote ni Ndugu”, ya mwaka 2020.
Kanisa katika mafundisho yake ya kijamii katika miaka hii yote, imesisitiza juu ya mambo yafuatayo:

1.    Haki ya Uhai:
    Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu kutungwa mimba hadi kifo. Kila binadamu siyo tu ana haki ya kuishi, bali pia ana haki ya kupata heshima. Katika mafundisho yake yote, Kanisa linasisitiza kwamba kila binadamu ameumbwa katika sura ya Mungu, na watu wote wana haki sawa mbele ya Mungu, na hivyo wanastahili heshima.

2.    Auni (Subsidiarity):
    Hii ilisisitizwa hasa kuanzia na barua ya Papa Pio XI ya Quadragesimo Anno mwaka 1931. Madaraka ya juu yasichukue kile ambacho madaraka ya chini yanaweza, na yana haki nacho. Mkubwa asaidie kile ambacho mdogo hawezi peke yake kufanya, la sivyo unamnyang’anya heshima na juhudi zake.

3.    Mshikamamno na kufanya juhudi kwa wema wa wote (Common Good):
    Watu hatuko kisiwa, hivyo lazima kusaidiana kama binafsi, kama junuiya, na kama mataifa.

4.    Upendo ndio upeo wa yote:
    Hapa siyo upendo wa kihisia, bali ni upendo wa kweli wa kujitoa kwa ajili ya wengine.
    Hayo maagizo manne yanakuwa msingi wa haki na wajibu katika Mafundisho ya Kanisa juu ya jamii kama haki ya kupata kazi; haki ya familia; haki ya uhuru wa kuabudu na kuwasiliana; utunzaji wa mazingira; haki ya kuwa na mali binafsi; kujali maskini; na wasiojiweza.

Masista na Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose Tagaste, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyofanyika parokiani hapo.

