Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akiwabariki Watawa wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Watawa iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo. (Picha na Yohana Kasosi)

DAR ES SALAAM

NA MATHAYO KIJAZI

Watawa nchini Tanzania wametakiwa kutokengeuka, wakidhani mahali walipo wamepotea njia, bali watambue kuwa wanapaswa kuyaishi yale waliyoyapokea kwa furaha, kwa sababu wao ni zawadi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya Kanisa.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati akitoa homilia katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Watawa iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo.
“Nasema hivyo nikijua kwamba hapa na pale, wapo Watawa wanaokengeuka, wako wanaodhani wamepotea njia, na katika mahangaiko, wanabadili mwelekeo….
“Naomba yale ambayo mmeyapokea kwa unyofu, mmeyapokea kwa furaha, na mmetamka kwa hiari yenu kwamba mtayaishi, basi muyaishi,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Aidha, Askofu Ruwa’ichi aliwashukuru wote kadri ya karama zao mbalimbali, akiwaomba kuziendeleza karama hizo katika maisha yao.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliwataka Watawa hao kuwa watii kwa Mungu na mpango wake, kwa ajili yao na Kanisa, pia Ulimwengu.
“Tumejitosa kwa nadhiri zetu kumfuata Kristo, Nuru ya Ulimwengu, ambaye ni Mtii, ambaye ni Fukara, ambaye ni mwenye Usafi Kamili wa Moyo.
“Na kama ndivyo, basi tunao wito wa kuwa watii, watii kwa Mungu na mpango wake kwa ajili yetu, kwa ajili ya Kanisa, na kwa ajili ya Ulimwengu,” alisema Askofu Ruwa’ichi.
Alisema kuwa watawa hao wanatakiwa kuwa wasafi wa moyo, wakiishi kitakatifu, wakiishi kwa upendo, na kushuhudia na kuutangazia Ulimwengu upendo wa Mungu.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Ruwa’ichi katika Ulimwengu wa sasa, wapo wanaowashangaa Watawa kwa kukubali kuishi maisha ya ufukara, usafi wa moyo na utii, wakidhani kwamba wamepotea njia, bali watambue kuwa mbele ya Mungu, maisha ya Wakfu, ni Matakatifu.
Aliwataka Watawa kuuishi utakatifu wa maisha yao pamoja na ushuhuda unaowapasa, ili kwa njia yao, Kristo atambulike, aungamwe, na aaminiwe na wengi.
Askofu Mkuu aliwasisitiza Watawa hao kuwa na shauku ya kumuona, kumpokea, kumuungama, pamoja na kumtukuza Kristo kwa maisha matakatifu na ya kumpendeza Mungu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Wakristo wametakiwa kufuata nyayo za Mtakatifu Theresa wa Kalkuta za kuwasaidia watu wenye uhitaji, hasa wanaoteseka kiroho, ili wawapatie faraja katika maisha yao ya kila siku.
Hayo yalisemwa na Sista Carmela anayefanya utume wake katika Kituo cha Furaha na Amani kilichopo Parokia ya Familia Takatifu – Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, baada ya Tumaini Media kufanya matendo ya huruma Kituoni hapo.
“Karibuni katika Kituo hiki cha Furaha na Amani, kama mnavyoona hapa kuna watoto, wazee pamoja na walemavu... Kituo hiki siyo kipya sana, kwani kilianzishwa mwaka 1976, na kimetoa huduma kwa miaka hiyo yote, na bado kinaendelea kutoa huduma.
“Tunafuata nyayo za Mama Theresa wa Kalkuta, kile alichokifanya, na anatamani na sisi tuendelee kukifanya, kuwatembelea na kuwajua wenye shida au wahitaji, siyo tu kwa ajili ya mavazi au chakula, wapo watu wengine ambao wanateseka kiroho, kwa hiyo tunatakiwa kuwagusa waliokata tamaa ili warudi kwa Mungu,” alisema Sista Carmela.
Aliongeza kuwa ni vyema kila mmoja akajitahidi kuwa mwanga kwa wengine, ili wanapomwona yeye, wamwone Mungu kutokena na jinsi yeye anavyoishi.
Sista Carmela aliwashukuru wafanyakazi wa Tumaini Media pamoja na wadau mbalimbali kwa majitoleo yao katika kituo hicho, akiwaomba kuendelea na moyo huo, kwani Mungu anawaita wote ili wawe Watakatifu.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu- Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kassembo aliwashukuru Wanatumaini Media waliokwenda kufanya matendo ya huruma.
“Lakini kwa namna ya pekee tunaishukuru sana familia ya Tumaini Media kwa majitoleo yenu mazuri. Hapa tunajifunza jambo moja - ‘furaha katika kutoa’. Tunapomtolea Mungu, tunabarikiwa zaidi;
“Kwa hiyo Mungu azidi kuwabariki, na hasa Wanatumaini Media tunapomshukuru Mungu kwa miaka 30 ya Utume wetu katika Kanisa, ni miaka mingi sana hiyo. Katika miaka yote hiyo, kuna watu wengi wamefaidika, kuna watu wengi wamepata uponyaji,” alisema Padri Kassembo na kuongeza,
“Tunaendelea kuwashukuru na kuwaombea kwa Mungu ili kazi hiyo iendelee zaidi kwa msaada wa Mungu, na kwa msaada wa Waamini ambao wanaendelea kujitolea kwa hali na mali ili kuhakikisha Injili inamfikia kila mmoja wetu,” alisema Padri Kassembo.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Tumaini Media, Arnold Kimanganu alisema kuwa kama Wakristo Wakatoliki, jukumu lao ni kushirikiana, akiongeza kuwa amefarijika kuona namna huduma inavyotolewa katika Kituo hicho.
Kimanganu alimshukuru Padri Kassembo kwa kuwa kiunganishi kizuri kwa Tumaini Media na Kituo cha Furaha na Amani.

