SIMANJIRO
Na Mwandishi wetu
Wachimbaji wa madini ya Green Garnet eneo la Lemshuku, Kata ya Komolo Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wamelalamikia kwa Waziri wa Madini, Anthony Mavunde juu ya changamoto ya ukosefu wa maji, nishati ya umeme na kuwa na ubovu wa barabara.
Mmoja wa wachimbaji madini ya Green Garnet, Mkurugenzi wa Kampuni ya Chusa Mining Ltd, Joseph Mwakipesile alisema hayo wakati akizungumza na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde baada ya kutembelea machimbo ya Lemshuku.
Mwakipesile alisema kuwa huduma ya maji ni changamoto kubwa kwenye machimbo ya Lemshuku, na hakuna nishati ya umeme, hivyo kushindwa kufanya uchimbaji kwa uhakika.
“Maji yanafuatwa umbali wa kilomita 17 kutoka kijiji cha Komolo hadi hapa machimboni, na tulikuwa na kisima cha maji, ila hivi sasa tuna maji tunafuata mbali, na pia barabara ni mbovu,” alisema Mwakipesile.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini (MAREMA), Tawi la Lemshuku, Swalehe Abdalah aliiomba Serikali kufanikisha utatuzi wa changamoto hizo ili waweze kufanya shughuli za uchimbaji kwa uhakika.
“Tunakushukuru Waziri Mavunde kwa kufika Lemshuku na kuona mazingira ya hapa Lemshuku, tunaomba serikali imalize vikwazo tulivyonavyo ili tufanye kazi vyema,” alisema Swalehe.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Mavunde alisema atakutana na Mawaziri husika ili kuhakikisha changamoto hizo zinafanyiwa kazi kuwawezesha wachimbaji hao waweze kufanya kazi zao ipasavyo, na Serikali iongeze mapato.
Waziri Mavunde alisema miundombinu ikiboreshwa na changamoto zikipatiwa ufumbuzi, Watanzania hao watatajirika kwa kupata fedha nyingi, na serikali itaongeza mapato kupitia kodi.
Hata hivyo, ili kumaliza changamoto ya ukosefu wa huduma ya afya, ameendesha harambee ya ghafla ya ujenzi wa zahanati na kupatikana Sh23 milioni matofali 3,000 na mifuko 185 ya saruji
Aliuagiza uongozi wa mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Simanjiro, kuhakikisha pampu iliyozama kisima cha maji Lembole inatolewa ili wachimbaji wapate huduma wakati wakisubiri mradi mkubwa wa maji.
Akizungumza kuhusu mawasiliano alisema kwamba atazungumza na waziri husika ili mnara wa simu ufungwe kwenye machimbo hayo na hivyo mawasiliano yapatikane.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Lulandala alisema kuwa hii ni mara ya kwanza Waziri wa madini kufika kwenye machimbo ya Lemshuku, hivyo Waziri Mavunde anapaswa kupongezwa.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini nchini, Femata John Bina alisema Waziri Mavunde ni kiongozi wa pori kwa pori asiyekaa ofisini ndiyo sababu amefika Lemshuku huku Mwenyekiti wa chama cha mabroka Tanzania (Chamata) Jeremiah Kituyo amewaasa wanunuzi wa madini kukata leseni ili waweze kuwa huru na biashara yao.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka naye alisema wachimbaji hao wa Lemshuku wakitatuliwa changamoto zao watanufaika ikiwemo wachekechaji.