Baadhi ya Vijana waliopata Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, wa parokia ya Mtakatifu Ambrose Tagaste, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti hiyo.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, (aliyekaa) akiwa katika picha ya pamoja na Mapadri wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose Tagaste, na Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara. (Picha zote na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Tayari mwili wake umelala katika makaburi ya Kijiji cha Mpute huko mkoani Lindi, huku akiacha mabaki ya mtekenyo wa ala tamu za gitaa kwenye masikio ya mashabiki wake wa muziki wa dansi.
Ni ala za tamu na chungu,kwani kila shabiki anayekumbuka jinsi gitaa lilivyotekenywa kwenye wimbo maarufu wa ‘Kisa cha Mpemba’, ama ‘Bwana Kijiko’, anabaki kuwa na huzuni.Mtu huyu si mwingine bali ni marehemu Adolf Mbinga, mtaalamu wa kucharaza gitaa la solo na rhythm.
Mbinga ambaye alizaliwa mwaka 1967, alianza kuupenda muziki tangu akiwa kijijini kwao Mpute ambako mara kadhaa alikuwa akitumika kama miongoni mwa washereheshaji kwenye shughuli za jando, mwanzoni mwa miaka ya 1980.
Alikuwa akitumia sana gitaa la asili lililofungwa na kamba na nyaya katika shughuli hizo za jando.
Baadaye mwaka 1988 akajiongeza na kujiunga na Bendi ya Mondomondo huko Nachingwea.Mwaka 1989 akatua Dar es salaam akitokea ‘bush’ na kujiunga na Bendi ya Biko Stars na hakudumu, kwani mwaka 1992 akatimkia Bendi ya Carnival, na kupewa gitaa la rhythm.
Baadaye akapita bendi zingine nyingi, ikiwemo Diamond Sound, Twanga Pepeta, Mchinga Sound, na nyingine nyingi, ikiwemo Sikinde.
NEEMA
Huu ni wimbo wa kwanza kwa Mbinga kutunga katika maisha yake ya muziki akiwa na bendi ya Diamond Sound. Hiki pia ni kisa cha kweli ambacho kilimtokea mwenyewe wakati akiishi geto pale Kinondoni. Alimpata msichana kwa lengo la kuishi naye, lakini alimkimbia kwa sababu hakuwa na pesa.
Wimbo huo aliutunga mwaka 1996 akiwa na Diamond Sound, maarufu kama wana Kibinda Nkoi, ambao miaka hiyo ndiyo walioanza kuichangamsha nchi kwa miziki ya dansi la kizazi kipya.
KISA CHA MPEMBA
‘Kisa cha Mpemba’ ni miongoni kwa nyimbo maarufu kutunga akiwa Twanga Pepeta, na uliompa umaarufu. Wimbo huu ulitengenezwa mwaka 1998 katika studio za MJ Records (Master J). Hiki ni kisa cha kweli kabisa ambacho kilitokea Tabata ambapo Mbinga alishuhudia purukushani ya muuza duka mmoja (Mpemba) aliyepata sekeseke kutoka kwa jamaa ambaye mkewe alikuwa anapewa vyakula vingi kutoka duka la Mpemba huyo, kuliko thamani ya pesa aliyoacha.
Mbinga akatumia kisa hicho na kutengeneza wimbo ambao ndani yake aliongeza vionjo.
MTUHUMIWA
Mtuhumiwa si wimbo bali ni jina la utani alilopewa na wenzake mara baada ya kuiasi bendi ya Mchinga Sound.
Ikumbukwe kwamba mwaka 2000, Mbinga aliondoka ghafla katika bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’ na kwenda kumshawishi Mheshimiwa Mudhihiri Mudhihiri ambaye alikuwa Waziri kwa wakati huo, aanzishe bendi yake ambaye naye alikubali na kununua vifaa vya muziki.
Baada ya ushawishi huo kukubalika, ndipo wakaunda bendi ya Mchinga Sound ambayo ndani yake alikuwemo Mbinga mwenyewe, Mwinjuma Muumini, Deo Mwanambilimbi, Roshi Mselela, Rogart Hega Katapila, na wengine wengi.
Mbinga alitoka na tungo iitwayo ‘Kidomodomo’ambayo aliitunga akiwa Twanga Pepeta na kwenda kuirekodi Mchinga, na kufuatiwa na nyimbo zingine nzuri kama Kisiki cha Mpingo, na Fadhila kwa Wazazi.
Nyimbo zote za Mchinga Sound, kazi za kurekodi gitaa la solo na rhythm zilifanywa studio na Mbinga mwenyewe.
Wakati Mchinga Sound ilipokolea na kuwa maarufu nchini, ghafla Mbinga ambaye alikuwa kiongozi mkuu, aliondoka kwenye bendi hiyo na kurudi Twanga Pepeta. Kwa tafsiri nyingine ni kama alimuacha kwenye mataa Mheshimiwa Mudhihiri asijue nini cha kufanya, hasa ikizingatiwa alikuwa hajui lolote kuhusu masuala ya muziki, ikiwemo kuongoza bendi.
Hicho ndicho kikawa chanzo cha bendi hiyo kuvunjika na kusambaratika, kwani wanamuziki wengine wote waliondoka na kwenda kwenye bendi zingine.
Aliporudi Twanga Pepeta, wanamuziki wenzake walimpa Mbinga jina la mtuhumiwa wakiamini kwamba Mheshimiwa Mudhihiri alimtuhumu kwa usaliti wa bendi ya Mchinga Sound.
Hivyo, Mbinga ameondoka duniani akiwa ameacha majina ya utani ya ‘Mtuhumiwa’ na ‘Chinga One’.Jina la Chinga One lilitokana na kabila lake la Kimakonde.
KIFO CHAKE
Mwanzoni mwa mwaka huu, Mbinga aligundulika kwamba anaumwa mara baada ya ndugu, jamaa na marafiki kubaini kutetereka kwa afya yake.
Inaelezwa kwamba alikuwa akiumwa kwa muda mrefu ugonjwa ambao mwenywe hakutaka kuuweka hadharani, lakini aliwaficha hata ndugu na jamaa hadi kufikia katika hali mbaya.Jambo baya zaidi, alikuwa hataki kutumia dawa alizokuwa anapewa hospitalini.
Kufuatia hali yake kuwa mbaya zaidi, ilifikia hatua ikabidi asafirishwe kurudishwa kijijini kwao Mpute, ambako usiku wa Juni 15 mwaka huu, alifariki dunia na kuzikwa Juni 17.