NA MATHAYO KIJAZI

Wakati Redio Tumaini ikiadhimisha Jubilei ya Miaka 30 tangu kuanzishwa kwake maadhimisho ambayo yameonekana kufana, imeelezwa kuwa mtu anayetunza afya ya akili, ataweza kuamua na kutenda mambo mema maishani  mwake.
Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu- Mburahati, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Vitalis Kassembo, alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa Redio Tumaini kutimiza miaka 30, tangu kuanzishwa kwake Februai 3, mwaka 1994.
Aliwasisitiza Waamini kuitunza afya ya akili na roho, wakiitunza miili yao ili waendelee kuunda utakatifu katika maisha yao.
“Katika maisha, wengi wetu mara nyingi tunajikuta tunaumwa afya ya akili. Afya ya akili imetusababishia miili yetu isiwe na afya njema. Hata hivyo, magonjwa hayo yametufanya tuteseke mno, kwa sababu wakati mwingine unaweza kupewa habari ya msiba wa kifo cha mtu wako wa karibu, unjikuta unashikwa na ‘presha’ kwa kuwa akili yako haikuwa tayari kupokea habari hiyo,” alisema Padri Kassembo.
Padri Kassembo aliwaasa Waamini kuwa na utayari wa kumtumikia Mungu, kwani anayefanya mambo ya Mungu, na Mungu naye hufanya mambo ya mtu huyo.
“Tunakumbushana kufanya Tafakari ndugu zangu. Tuwe na utayari wa kumtumikia Mungu…kumbuka kwamba unapoamua kufanya mambo ya Mungu, na Mungu naye anafanya mambo yako,” alisema Padri Kassembo.
Ka mujibu wa Padri Kassembo Waamini wanatakiwa kujenga utamaduni wa kusameheana, wanapokoseana, kwani hiyo itawafanya wazidi kupokea baraka za Mungu katika maisha yao.
Aidha, Padri huyo aliipongeza      Tumaini Media, hasa Redio Tumaini kwa kutimiza miaka 30 tangu ilipoanzishwa, akisema chombo hicho cha habari kina mchango mkubwa katika kuinjilisha na kuhabarisha.
Alibainisha kwamba wapo wagonjwa ambao hawawezi kwenda popote, ila wanafarijika wanaposikiliza Redio Tumaini, kutazama Tumaini Tv, na kusoma taarifa mbalimbali zinazoandikwa katika gazeti la Tumaini Letu.
Kwa upande wake Mratibu wa Matukio ya Kanisa Tumaini Media, Gaudence Hyera, alimshukuru Padri Kassembo kwa kukubali Sherehe za Miaka 30 ya Redio Tumaini zifanyike parokiani hapo.
Hyera alisema kuwa Familia Takatifu ndiyo chanzo cha yote yanayoendelea kutendwa na Kanisa, hivyo Misa hiyo kuadhimishwa katika Parokia ya Familia Takatifu, ni kumshukuru Mungu aliyeamua Familia hiyo iwepo.

