Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Vijana wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli, Bunju Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, walioimarishwa kwa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara wakiwa kanisani wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti hiyo hivi karibuni.

Wanachama wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Misa Takatifu ya Sherehe ya Somo wao, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Manzese jimboni humo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, akimpongeza Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Ukardinali wake, wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu akisalimiana na kijana James Peter, mwamini wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, jimboni humo, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara. Kulia ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Dominic Somola.

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam akiwasha mshumaa wa Jubilei yake ya Miaka 25 ya Ukardinali wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei hiyo iliyokwenda sanjari miaka 52 ya Upadri wake na miaka 40 ya Uaskofu wake, iliyoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jimboni humo. (Picha na Yohana Kasosi)

Dar es Salaam

Na Bruno Bomola

Wakati Mwadhama Polycarp Joseph Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Ukardinali, sanjari na Miaka 52 ya Upadri wake, amekemea vitendo vya ushoga, akidai vikiendelea, dunia itamalizika.
Adhimisho la Jubilei hiyo pia limeambatana na kumbukizi ya Miaka 39 ya Uaskofu, tangu alipowekwa wakfu Januari 6, mwaka 1984 na Mtakatifu Yohane Paulo II (Papa-1978-2005), Mjini Roma, Italia.
Itakumbukwa kwamba Kardinali Pengo aliyezaliwa Agosti 5 mwaka 1944 katika Kijiji cha Mwazye, mkoani Rukwa, aliwahi kuwa Katibu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, kwa miaka miwili kuanzia Juni 1971 hadi 1973.
Akizungumza na Tumaini Media katika kusheherekea Jubilee hiyo, Kardinali Pengo alisema kuwa kwa nini Roma kuna Makardinali wengi kuliko katika Nchi nyingine, ni kwa sababu Roma ndiyo Makao Makuu ya Baba Mtakatifu, na hivyo inafanya kuwe na wasaidizi wengi wa karibu.
“Kazi kubwa ya Kardinali ni kumshauri Baba Mtakatifu, na ndiyo maana Roma wako wengi, ili wawe karibu naye, licha ya wengine kutawanyika katika nchi mbalimbali.
Agano lake na Mungu limetimia
Aidha, Kardinali Pengo alisema kwamba kuhudumu kwake kwa miaka 25 kama Kardinali, siyo kitu cha kawaida, kwa sababu mara nyingi Makardinali wanachaguliwa wakiwa na umri mkubwa, hali inayosababisha wasiishi miaka 25 baada ya hapo.
“Namshukuru Mungu kwa zawadi hii, kwani wanaofahamu historia yangu kwa miaka ya hivi karibuni, wakati wowote nilikuwa tayari kwenda kwa Mwenyezi Mungu, lakini mwenyewe alitaka niwepo hadi sasa,” alisema Kardinali Pengo.
Alibainisha pia kuwa katika jambo la kufurahisha ndoto aliyoota imetimia, kwani alitamani kabla Mungu hajamchukua, ashuhudie Jimbo Kuu la Dar es Salaam liwe limefikisha Parokia 100, na sasa Jimbo hilo lina Parokia 150 na Parokia Teule zinazoendelea vizuri.
“Nilipostaafu zilikuwa Parokia 137 na bado zimeongezeka, na kwa sasa tutafika 200. Ni baraka kwamba Mungu amesikiliza ombi langu, na nitoe moyo wa shukrani kwa waamini wa Dar es Salaam kwa sababu sasa hatutegemei tena wafadhili kutoka nje, kwani wanajikaza kufanya kazi hiyo waamini wenyewe,” aliongeza kusema Kardinali Pengo katika mahojiano maalumu na gazeti Tumaini Letu.
Alisema pia kuwa wakati anashika Madaraka ya kuliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kulikuwa na Parokia 20 tu, hivyo hakutegemea misaada kutoka kwa wafadhili, na ndiyo maana amefikia hapo.
Ajivunia Umisionari ulivyoleta Padri Mzawa Mafia
Akizungumzia kuhusu Shemasi mzawa kutoka Parokia ya Mafia, mkoani Pwani, anayetarajia kupata Daraja Takatifu la Upadri Julai 7 mwaka huu, Kardinali Pengo alisema kuwa hiyo ni ishara ya baraka kutoka kwa Mungu, kwa sababu ni kitu ambacho watu walidhani hakiwezekani Mafia kutoa Mapadri kutokana na asili yake.
Kardinali Pengo alisema kuwa, “Hii ni mbegu na matunda ya mwanzo kabisa ya safari ya Umisionari kule Mafia. Natamani siku anakwenda kusherehekea Misa yake ya kwanza, Mungu akinipa uhai, na mimi niwepo kama nitapangiwa na Askofu Mkuu.”