LONDON, England
Dillian Whyte yuko tayari kwa mechi ya marudiano na mpinzani wa uzito wa juu wa Uingereza, Anthony Joshua, katika ukumbi wa O2 Arena, Agosti 12 mwaka huu, lakini kifungu cha marudiano ya pambano hilo, ni mazungumzo magumu.
Whyte ambaye ni mwana masumbwi mahiri na alimshinda Joshua, kabla ya AJ kumshinda mwaka 2015 na sasa Whyte bado anataka nafasi ya kulipiza kisasi hasara hiyo.
Whyte alianza tena mazungumzo wiki jana baada ya kumpinga kwa maneno promota Eddie Hearn kuhusu kukatika kwa mawasiliano kuhusu mechi ya marudiano inayotarajiwa kuwa kubwa, ambayo inatarajiwa kuandaliwa katika uwanja wa The O2 mnamo Agosti 12.
Whyte ana ushindani wa muda mrefu na Joshua na alimshinda AJ kama mwanariadha, kabla ya Joshua kushinda medali ya dhahabu ya Olimpiki huko London mwaka 2012.
Na Joshua tayari amekuwa akihusishwa na pambano linalotarajiwa kupigwa na Deontay Wilder, litakalofanyika Mashariki ya Kati baadaye mwaka huu.