NA MWANDISHI WETU

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Dominiko - Mbezi Juu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Daniel Kilala amesema kuwa kila Mbatizwa anatumwa kupokea wajibu wa kutangaza Injili kwa maneno na matendo yake.
Padri Kilala aliyasema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Domonika ya Tano ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Paulo anatukumbusha wajibu wetu wa kuhubiri Injili. Sisi sote katika Ubatizo, tulipobatizwa, tumeshirikishwa Ukuhani, Ufalme, na Unabii wa Kristo. Kumbe kila Mbatizwa anapokea wajibu wa kutangaza Injili kwa maneno na matendo yake,” alisema Padri Kilala.
Padri huyo aliwaasa Waamini kuacha kukata tamaa, akiwasihi kuwa na matumaini kila wakati, kwani Mungu yuko pamoja nao kila wakati.
Aliwasisitiza kutokupenda tu mambo yao binafsi, bali wapende pia mambo yanayomhusu Mungu, akisema, “Watu wanapenda sherehe tu, hata ndoa nyingi zinavunjika kwa sababu ya kutokuwaombea wanandoa, badala yake watu wanaangalia tu sherehe wakati wa harusi,” alisema Padri Kilala.
Padri Kilala aliwaonya Wakristo kuepuka kutawaliwa na mambo ya anasa na choyo katika maisha yao, akisema kuwa jambo hilo linasababisha baadhi ya mambo yao kuwa magumu.
Aliwataka kuitumia Dominika ya Tano ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa kutafakari kuhusu mateso na mahangaiko mbalimbali wanayoyapata, huku wakizidi kumtumainia Kristo katika maisha yao.
Aliongeza kuwa hata wanapokumbana na changamoto mbalimbali za kimaisha, hakuna yeyote wa kumkimbilia, zaidi ya Kristo pekee, kwani yeye ndiye muweza wa mambo yote.
Alibainisha pia kuwa Waamini wanapaswa kutumia muda wao kuwasiliana na Mungu, huku wakitambua umuhimu wa sala, pamoja na kutenga muda maalum kwa ajili ya kusali.
Katika hatua nyingine, Padri Kilala aliwataka waamini kuitegemeza Tumaini Media kwa kuendelea kukiunga mkono chombo hicho, ili Injili iendelee kutangazwa Tanzania na duniani kote.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei wa Parokia hiyo, Neo Pascal, aliishukuru Tumaini Media kwa namna inavyoendeleza uinjilishaji, akiwasihi Waamini kuendelea kukitegemeza chombo hicho.
Naye Katekista Joseph Francis alisema kuwa wao kama Wakristo, hawana budi kuendelea kujikita katika sala, kwani hiyo itawasaidia kupata neema ya Mungu katika maisha yao.

