Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Wakazi wa Bunduki waaswa kutunza hifadhi Hululu

Afisa Misitu Kata ya Bunduki, Protches Elias akiwa katika doria ndani ya Hifadhi ya Hululu mkoani Morogoro. Afisa Misitu Kata ya Bunduki, Protches Elias akiwa katika doria ndani ya Hifadhi ya Hululu mkoani Morogoro.

MOROGORO

Na Winfrida Kobelo-SJMC

Wakazi wanaoishi karibu na Hifadhi ya Hululu iliyopo Kata ya Bunduki, mkoani Morogoro wametakiwa  kuitunza hifadhi hiyo.
Kauli hiyo imekuja wakati huu Taifa linapoendelea na harakati za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ambayo yamezidi kuwa tishio duniani kote.
Wakizungumza na gazeti  Tumaini Letu hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa mazingira wa kata hiyo walisema kuwa kwa sasa wanatumia njia mbalimbali kudhibiti uharibifu wa hifadhi hiyo, ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara.
Afisa Misitu wa Kata hiyo, Protches Elias alisema kwamba wamekuwa wakitoa elimu kwa wanakijiji, ili wahakikishe mazingira yanatunzwa, ikiwemo kutokuchoma moto katika misitu iliyomo ndani ya vijiji hivyo.
“Tumekuwa tukitoa elimu kwa vijiji na vitongoji kuhusiana na majanga ya moto pamoja na uanzishwaji wa vitalu vya miti, na upandaji miti. Pia tunafanya doria za mara kwa mara ili kukabiliana na vitendo vya uharibifu kama vile ukataji miti, kilimo na upitishwaji wa mifugo ndani ya hifadhi,” alisema Afisa Misitu huyo, na kuongeza,
“Suala lingine ni ulinzi na uimarishaji wa mipaka ya hifadhi kwa kufyeka na kusafisha mipaka ili miti iliyopo mpakani ikue vizuri na hivyo kuzuia majanga ya moto ambayo yanaweza kusababishwa na mashamba ya wenyeji yaliyo jirani.”
Akizungumzia changamoto wanazokumbana nazo katika kuitunza hifadhi hiyo, Afisa Misitu huyo alisema kuwa changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa watumishi, na baadhi ya wananchi kufanya shughuli za kilimo katika maeneo ya pembezoni mwa hifadhi hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Mazingira katika Kijiji cha Vinile kilichopo karibu na hifadhi hiyo ya Hululu, Paulo Joseph alisema kuwa wananchi ndio watunzaji namba moja wa hifadhi kutokana na kamati mbalimbali za mazingira ambazo zimeundwa kwa ajili ya kusimamia misitu na kupanda miti, kwani misitu ndiyo chanzo cha upatikanaji wa maji.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo aliwaasa wananchi kuendelea kutunza na kuyathamini mazingira kwa kuachana na tabia za kukata miti, kuchoma moto misitu, pamoja na kuharibu vyanzo vya maji, ili kuepuka madhara yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Veronica Mwenda, mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Mazingira katika Kata ya Bunduki, alieleza kuwa bado wanakumbana na changamoto za matukio ya uharibifu wa misitu, kama vile ukataji hovyo miti.
Naye mkazi wa Kijiji cha Maguruwe kilichopo Kata ya Bunduki, Josephina Christopher, alisema kuwa wameunda baadhi ya vikundi vya upandaji miti katika vitalu kwa ajili ya kutokomeza uhaba wa miti katika misitu hiyo.
“Kwa mfano, pale kijijini kwetu tumekuwa na baadhi ya vikundi mbalimbali mahsusi kwa kupanda miti, na hii ni kwa sababu tunaipenda hifadhi ya Hululu, maana ile ni hazina ya asili tunayojivunia,” alisema Josephina.
Aidha, hifadhi ya Hululu kwa jina lingine hujulikana kama Maporomoko ya Maji ya Hululu, na yana urefu wa sentimita 80 kutoka yanapotoka hadi yanapotiririka, yaliyopo ndani ya msitu wa hifadhi ya mazingira asilia ya Uluguru.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.