Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyyopita, tuliwaletea jinsi Kanisa lilivyoanzisha Sheria za Kuendesha Kanisa. Leo tunawaletea jinsi Mashirika ya Kitawa yalivyoimarisha mwamko wa Ukristo Duniani.
Sasa endelea…
Kanisa Mlezi wa Elimu:
Katika kipindi hiki, Kanisa lilifufua elimu kuanzia ngazi ya parokia hadi chuo kikuu. Sasa kujua kusoma na kuandika ilikuwa ni fahari na kila mmoja alitamani na kuitafuta elimu.
Wakati huo, ni Kanisa tu ndilo lilikuwa na watu waliokuwa na ujuzi huo. Hivyo, liliongoza katika kuweka utaratibu wa elimu. Pole pole, Wafalme na Viongozi wengine walifuata baada ya kupata elimu toka Kanisani.
Kila Parokia ilikuwa na shule chini ya mwalimu au Katekista ambaye wakati huo huo alikuwa Msakristia, akisimamia usafi na mapambo kanisani, pamoja na kutayarisha mavazi na mambo mengine ya ibada.
Huyu alikuwa vile vile ‘kwayamasta’ akisimamia na kuongoza nyimbo wakati wa ibada, na alifundisha katekisimu kwa watoto wadogo na watu wazima waliojitayarisha kwa sakramenti mbalimbali.
Katika shule ya parokia, Katekista huyu aliwafundisha watoto kusoma na kuandika, pamoja na hesabu za msingi. Kama parokia ilikuwa kubwa, ilikuwa na Makatekista wengi kufuatana na mahitaji.
Wale waliofuzu parokiani na kufaulu, waliendelea na shule ya kati kwenye monasteri na kathedrali (cathedral), iliyokuwa kwenye makao makuu ya Askofu. Kuingia katika Shule ya Kati (Middle School), matajiri walilipia karo, lakini maskini wenye akili, walisomea bure.
Katika Shule ya Kati walijifunza masomo matatu ambayo wakati ule yalikuwa ya msingi (Trivium) yaani Lugha (Grammar), Uandishi wenye mbinu za falsafa (Dialectics), na Usemaji au namna ya kutoa hotuba (Rhetoric).
Wakati huo huo pia waliwafundisha masomo ya sayansi manne (Quadrivium) yakiwa na Hesabu (Arithmetic), Geometry, Uwingu na Nyota (Astronomy), na Muziki.
Shule ya juu kabisa ilikuwa Chuo Kikuu. Chuo Kikuu cha kwanza kilifunguliwa mjini Paris, Ufaransa mwaka 1200 chini ya ulinzi wa Papa Innocent III.
Kuwa chini ya ulinzi wa Papa Innocent, kulikisaidia chuo hiki kisipate kubughudhiwa na watawala wengine, wakiwemo Wafalme, Watawala wadogo pamoja na Maaskofu waliomwogopa Papa.
Somo kuu katika chuo hiki kipya lilikuwa ni Tauhidi (Teolojia/Theology), elimu ya mafundisho ya dini. Baadaye vilianzishwa vyuo vikuu vingine katika kila nchi na kila utawala.
Ilikuwa ni fahari kubwa kuwa na Chuo Kikuu katika mji au jimbo, hivyo Papa, Maaskofu, Wafalme na Watawala wengine walishindana katika kuanzisha Vyuo Vikuu.
Vyuo Vikuu vilikuwa na vitivo vinne; Teolojia, Sheria, Matibabu na Usanii; (Theology, Law, Medicine and Arts). Walikuwa na digri tatu, moja ya kuingilia waliyoiita ‘determinance’ ya pili ilikuwa ya kufuzu, yaani ‘baccalaureatus’ (bachelor), na ya mwisho likuwa ‘Licenciatus’, ambayo ni sawa kama Masters.
Udaktari haikuwa digrii ambayo mtu aliipata kwa kujifunza shuleni, bali kama mtu alifanya kazi nzuri na kujulikana, alitunukiwa hiyo kama heshima.
Sasa, bado kuna udaktari wa heshima, lakini mara nyingine huna la kufanya na kazi ya elimu ambayo mtu amechangia, na mara nyingine bahati mbaya, unanunuliwa.