Kuhusu Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu, Kardinali Pengo, alisema kuwa binafsi ana mapenzi na watoto, kwani ni kitu kilicho moyoni mwake, kwa sababu ni rahisi kuwafundisha watoto na kuelewa kwa haraka kuliko watu wazima.
Akemea Ushoga, atoa angalizo dunia kumalizika
Aidha, kuhusu vitendo vya kikatili vinavyoendelea nchini, Kardinali Pengo alisema kwamba wanadamu wameingia kwenye matatizo hayo kwa sababu wamemsahau Mungu, hivyo akiwataka Watanzania kuheshimu misingi iliyowekwa na Mungu, ili kuepukana na majanga hayo.
Kwa mujibu wa Kardinali Pengo, ni vizuri kutafakari namna dhambi ya kwanza ilivyoingia duniani kwa mwanadamu, kwa sababu ya kukaidi agizo la Mungu kwa kula tunda walilozuiliwa na Mwenyezi, kwani kukaidi maagizo ya Mungu, ni kusambaratika kwa watu.
“Kama wanadamu wote tungesema tuishi tu wanaume, tuishi peke yetu na wanawake waishi peke yao, tumechoka na makelele na shida za ndoa, mbona tungejimaliza, na watu bado wanapiga kelele ni uhuru wangu niweze kukaa na mwanaume mwenzangu halafu iwe nini tunapaswa kutambua Mwenyezi Mungu yupo,” alisisitiza Kardinali Pengo.
Alisema kuwa kama wanadamu wanataka kuishi, yawapasa kuziheshimu amri za Mungu, kwa amani na utulivu, kwani kutenda kinyume chake ni kujimaliza wenyewe na kupelekea kupunguza umri wa kuishi.
Ashangaa Mungu alivyomwokoa hatarini
Akieleza namna ambavyo kumtumikia Mungu kumemshangaza, ni baada ya yeye binafsi kukata tamaa na madakatari wakidhani sasa muda wake wa kuishi duniani umekwisha, lakini mpaka sasa Mungu bado amemtunza, na wengi wamekuwa wakishangazwa na hali hiyo akiwa na afya tele.
“Tumwachie Mwenyezi atuelekeze kule anapotaka kwa kila mmoja wetu, na tutekeleze yale yapendezayo machoni pake, hii ndiyo zawadi kubwa na shukrani kwa Mungu,”aliongeza kusema Kardinali Pengo.
Katika kutekeleza kazi ya uinjilishaji, Kardinali Pengo aliwataka waamini na Watanzania kwa ujumla kuendelea kiwezesha Kituo cha Tumaini Media ili kiweze kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa kwa Kanisa kwa ujumla.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waamini na Wanachama wa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, wametakiwa kuwa na moyo wa kutubu wanapokosea, na pia kusamehe pale wanapokosewa, kwani huo ndio usafi wa ndani wa mwanadamu.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Padri Mary Maximus wa Shirika la Watumishi wa Upendo, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Katatifu ya Hija kwa Wanachama wa Chama cha Kitume cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, iliyofanyika katika Kituo cha Hija, Pugu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
“Katika maisha yetu ya kila siku, tujitahidi sana kuwa na moyo wa kutubu pale tunapokosea, na pia tusamehe pale tunapokosewa, kwa sababu huo ndio usafi wa ndani wa mwanadamu,” alisema Padri Maximus.
Alisema pia kuwa Moyo Mtakatifu wa Yesu na Moyo Safi wa Mama Bikira Maria, yote husaidia kuleta upendo katika maisha ya wanadamu, kwa kuwa mioyo hiyo ina huruma kwa Ulimwengu.
Akieleza sababu ya kuadhimisha mioyo hiyo miwili kwa wakati mmoja, Padri Maximus alisema kuwa Moyo Mtakatifu wa Yesu ulichukua upendo kutoka kwa Moyo Safi wa Mama Bikira Maria, hivyo haiwezi kutenganishwa.
Aliwataka Wakristo kuepuka kuwa na chuki katika maisha yao, badala yake waishi katika usafi wa ndani ili waweze kupokea baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Padri Maximus aliongeza kuwa ndoa nyingi huvunjika kutokana na kukosa usafi wa ndani, na uaminifu kutoka kwa wanandoa hao.
Padri huyo aliwasisitiza Wakristo kuepuka kukimbilia kwa waganga wa kienyeji wanapohitaji msaada, bali wamkimbilie Mungu pekee, kwani yeye ndiye anayeweza kuwasaidia.
Aliongeza kusema kuwa hata wanapopokea matusi na changamoto mbalimbali katika maisha yao, wanatakiwa kuyapokea, na kisha kuwa wanyenyekevu, wakiiga mfano wa Mama Bikira Maria, kwani yeye ni mnyenyekevu na asiye na hasira.
Padri Maximus alitumia nafasi hiyo kuwasihi Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu kuishi maisha ya huruma na upendo, akisema kuwa huo ni utume wao katika Kanisa.
Alisema kuwa ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kila kitu kinapatikana, hivyo waamini wanatakiwa kuitumia fursa hiyo adhimu kukuza utume wao kupitia chama hicho.