NA CELINA MATUJA

Imeelezwa kuwa waamini wanashindwa kupata mafanikio katika maisha ya kiroho na kimwili kutokana na kusali kwa mazoea.
Hayo yalisemwa na Mlezi wa Karismatiki Katoliki Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, Padri Henry Rimisho katika Kongamano la Uponyaji lililofunguliwa jijini Dar es Salaam.
Alisema hayo katika mada aliyofundisha juu ya toba na Damu ya Yesu Kristo, ambayo ndiyo silaha ya kuondokana na changamoto zilizosababishwa na mazingira au binadamu.
Alieleza namna nzuri ya kufanya toba kwa kutumia Damu ya Yesu Kristo, akisema, “Kwanza, Mwamini anatakiwa kukiri kuwa amekosa; hatua ya pili ni majuto kwa kuwa toba ya kweli inafuata na majuto; kujutia ni ile hali ya kuikataa dhambi na kuumia; tatu, toba ili ikamilike, lazima mdhambi ageuke na kuanza ukurasa mpya na kufanya mema, katika kutenda haki iwe kwa wenzake, kwenye familia, ama kazini kwake.”
Aidha, Padri Rimisho alisema kuwa mtu anapogeuka na kukiri kwa Mungu, anajipatia furaha ambayo itakuwa sehemu ya maisha yake, na Mungu atammiminia neema na baraka tele.
“Hivyo, kwa kutumia Damu ya Yesu, inapata kutakatifuza, kutakasa maeneo, na hiyo ni kwa mujibu wa Maandiko Matakatifu yanayosema, “Kikombe hiki ni Damu ya Agano Jipya iliyomwagika kwa ajili yenu, ambapo Mwamini anapata kufahamu mambo matatu muhimu ambayo ni; Damu ya Yesu; ya Agano Jipya; na iliyomwagika kwa ajili ya mwanadamu….
“Ikumbukwe kwamba Yesu Kristo mwenyewe alikufa na alifufuka, hivyo katika kufa kwake, alitoa Damu Yake ya gharama kubwa, ili kumkomboa mwanadamu katika maisha hapa Duniani,” alisema Padri Rimisho.
Padri huyo alisema kuwa katika Agano la Kale, damu ya wanyama ilikuwa ni ishara ya kutambuliwa na kutokudhurika, kwa mfano katika kabila, na ilileta upatanisho, ilifunika dhambi, damu hiyo ilitolewa kila wakati na kila mwaka, na hasa pale walipohitaji kushughulikia dhambi.
Aliongeza kuwa Yesu Kristo alijitoa kwa kumwaga Damu yake ili kuondoa dhambi za mwanadamu, na anaiita Damu ya Agano Jipya kwa sababu yeye alikuja baada ya Agano la Kale, ambalo Mtume Paulo analiita Agano Kuu, ni Agano Jipya kwa utendaji wake Yesu Kristo Mwenyewe.
Padri Rimisho alisema kuwa dhambi zilikuwa zinafunikwa tu, haziondolewi wakati huo wa Agano la Kale, ila kwa Agano Jipya, zinaondolewa kabisa.
“Damu hii ya Yesu ambayo tunasema kuwa ni ya Ukombozi, ni kwa sababu Mwanadamu alikuwa utumwani mwa adui shetani. Hivyo, ililipa deni na kutoa uhuru, kwa sasa Yesu anakuwa ni mjumbe wa Agano Jipya,” aliongeza kusema Padri Rimisho.
Aidha, aliwafafanulia Waamini kazi ya Damu ya Yesu, akisema kuwa kwanza inamwondolea mtu agano la uharibifu, yaani la nguvu za giza; inatumika katika hali ya hatari, ama kuota ndoto chafu kwa kusali.
Aliongeza kuwa kwa kupitia Damu ya Yesu, mwanadamu anayelindwa na nguvu za giza, itanena msamaha, inafuta laana na dhambi ambazo mwanadamu anazotenda.
Kadhalika, Padri Rimisho alibainisha kuwa Damu hiyo inafungua maeneo yaliyofungwa na mazingira, na madhara yake ni kwamba mtu anaweza kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine akiwa na mafanikio makubwa maishani mwake, lakini ghafla maisha yake yanakuwa si ya kuridhisha, hivyo anaweza kutumia Damu ya Yesu.
Alisema kuwa Damu ya Yesu Kristo ni ya Agano Jipya, kwa kuwa iwatutoa wanadamu katika utumwa wa dhambi na maonevu ya shetani, hivyo ililipa deni la mwanadamu na Yesu, ambapo sasa ni mjmbe wa Agano Jipya.
Aliongeza kuwa ni lazima kuelewa kwamba Damu ya Yesu inavunja na kuharibu kila nguvu ya giza na agano la shetani, kwani wapo baadhi wanaota ndoto mbaya, na za kutisha.
Hata hivyo, Padri Rimisho alisema kwamba hakuna atakayedhurika ikiwa ataitumia Damu hiyo, kwani ina nguvu, na imemnunua kila mmoja, hivyo ni ulinzi unaofuta laana na dhambi zinazotendwa na mwanadamu.

