Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki
iliyopita, tulianza kuwaletea historia ya Mtaguso Mkuu wa Trento uliokutana katika kipindi ambacho Kanisa lilikuwa na changamoto. Leo tunaendelea kuwaletea historia ya Mtaguso Mkuu wa Trento licha ya upinzani mkubwa kutoka kwa wafalme, Papa Pius IV, aliweza kukiitisha Kikao cha Tatu cha Mtaguso wa Trento. Sasa endelea…
Papa Pius IV (1559-1565):
Papa Paulo IV, alifuatwa na Papa Pius IV mtu wa wastani. Papa Pius alijaribu kuyapa mageuzi ya Papa Paulo IV sura ya utu bila kuyageuza.
Katika kazi hii alisaidiwa na mpwa wake Karoli Borromeo aliyempa ukardinali na uwaziri mkuu akiwa na umri wa miaka 21 tu.
Bahati nzuri Borromeo alikuwa mtu mtakatifu na mwenye busara.
Kikao cha Tatu 1562-63:
Licha ya upinzani kutoka kwa wafalme, Papa Pius IV, aliweza kukiitisha Kikao cha Tatu cha Mtaguso wa Trento. Hitimisho hili liliwezekana kwa msaada wa uelewa na diplomasia ya Kardinali Karoli Borromeo.
Baada ya kuweka vizuri matokeo ya mazungumzo yote ya vikao vya mtaguso yaliyoweka bayana mafundisho ya Kanisa Katoliki na kuweka sheria za kudhibiti utovu wa nidhamu, Mtaguso ulihitimishwa Desemba 3, 1563.
Maazimio yake yaliwekwa sahihi na wawakilishi wanne wa Papa, mapatriarka 3, maaskofu wakuu 25, maaskofu 169, maabate 7 wa monasteri kubwa, wakuu wa mashirika ya watawa 7 na wasimamizi wa majimbo 10.
Vilevile wawakilishi mabalozi wa wafalme Wakatoliki waliweka sahihi zao. Papa alithibitisha maamuzi ya mtaguso huo na kutoa hati ya kuyafanya mafundisho rasmi ya kanisa.
Ni vizuri kuona baadhi ya mafundisho ya Mtaguso wa Trento kwa kifupi na sheria zilizowekwa kudhibiti utovu wa nidhamu. Kwanza tuone baadhi ya mafundisho ya imani ya Trento.
1. Tofauti na Waprotestanti waliosema kwamba imani inatokana na Biblia tu, Mtaguso wa Trento ulisema ukweli wa imani ya dini unatokana na Biblia pamoja na mapokeo ya kanisa.
Mapokeo ni yale mafundisho na desturi zilizotoka katika kanisa la mitume na kuja kwetu bila kuwa katika Injili.
2. Vitabu vyote vya Biblia kama vinavyokutwa katika Biblia ya Septuaginta, vimeandikwa chini ya uvuvio wake Roho Mtakatifu na ni sehemu ya maandiko matakatifu.
Vitabu vya Agano la kale kwa Wakatoliki toka asili ni 46 wakati Waprotestanti wengi wana vitabu 39 tu.
3. Kanisa Katoliki pekee, lililoanzishwa na Kristo ndilo lenye mamlaka ya kufafanua neno la Mungu na si kila mmoja anavyoona kivyake.
4. Wakati Luteri alisema mtu anaokolewa na imani tu, Mtaguso Mkuu wa Trento, ulifundisha kwamba muumini anaokolewa kwa imani yenye matendo mema.
Imani bila matendo haiwezi kuleta wokovu. Walikosoa mafundisho kwamba baada ya dhambi ya asili binadamu hana utashi tena wa kusema hapana kwa dhambi.
Mtaguso unafundisha kwamba Mungu anampa binadamu uwezo wa kukubali au kukataa dhambi.