Dar es Salaam

Na Israel Mapunda

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeishauri Serikali kutunga Sheria ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit Agency: DART), ili kupeleka huduma hiyo katika majiji yote nchini.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Denis Londo alisema hayo wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kutembelea na kukagua ujenzi wa barabara ya mabasi ya haraka kutoka Gerezeni Kariakoo hadi Gongolamboto.
Londo alisema kuwa kuna haja kwa Serikali kuandaa maeneo ili kupunguza gharama ya fidia kutokana na miradi mingi ikifanyika na kuwa na gharama kubwa kwa sababu ya ulipaji fidia.
Alisema pia kuwa mitambo ya wakandarasi inapoisha, serikali inatakiwa kuichukua mitambo hiyo na kuendelea kutumia katika miradi mingine, na siyo kuitelekeza au kuiuza kama vyuma chakavu.
Wabunge hao walisema kwamba katika kuweka miundombinu ya miradi ya barabara, kuwe na ushirikiano wa kuandaa na kutenga maeneo mapema yatakayotumika, ili kukwepa kulipa fidia pindi watakapohitaji kuendeleza miji.
Kamati hiyo imesema pia kwamba kuna haja kwa Serikali kuandaa maeneo ili kupunguza gharama ya fidia kutokana na miradi mingi imekuwa ikifanyika na kuwa na gharama kubwa ambayo inachangiwa na ulipaji fidia.
Naye Waziri Wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Angela Kairuki, alisema kuwa uwepo wa DART umesaidia kwa kiasi kikubwa sekta ya usafirishaji, akiahidi kuandaa rasimu ya Sheria Mahsusi ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka itakayosaidia kutatua vikwazo katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa DART, Mhandisi Fanuel Karugendo alisema kuwa kuna maelekezo ya kamati wanayafanyia kazi katika utoaji wa huduma bora za usafiri mijini kote nchini.
Alisema kuwa DART imetimiza miaka 15, hivyo wanaendelea na ujenzi wa miundombinu kwa awamu kwa kila maeneo yaliyoanishwa katika jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, ni ujenzi wa awamu ya tatu ambao unahusisha barabara ya Nyerere hadi Gongolamboto yenye urefu wa kilomita 23.6 ambao mradi huo unatekelezwa kwa mgawanyo wa mafungu mawili, ambapo kipande cha kwanza kinafanywa na Mkandarasi kampuni ya Synohydro kutoka China, na kipande cha pili ni kwa upande wa majengo ambapo mapitio ya usanifu yako katika hatua za mwisho, na yanafanywa na kampuni ya UNITEC Civil Consultants Ltd, ya Tanzania.

Dodoma

Na Mwandishi wetu

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amekemea vitendo vya mateso na unyanyasaji kijinsia vinavyofanyika dhidi ya mabiinti wa shule kwa kukeketwa, kuwaajiri kama wafanyakazi wa ndani, na kuwaozesha.
Chongolo alitoa onyo hilo mjini Dodoma baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa katika Shule ya Sekondari Chilonwa, iliyopo wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Alisema kuwa tabia ya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike haivumiliki na haikubaliki, akiitaka Jamii kubadili mtazamo na kuwafichua wote wenye kujihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Katika hatua nyingine, Chongolo alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maji pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI, kuweka mkakati maalum utakaowezesha kujengwa kwa miundombinu ya maji shuleni hapo na maeneo mengine yanayotoa huduma za jamii.
Chongolo alitembelea Wilaya ya Chamwino baada ya kuhitimisha ziara yake katika Wilaya za Kongwa na Mpwapwa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku nane mkoani Dodoma kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Wakati huo huo, Chongolo aliitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), kuwawezesha zaidi wafugaji wadogo ili watoke katika ufugaji wa kawaida, na wafikie daraja la ufugaji wa kibiashara.
Alitoa agizo hilo wakati alipotembelea NARCO Ranchi ya Kongwa Mkaoni Dodoma, katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Akizungumza katika Ranchi hiyo, Chongolo alisema kuwa kuna wafugaji ambao wana mifugo mingi, lakini haiwafaidishi kutokana na kukosa elimu ya ufugaji kibiashara, na hivyo kutumia mazao ya Ng’ombe kama ngozi na Pembe katika matumizi yasiyo na tija kwao.
Aidha, aliagiza kupelekwa mbegu katika maeneo ya malisho ya wakulima wa kawaida ili kulima mazao ya ng’ombe yatakayosaidia katika malisho, hasa katika kipindi cha kiangazi ambacho kuna changamoto ya malisho.
Kwa upende wake, Mkurugenzi wa NARCO Peter Msofe ameiomba Serikali kuwawezesha katika miradi miwili yenye thamani ya Shilingi bilioni 84 yenye lengo la kutoa Elimu kwa Wanawake na Vijana kuhusu ufugaji, pamoja na mradi wa unenepeshaji ng’ombe.
Ranchi hiyo ya Kongwa ina hekta 38,000 ambapo ndani yake kuna mifugo 30000, huku hekta 18,000 wakipewa wawekezaji, wakiwemo wananchi.

Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services Agency: TFS) umesema kwamba utaendelea kuhamasisha Watanzania kujikita katika ufugaji nyuki kwa kuzingatia maelekezo yote muhimu, na kuwa na vifungashio vyenye ubora unaokubalika.
Hayo yalisemwa na Ofisa Ufugaji Nyuki, Masoko na Leseni wa TFS, Theresia Kamote, wakati wa Maadhimisho ya Barcode Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.