NA MWANDISHI WETU

Mtandao wa Jinsia Tanzania (Tanzania Gender Networking Program: TGNP) umesema kwamba utaendelea kutekeleza kwa kishindo mpango wake wa kupinga vitendo vya ukatili ili kutokomeza ukeketaji nchini.
Afisa wa Idara ya Ujenzi Nguvu za Pamoja na Harakati, Flora Ndaba, akizungumza katika Kongamano la kupinga vitendo hivyo alisema kuwa wamejadili mada mbalimbali na kuona kwamba kuna jinsi ya kuwekeza katika wanawake na kwa mabinti walionusurika kukeketwa.
Alisema kuwa wametumia Bonanza na Sinema ambayo imeandaliwa na Mtandao huo kwa lengo la kupaza sauti zao kuujulisha Umma kuhusiana na Janga hilo la ukeketaji.
“Tupo kwenye Soko la Kivule, na hapa tupo na wadau ambapo kuna sinema ambayo imeandaliwa na TGNP,” alisema Flora.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii, Magdalena Msaki alibainisha kwamba wao wamejipanga kuzuia ukeketaji, kwani kisheria hasa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, ukeketaji ni kosa la jinai.
“Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 na iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019, ukeketaji ni kosa la jinai, kwa hiyo tunataka kutoa elimu kwa jamii inayotuzunguka katika Kata hizi tatu,” alisema Magdalena.
Kwa upande wake mmoja wa Wanaharakati wa Masuala ya Jinsia, Seleman Bishangazi alisema kuwa wameamua kushirikisha Vijana kwa madhumuni ya kupaza sauti zao ili jamii itambue kuwa ni jambo baya, na hivyo kuachana na jambo hilo.
Maadhimisho hayo yamebeba kaulimbiu “Sauti yangu, Hatma yangu” na kufanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam wilayani Ilala.

KASESE, Uganda

Askofu Francis Aquirinus Kibira Kambale wa Jimbo Katoliki la Kasese nchini Uganda, amewatahadharisha Wakristo dhidi ya ubaguzi kwa misingi ya Dini na kabila.
Aidha, amewasihi waamini hao kuhakikisha wanazingatia maendeleo na elimu kwa manufaa ya jamii husika, badala ya kuendekeza ubaguzi miongoni mwao.
Askofu Kibira alitoa onyo hilo katika hotuba yake baada ya kuadhimisha Misa Takatifu ya Shukrani ya Mchungaji Restetuta Biira Katusabe, binti wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu “Madada wa Banyateresa”, iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Nyabirongo, jimboni humo.
Katika hotuba yake, Askofu Kibira anayehusishwa na kusaka maendeleo, kuchukia umaskini na chuki miongoni mwa jamii kwa Wakristo waliopoteza ubinadamu kati yao, aliwataka waishi pamoja kwa amani.
Askofu Kibira alirejelea onyo lake la awali kwa wakuu wa familia dhidi ya kugawanya vipande vya ardhi miongoni mwa watoto, lakini kutumia ardhi iliyopo kwa tija ambayo itasaidia kuongeza mapato, ikiwemo karo ya shule kwa watoto wao.
Katika Misa hiyo, Askofu Kibira Kambale alimteua na kumtuma Padri Leosio Masereka kwenda kufanya utume katika Seminari Kuu ya Kitaifa ya Mtakatifu Paulo-Kinyamasika, baada ya kuhitimu Shahada yake ya Uzamivu (PhD) ya Liturjia kutoka Roma.
Askofu Kibira aliwaomba wazazi kuwatoa watoto wao ili wafanye kazi za Kanisa na kuwasaidia hasa katika elimu rasmi na isiyo rasmi, na kutaja familia kuwa shule ya kwanza, na wazazi ndio waalimu wa kwanza.
Akiongoza hotuba wakati wa Jubilei ya Fedha katika maisha ya Kidini ya shukrani ya Misa ya Mchungaji Jacinta Mbambu pamoja na kuadhimisha viwango tofauti vya elimu katika familia ya Padri Leosio, Askofu Kibira alibainisha kuwa kasisi huyo alimaliza PhD yake huko Roma, kabla ya kumteua kuwa Mhadhiri wa Seminari Kuu ya Kitaifa ya Mtakatifu Paulo.
Katika Homilia yake, Askofu Kibira aliwataka wazazi na walezi kufanya kazi ya kuwajenga watoto wao ili kuendana na huduma ya Kanisa na kuwekeza katika malezi ya watoto, huku akiwakumbusha kuendeleza upendo, msamaha na uvumilivu miongoni mwa mambo mengine.

