DAR ES SALAAM
Na John Kimweri
Imeelezwa kuwa kiburi cha elimu ni sababu mojawapo inayowafanya watu kuacha kumwamini Mungu, na kutegemea utashi wao na mali walizonazo, kama jawabu katika maisha.
Kauli hiyo ilitolewa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, wakati akitoa homilia yake kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 125, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Martin wa Porres, Mwananyamala.
Askofu Musomba (pichani) alisema kuwa kiburi ni dhambi na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani, akiwataka waamini kuhakikisha licha ya elimu walizonazo, lakini watambue uwepo wa Mungu katika maisha yao kwa sababu bila yeye, hawawezi kufanya kitu chochote.
“Kiburi cha usomi kinaweza kusababisha mtu akaona kuwa hakuna Mungu, na eti anajiweza yeye mwenyewe bila ya msaada wa Mungu, kiburi ni dhambi kubwa sana na ndiyo chanzo cha migogoro mingi duniani,” alisema Askofu Musomba.
Askofu Musomba, alieleza kuwa kiburi kingine ni cha maendeleo na kiroho, akiwaonya waamini wanaojiona kuwa wamekamilika kuliko wengine kuacha kufanya hivyo.
Aliwakumbusha wazazi kuhakikisha kuwa wanapowarithisha watoto wao mali na vitu vingine vya thamani, wasisahau kuwarithisha imani, kwani hilo ni jambo lisiloharibika wala kuchakaa.
Aidha, aliwataka waimarishwa kutambua kwamba wanapopokea Sakramenti hiyo, Roho Mtakatifu anaingia ndani mwao na kuwafanya kuwa wapya katika kila jambo, huku akiwaasa wazazi nao kuwa na desturi ya kusali pamoja, na pia kusoma Neno la Mungu na watoto wao.
Alisema kwamba Roho Mtakatifu ni nyenzo ya utume ya kuwasaidia waamini kuinjilisha hapa duniani, na kudai kuwa utume wa kweli unatakiwa kuanzia kwenye ngazi ya familia.
Kwa mujibu wa Askofu Musomba, utii unamfanya mtu akabidhi utashi na kuwa mtii kwa Mungu mwenyewe, na kuongeza kwamba pia utii huendana na usikivu, ambapo mwisho wake huleta unyenyekevu kwa mtu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia hiyo, Jeremia Mchomvu, alisema kuwa Parokia hiyo ina jumla ya waamini 6757, kutokana na sensa iliyofanyika Januari mwaka 2020.
Alisema kuwa Parokia kwa sasa ina mpango wa kununua nyumba mbili, ili kupanua eneo la kanisa.