DAR ES SALAAM
Na Arone Mpanduka
L’Orchestra African Fiesta, mara nyingi ilijulikana kama African Fiesta, ilikuwa bendi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yenye mtindo wa soukous, iliyoanzishwa na Tabu Ley Rochereau na Dk. Nico Kasanda mnamo mwaka 1963.
Tabu Ley Rochereau(kwa sasa marehemu) ni mwanamuziki mwenye historia ndefu katika tasnia hiyo, aliyezaliwa Novemba 13, 1940 huko Bandundu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC).
Kwa kushirikiana na mpiga gitaa Dr. Nico Kasanda, waliasisi muziki wa Soukous ambao uliwafurahisha Waafrika kwa muda wa miongo minne, wakiutangaza muziki huo kimataifa kwa kuunganisha muziki wa asili ya Kongo na Cuba, Caribbean na Rumba ya Latin America (Amerika ya Kusini).
Tukianzia mwaka 1954, akiwa na umri wa miaka 14, Tabu Ley aliandika wimbo wake wa kwanza ulioitwa ‘Bessama Muchacha’ aliourekodi akiwa na Bendi ya African Jazz ya Joseph Kabasele (Grand Kale ama Pepe Kalle), na baada ya kumaliza elimu ya juu, alijiunga na bendi hiyo kama mwanamuziki kamili.
Tabu Ley aliimba wimbo wa kupigania uhuru wa watu weusi ulioitwa ‘cha cha’ ambao ulitungwa na Joseph Kabasele ‘Grand Kale’ wakati Congo ilipopata uhuru mwaka 1960, wimbo ambao ulipelekea yeye kupata umaarufu mkubwa.
Alibakia na bendi ya African Jazz mpaka mwaka 1963 wakati yeye na Dr. Nico Kasanda walipounda kundi lao lililoitwa African Fiesta.
Miaka miwili baadaye, Tabu Ley na Dr. Nico walitengana, na Tabu Ley aliunda kundi lake lililoitwa African Fiesta Nationale, pia bendi hiyo ilifahamika kama African Fiesta Flash. Kundi hilo lilikuwa na mafanikio kwa kuongoza mauzo katika historia ya Afrika.
Mwaka 1970 alirekodi wimbo uliokuwa umeshika chati za juu za Kiafrika uliojulikana kama Afrika Mokili Mobimba, na uliuza zaidi ya nakala milioni moja.
Mzee huyo alifyatua nyimbo zingine kali za Ibragimu, Sukaina, Ponce Pilate, Cadance Mudanda na Boya Ye. Zingine zilikuwa Mbanda ya Ngai, Maze,Nzale, Sima Mambo Revens Itou, Nalingi yo Linga, Nadina, na nyingine nyingi.
Papa Wemba na Sam Mangwana walikuwa ni miongoni mwa wasanii maarufu wa muziki wa Kiafrika ambao walikuwa sehemu ya kundi hilo.
Sambamba na kundi la Franco Luambo Lwanzo Makiadi lililoitwa T.P.OK. Jazz, kundi la Afrisa lilikuwa moja kati ya makundi makubwa ya Kiafrika. Walirekodi nyimbo kama vile Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo.
Katikati ya miaka ya 1980, Tabu Ley alivumbua vipaji vya waimbaji na wachezaji.Mwanamama M’bilia Bel ndiye aliyesaidia kuipa bendi yake umaarufu zaidi. M’bilia Bel alikuwa mwimbaji wa kwanza wa kike wa muziki wa Soukous, na kukaribishwa kwa shangwe Afrika nzima.
Baadaye Tabu ley na M’bilia Bel walioana, na harusi yao ilifungwa ndani ya ndege wakati wakiwa hewani, na baada ya harusi, wakafanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike waliyemwita Melodie kwa jina.
Mnamo mwaka 1988, Ley alimtambulisha mwimbaji mwingine wa kike Faya Tess. Lakini baada ya ujio wa Tess katika bendi hiyo, kulimfanya M’bilia kuondoka kwa kile kilichoelezwa kuwa wivu wa kimapenzi baina ya wana ndoa hao ulioingilliwa na Faya Tess.
Mara baada ya M’bilia Bel kujitoa katika kundi la Afrisa Intrenationale, pamoja na upinzani mkubwa na kundi la T.P.OK. Jazz, Bell aliendelea kupoteza umaarufu.
Mwanzoni mwa miaka ya 1990, Tabu Ley aliishi Kusini mwa California nchini Marekani, na alianza kurekebisha muziki wake ili uendane na mashabiki wa kimataifa kwa kuingiza lugha ya Kiingereza katika mashairi yake.
Alipata mafanikio kwa kutoa albamu kama vile Muzina, Exile Ley, Africa Worldwide, na Babeti Soukous.
Mwaka 1996, Tabu Ley alishiriki katika albamu ya Gombo Salsa iliyotengenezwa na Salsa Music Project Africando. Wimbo uliojulikana kwa jina la ‘Paquita’ kutoka katika albamu hiyo, ikiwa ni toleo jipya alioimba mwishoni mwa miaka ya 1960 katika bendi ya African Fiesta, na ulishika chati katika medani ya muziki.
Mwishoni mwa miaka ya 1990 Rais Mobutu Sese Seko Kuku Ng’endu Wazabanga alipoondolewa madarakani (mwaka 1997), Tabu Ley alirudi Kinshasa na alipewa nafasi ya Uwaziri katika Baraza la Mawaziri katika Serikali mpya ya Rais Laurent Kabila.
Kufuatia kifo cha Laurent Kabila miaka miwili baadaye, Tabu Ley aliendelea na wadhifa huo chini ya Rais Joseph Kabila.
Katika miaka ya 2000, Tabu Ley alianza kupatwa na maradhi, ikiwemo ugonjwa wa kiharusi ambao ulisababisha kufariki kwake ulipofika mwaka 2013.
Tabu Ley alikuwa katika hali mbaya kiafya toka mwaka 2008 baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi, na alikutwa na umauti wakati akipatiwa matibabu katika hospitali moja nchini Ubelgiji.