NDOLA, Zambia

Jimbo Katoliki la Ndola nchini Zambia, limeweka historia kubwa kutokana na Jengo jipya la Kanisa katika Parokia ya Mtakatifu Antonio Fasani wilayani Ndola, ambalo limebarikiwa na kuwekwa wakfu.
Akihubiri katika adhimisho la Misa Takatifu ya uzinduzi wa kanisa hilo, Askofu Benjamin Phiri wa Jimbo hilo, alisema kuwa kiini cha wongofu wa kweli, ni kusika Neno la Mungu.
Alisema pia kuwa utakatifu wa kweli unaenea zaidi ya kuta za kanisa, akisema unyofu wa mioyo kama kipaumbele kuliko ukuu wa jengo lolote, kukumbusha kutaniko umuhimu mkubwa wa imani thabiti na ya kujitolea.
“Baraka na kuwekwa wakfu kwa jengo jipya la kanisa, siyo tu kuwa ni wakati wa kusherehekea, bali pia ni ukumbusho wa kuhuzunisha wa imani ya kudumu na roho ya Jumuiya ambayo inapaswa kuunganisha Parokia pamoja,” alisema Askofu Phiri.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Charles Tembe, aliwashukuru waamini wa Parokia hiyo kwa kujitolea kwao bila kuyumbayumba katika kulisaidia Kanisa.
“Tukio hili linasimama kama ushuhuda wa dhamira isiyoyumba ya Jumuiya ya Parokia ya Mtakatifu Antonio Fasani, ikiashiria sura mpya katika safari yao ya kiroho ndani ya kuta zilizowekwa wakfu za kanisa lao jipya lililobarikiwa,” alisema Padri Tembo.
Padri Tembo alisema kuwa huo ni wakati muhimu katika sherehe hiyo ya kuwekwa wakfu kwa madhabahu na Askofu Phiri, ambaye aliipaka mafuta na kuchoma uvumba, kuashiria utakaso wa nafasi hiyo takatifu.
Miongoni mwa watu waliohudhuria kuwekwa wakfu kanisa hilo ni Mkurugenzi wa Kichungaji, Padri Ephraim Mapulanga; Waziri wa Mkoa wa Copperbelt, Elisha Matambo, na Makuhani wengi na wanadini.

ZOMBA, Malawi
Jimbo Katoliki la Zomba nchini Malawi limetoa msaada wa unga wa mahindi uliosindikwa kwa watu walioathirika na njaa katika jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa kuchangia unga katika Parokia za Chipini na Lisanjala, Askofu wa jimbo hilo, Mhashamu Alfred Chaima aliwataka wanufaika wa msaada huo kuwaombea wananchi walioweka rasilimali pamoja katika kuchangia unga huo.