RUKWA
Na Lusungu Helela
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu, amesema kuwa Serikali imepanga kutangaza jumla ya ajira mpya 37, 616, huku ajira za kada ya Ualimu, Afya na kada nyinginezo, ikiwemo kada ya Uhasibu na Ugavi, zikiwa tayari zinaendelea kutangazwa, lengo likiwa ni kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi nchini.
Sangu alisema hayo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji vya Kitete, Laela, Kamsamba na Kavifuti vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu alipouteliwa kushika wadhifa huo.
Akizungumzia nafasi za ajira ya Ualimu ambazo tayari zimeshatangazwa na Sekretarieti ya Ajira kwenye ngazi ya mikoa kulingana na mahitaji ya mkoa husika,. Sangu alisema kuwa utaratibu wa kuwapata waalimu kwa mwaka huu umeanza kuwa wa tofauti ukilinganisha na ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.
Alifafanua kuwa usaili huo umeanza kufanyika kwa kada ya Ualimu kwa sababu nafasi za ajira za Ualimu ni chache, ukilinganisha na idadi ya walimu wa shule ya msingi na sekondari waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini, ambapo zaidi ya waalimu 100,000 wapo mitaani wakiwa hawana ajira.
Alisema kuwa Serikali imekuja na uamuzi huo ili kuchagiza dhana ya ushindani kwa lengo la kuhakikisha kila mwenye sifa stahiki, anapata ajira katika mazingira aliyopo pasipo kulazimika kusafiri kwenda Dodoma au Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya usaili.
Kufuatia hatua hiyo. Sangu alitoa wito kwa vijana waliohitimu vyuo mbalimbali hapa nchini kuchangamkia nafasi hizo za ajira, huku akiwataka wajiandae ipasavyo kwa ajili ya usaili huo, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kada hiyo ya Ualimu kufanya usaili
Alitumia fursa hiyo kuwatoa wasiwasi wote walioomba nafasi hizo za Ualimu, huku akiwahakikishia kuwa Ofisi yake yenye dhamana ya kusimamia masuala ya ajira nchini, imejizatiti kuhakikisha mchakato huo wa kuwapata waalimu wenye sifa stahiki utakuwa huru na wa haki.