Namna ya kufundisha chuoni ilikuwa kwa kufundisha (lectio/lectures), kuuliza maswali (questio/questioning) na kubishana (disputatio/disputatioing). Vyuo vikuu hivi vilichangia sana katika kuiinua Ulaya katika nyanja zote. Hata na safari za uvumbuzi ambazo ziliwachukua hadi Asia na Marekani, zilitokana na maendeleo ya elimu toka vyuo hivi.
Elimu ya Teolojia na Falsafa yatukuka:
Wakati huu Elimu ya Dini, au Teolojia, ndiyo ilikuwa elimu mama. Mtakatifu Anselmo aliandika kwamba falsafa (au elimu dunia) ni mjakazi wa Teolojia (au elimu dini). Mfumo wa elimu dini wa wakati huo uliitwa scholasticism.
Ulaya ilikuwa imeunganika katika Kanisa moja, Imani moja na Falsafa moja. Ye yote aliyefundisha kinyume na imani hiyo, alikuwa ni mzushi, na alistahili kufa.
Hata hivyo, ndani ya Imani hiyo palikuwa na uhuru mkubwa sana wa kufikiri, kutafiti na kubuni vitu mbalimbali ili mradi yote ni kwa ajili ya kujenga ufalme wa Mungu, na siyo kinyume chake.
Waalimu waanzilishi wa elimu hii walikuwa Mtakatifu Anselmo (1033-1109, Abelard (1079-1142), na Peter Lombard. Mwalimu mkubwa aliyeitwa daktari wa kimataifa (universal doctor) alikuwa Mtakatifu Alberto Mkuu (1193-1280.
Alberto alikuwa mtaalamu wa elimu dini, falsafa; fizikia na elimu nyingine za dunia. Aliweza kuoanisha elimu yote kwa pamoja na kuielekeza kwa Mungu.
Walimu wakuu wengine walikuwa Mtakatifu Bonaventura Mfansiskani, ambaye alitumia njia ya Mtakatifu Augustino, na mwanafalsafa wa zamani Mgiriki, Plato, kuelezea mambo ya dunia, akianzia kwa Mungu na uumbaji kwenda chini.
Mwingine alikuwa Mdominikani Mtakatifu Tomaso wa Akwino, ambaye alitumia njia ya Mtakatifu Alberto Mkuu kwa kutumia mwanafalsafa wa zamani Mgiriki, Aristotle akielezea mambo yote ya dunia kuanzia matukio ya binadamu ya kila siku, na kuelekea juu kwa Mungu.
Mtakatifu Tomaso vile vile alitunga nyimbo nyingi nzuri zinazoimbwa hadi leo kama ‘Lauda Sion Salvatore, Pange lingua gloriosa, Adorote devote, n.k. Nyimbo hizi zimetafsiriwa sasa katika kila lugha ambako Ukatoliki umefika.
Elimu ya Scholarsticism iliunganisha elimu zote chini ya elimu ya Mungu (Teolojia). Wanateolojia hawa walitumia waalimu mashuhuri wa elimu zote za zamani kutoka kwa Socrates, Plato, Aristotle, Archmides na wengine. Walionyesha wazi kwamba kila tamaduni inaweza kutumia mapokeo ya busara ya babu zao kuelezea Imani katika Mungu na Kristo.
Kufufuka kwa Roho ya Dini:
Maadili ya kidini sasa yalikubaliwa na kila mmoja na kuwa alama ya ustaarabu. Mifano ya kuigwa au mashujaa wa jamii walikuwa ni watakatifu, maaskari watawa (knights) wenye nadhiri za kutetea wanyonge, watu waliokwenda kupigana vita vitakatifu kukomboa Yerusalemu, na watu waliojitoa kwa Mungu kwa namna moja au nyingine.
Haki za watu zililindwa na kutetewa. Hadithi zilizosimuliwa au kutungwa wakati huo zilikuwa ni zile za ushupavu wa kidini. Kwa kifupi, fasheni ya siku hizo ilikuwa kujenga ufalme wa Mungu.
Mashirika ya watawa yalichangia sana katika mwamko huu wa kidini. Mwaka 1000 BK palikuwepo Shirika la Wabenedictini tu, lakini kufika mwaka 1400, palikuwapo Mashirika mengi sana ya Watawa kwa ajili ya matakwa mbalimbali ya wakati huo.
Mashirika haya yote yalikuwa chini ya ulinzi wa Baba Mtakatifu. Shirika lililofungua dimba ni Monasteri ya Kluni.