MTWARA
Na Ibrahim Munanka – SJMC
Maaskofu wa Makanisa ya Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki na Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Lindi –Masasi wamesema kuwa kazi ya Uinjilishaji katika maeneo hayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa Wachungaji na rasilimali fedha.
Wakizungumza na gazeti Tumaini Letu katika mahojiano maalumu yaliyofanyika mkoani Mtwara hivi karibuni, Viongozi hao wa Dini waliyoko katika Mikoa ya Lindi na Mtwara, akiwemo Askofu Yeriko Ngwema wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki (Mtwara na Lindi), na Askofu Dk. James Almas wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Masasi, waliwataka Wakristo waishio mijini kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za uinjilishaji katika maeneo ya misioni, ambako bado kuna changamoto kubwa za kimisionari na kiroho.
Wachungaji bado tatizo katika Uinjlishaji:
Kwa upande wake, Askofu Yeriko Ngwema alisema kuwa wanakabiliwa na uhaba wa Wachungaji na changamoto za kifedha ambazo zinakwamisha mipango ya maendeleo ya Kanisa katika maeneo hayo.
Alifafanua kuwa eneo hilo lina Makanisa 15 pekee na Wachungaji ni wachache kiasi kwamba mmoja analazimika kusafiri kutoka kituo kimoja cha kazi hadi kingine kuendesha ibada kwa waamini.
“Wakati mwingine, Mchungaji mmoja anaweza kuendesha ibada katika vituo vitatu tofauti kwa siku moja,” alisema Askofu Ngwema.
Aliongeza kuwa historia ya Ukoloni na Dini zilizotangulia katika maeneo hayo zilileta ugumu kwa watu kupokea mafundisho mapya ya Kikristo.
Kwa upenda wake, Dean Geofrey John Mposola, Msaidizi wa Askofu Ngwema, alisema kwamba uinjilishaji katika vijiji ni muhimu zaidi.
Alieleza kuwa Wakristo mijini wanapaswa kuiombea misioni ili kuwasaidia wale wanaopinga Injili, ili waipokee.
“Huku vijijini kuna utajiri mkubwa wa watu ambao hawajawahi kuipokea Injili, ni jukumu letu kufika huko,” alisema Dean Mposola.
Mchungaji ahudumia makanisa mengi:
Naye Askofu Dk. James Almas wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Masasi, alisema kuwa changamoto zinazolikabili kanisa lake kwenye maeneno hayo, linajumuisha eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 68,000.
Askofu Almas alisema kuwa licha ya juhudi za kuhubiri Injili kupitia mikutano ya nje na semina za ndani, changamoto za kiuchumi zimeathiri maendeleo ya Kanisa hilo.
“Uchumi wa eneo hili ni mgumu kutokana na hali ya hewa isiyotabirika, mvua zinaponyesha sana au kutoponyesha kabisa, mazao yanaharibika, na hii inaathiri uwezo wetu wa kuwatunza Wachungaji,” alisema Askofu Almas na kuongeza,
“Kwa sasa, matunzo ya wachungaji yamekuwa magumu sana, hali ambayo inawafanya wengi kushindwa kumudu mahitaji yao ya kimsingi….
“Licha ya changamoto hizo, Dayosisi ya Masasi imepiga hatua katika uinjilishaji, ambapo mwaka 2023, Idara ya Wanawake ilieneza Injili vijijini, na watu wanane kutoka madhehebu mengine ya dini walibatizwa na kuwa Wakristo.
Semina zasaidia kueneza Injili Vijijini:
Askofu Almas alisema kuwa jitihada hizo ni matokeo ya juhudi kubwa za semina za ndani kwa Waamini na mikutano ya Injili.
Askofu Almas alibainisha pia kuwa malengo makuu ya dayosisi ni kuongeza watumishi wa Injili, hasa wanawake na vijana, pamoja na kujitegemea kiuchumi.
Alieleza kuwa wameanza kuwaandaa wanawake wawili kwa ajili ya kupata Diploma ya Theolojia, na wengine 12 wakiwa na Vyeti kutoka vyuo mbalimbali kama Bunda Bible College na Nairobi Salvation Army.
Hata hivyo, changamoto ya ukosefu wa wataalamu wa ujenzi imekuwa kikwazo kikubwa, kwani Kanisa linajitahidi kukamilisha ujenzi wa makanisa makubwa 72, lakini hakuna watu wenye ujuzi wa kuyajenga mpaka kufikia hatua ya kupaua.
“Tunawaomba Wakristo wenye ujuzi mbalimbali kujitolea kusaidia katika kazi hii kwa ajili ya ufalme wa Mungu,” alisema Askofu Almasi.
Wakristo wanapaswa kukumbuka agizo kuu la Bwana Yesu Kristo, lililopo katika Injili ya Mathayo, 28:19, linalowataka kwenda na kuwafanya mataifa yote kuwa wanafunzi wa Bwana Yesu Kristo kwa mafundisho na kwa kuwabatiza. Wito huu unawataka kutoka mahali walipo na kuwaendea watu kwa mali na vipawa, pamoja na nguvu.