Nottingham, England
Andy Murray anajiandaa kwa Wimbledon yake ya 15, itakayoanza Julai 3 mwaka huu, huku nyota huyo mwenye umri wa miaka 36, lakini hatazami kustaafu hivi karibuni.
Andy Murray anatumaini Wimbledon ya mwaka huu haitakuwa yake ya mwisho, akisema kwamba anataka kujituma kwa kucheza kwa kiwango cha juu sana kabla ya kutundika daluga lake.
Murray alitolewa katika robo fainali na Sam Querrey huko Wimbledon mnamo 2017, na kazi yake ilionekana kuwa mwisho baada ya kutolewa kwenye Australian Open mnamo mwaka 2019, lakini upasuaji wa kurekebisha nyonga yake ulimpa nafasi ya pili mchezaji huyo wa zamani wa Ulimwengu.
Ushindi wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 katika michuano ya hivi majuzi ya Nottingham Challenger, ulimpeleka kwenye cheo chake cha juu zaidi tangu upasuaji wake wa nyonga akiwa nambari 38 duniani.
Murray aliorodheshwa katika nafasi ya 839 duniani mnamo Julai 2018 alipopata nafuu baada ya upasuaji wake wa kwanza wa nyonga, kushindana na Grand Slams tena kulionekana kuwa tumaini la kusikitisha, lakini amepambana, na sasa ana matumaini makubwa ya kushindana tena katika daraja la juu la mchezo huo.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Ukikatiza katika mitaa mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, hasa muda wa jioni, utakutana na vikundi vya vijana wakicheza soka.Mara nyingi huwa wanakuwa na timu zao zenye majina yaliyobeba mitaa wanayoishi.
Pia, huenda mbali zaidi na kuanzisha ligi za mtaani ambazo hutumika kuburudisha nafsi zao na za mashabiki wao.
Wachezaji hunufaika na zawadi zinazowaniwa kwenye ligi husika kama vile mbuzi, ng’ombe, kuku pamoja na malipo ya kiasi kidogo cha fedha, huku mashabiki wakinufaika na burudani wanayopata kupitia timu za mitaa yao.
Utamaduni huo wa soka la mtaani umeibua jina maarufu la ‘Ndondo’.Jina hili limeibuka tangu miaka ya zamani, hasa kutokana na mtindo wa ligi na wachezaji wake.
Mtindo wenyewe ni namna wachezaji wanavyopatikana na kutumika katika timu za mitaani.
Neno ‘ndondo’ limeibuka kutoka kwenye wali maharage, na kama usivyofahamu, mboga ya maharage imepewa jina la ndondo, kivipi? Katika miaka ya zamani, wachezaji wengi wa mtaani malipo yao hasa yalikuwa wali na maharage, kwa maana kwamba mchezaji akitakiwa na timu fulani kwa ajili ya mechi za mtaani, atatakiwa kukusanyika na wenzake mapema kabla ya mchezo, na kinachofuatia ni kula wali na maharage, kisha mechi ikimalizika anapewa neno ‘asante’ na kuondoka.
Ikitokea viongozi husika wa timu wakijiongeza, mchezaji anapata walau nauli ya kwenda na kurudi pamoja na wali maharage.
Katika miaka ya hivi karibuni hadi sasa kumekuwa na mabadiliko kiasi, kwani licha ya mchezaji kula wali na maharage, pia hupewa posho fulani ambayo ndani yake inaweza kumsaidia kwa nauli na kununua mahitaji yake mengine madogo madogo.
Kutokana na kuwepo kwa staili hiyo, ndipo neno ‘ndondo’ likawa linatumika na kuvuma, hata wachezaji wenyewe wa mtaani wakikodiwa sehemu kwenda kuichezea timu fulani, utasikia “Ninakwenda kwenye ndondo”, akimaanisha anakwenda ‘kupiga’wali maharage na kucheza soka.
Huko kwenye soka la ‘ndondo’ masuala ya usajili yapo kama yalivyo kwenye ligi kubwa, ingawa tofauti yake ni kwamba usajili wa soka la mtaani hufanyika kulingana na mashindano maalum, na si msimu mzima wa mwaka ama miaka.
Kwenye soka la ‘ndondo’, kwa mwezi mchezaji anaweza kuchezea hata timu 10 zinazoshiriki michuano tofauti kwenye maeneo tofauti, kwa mfano, anaweza kuchezea timu A ya ligi fulani ya Ilala, na wakati huo huo akawa anachezea timu X ya ligi fulani ya mtaani huko Temeke, ilimradi tu hayo mashindano ya mtaani yawe hayana muingiliano wowote.
Kuna wakati hata wachezaji wanaocheza Ligi Kuu ama Daraja la Kwanza, nao wamekuwa wakiongeza nguvu kwenye ligi hizi za mtaani, wakiamini kwamba wanatoa mchango kwa timu za mitaa yao ambazo zimewalea na kufika walipofika.
Kwenye ligi hizo za mtaani, kama ikitokea kuna ligi ya kuwania kombe la mbuzi, basi mbuzi huyo atachinjwa na kuliwa na wali, pamoja na wachezaji wote walioshiriki kupata ubingwa.
Mbali na yote, mechi za mitaani ndizo zinazosaidia kuibua vipaji vya wachezaji ambao leo hii wanang’ara katika timu za Ligi Kuu nchini, hasa kutokana na kukosa mfumo thabiti wa kukuza vipaji vya vijana wadogo, kama ilivyo katika nchi zingine.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Kocha mkuu wa timu ya KMC ya Kinondoni Jamhuri Kihwelo amesema anataka kufanya mpango wa kumshawishi golikipa mstaafu Juma Kaseja, ili msimu ujao arejee langoni kuitumikia tena timu hiyo.
Kaseja alitangaza kustaafu soka mwishoni mwa msimu wa 2021/2022 akiwa na timu ya KMC na kuhamia kwenye jukumu lingine la kuwa kocha wa magolikipa wa timu za taifa.
Kihwelo, maarufu kama Julio, hivi karibuni alivutiwa na kiwango kilichoonyeshwa na nyanda huyo wa zamani wa Moro United, Simba SC, Yanga na Taifa Stars, wakati alipoichezea timu ya Ali Kiba katika mechi ya hisani dhidi ya timu ya Mbwana Samatta.
Katika mechi hiyo ya tamasha la SamaKiba, Kaseja alionyesha kwamba bado ana kitu anaposimama langoni, licha ya timu yake kufungwa mabao 4-2 na timu ya Samatta kwenye uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es salaam.
“Kaseja bado ni kipa mzuri sana licha ya kustaafu.Nikiwa kama kocha wa KMC, nitamshawishi ili aweze kurudi na kuitumikia timu hii msimu ujao,”alisema Julio.
Alisema kwamba Mungu akipenda atamchukua kipa huyo na kumrejesha ndani ya KMC kwa sababu ni mtu anayejitambua kwa kujali mazoezi, na bado uwezo wa kudaka anao.
Hadi gazeti linaingia mtamboni, juhudi za kumpata Kaseja mwenyewe ziligonga mwamba kufuatia simu yake kuita bila kupokelewa, ingawa mara ya mwisho wakati ametangaza kustaafu soka, alidai kuwa amefanya hivyo ili kuwapa nafasi vijana wanaochipukia kwa sasa.
Mbali na hilo, inaelezwa kwamba alichoshwa na maneno ya watu waliokuwa wakimzodoa kwa madai kwamba anaziba nafasi za vijana, wakati yeye tayari umri wake umekwenda.
Kaseja alianza kuonekana kwenye medani ya soka la ushindani mwaka 2000 akiichezea Moro United aliyojiunga nayo ikiwa Ligi Kuu, akitokea Shule ya Sekondari ya Makongo, na kucheza kwa msimu mmoja.
Mwaka uliofuata alijiunga na Simba aliyoichezea kwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 kwa misimu tofauti.
Pia, Kaseja aliichezea Yanga katika vipindi viwili kama ilivyo kwa Simba, na baadaye alijiunga na Kagera Sugar, kisha kutimkia Mbeya City, na kumalizia KMC.

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Nicholaus wa Tolentino, Msingwa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kipaimara hivi karibuni parokiani hapo.