Na Dkt. Nkwabi Sabasaba
ILIPOISHIA
MAISHA YA KAZI YA NDANI:
Hii ni nguvu yako ya ndani kama vile hamasa; hisia; imani; na unajisikiaje furaha yako. Maisha ya kazi ya ndani yanaweza kukufanya uifanye kazi kwa kiwango cha juu au cha chini, iwapo unafanya kazi ungali umevunjika moyo.
Nguvu ya kusonga mbele huchochewa na maisha ya kazi ya ndani kwa mujibu wa Dr. James Watts. Maisha ya kazi ya ndani yanaweza kuchochea kanuni ya maendeleo ifanye kazi pia.
Endelea...
Mabadiliko madogo madogo yanaweza kuchochea maisha ya kazi ya ndani. Mfano, mtaji wa sh. 5,000 au elfu kumi, utahusisha bidhaa ndogo ndogo ambazo kila mtu ana uwezo wa kuvinunua, na kwa kadri watu wanaponunua wengi kwa wakati mmoja, ndipo hamasa yako ya kuendelea kufanya biashara hiyo, inavyokua. Unapoona watu wengi wananunua bidhaa yako kwa wingi, japo ni ndogo, maisha ya kazi ya ndani yanaoongezeka. Unajiona umefanya jambo.
Mnamo mwaka 1983, Steve Jobs alikuwa akijaribu kumshawishi John Sculley aache kazi ya muhimu sana kwenye kampuni ya Pepsico ili awe Mkurugenzi Mkuu wa Apple. Jobs anaripotiwa kumwambia, “Je, unapenda kuyatumia maisha yako yote yaliyobaki kuuza maji yaliyotiwa sukari, ama unataka nafasi ya kuubadili ulimwengu?”. Kauli hii ya Jobs inataka kutuambia kwamba kuna kazi zenye maana. Kazi yenye maana ni ile ambayo italeta mabadiliko kwa watu, na itatutia moyo kuona inavyoleta mabadiliko.
AINA SABA ZA IMANI-MAZOEA ZISIZO NA FAIDA, NA JINSI YA KUZITOA:
Mambo yanayotuzuia kusonga mbele ni imani zetu binafsi. Imani hizi zimezaliwa kutokana na sababu kwamba jambo hili tuna uzoefu nalo, au tumekuwa tukiambiwa, au kufundishwa. Watu waliofanikiwa ni wale walioamuru kukana imani hizo na kufanya kilicho mbele yao.
Mfano:
- Kwa kuwa kitabu pekee ambacho hakina makwazo ni quran au biblia, maana yake ni kwamba kusoma vitabu vingine, nitakwazika.
- Kuchagua tovuti (website) na kuzitembelea, zingine huna mapenzi nazo.
- Kuamini kuwa watu wafupi ni wabishi, kwa hiyo hupendi ushirika nao, n.k.
Ebu sasa tutazame aina za imani mazoea, ambazo hazina faida, na namna ya kuondokana nazo:
1. KUTEGEMEA KITU KUTOKA KWA WENGINE, AU KUTOKA MAISHANI:
Haimaanishi kwamba uache kushirikiana na wengine ili kupata mchango wao. Ukweli, wewe ndiyo kichocheo kikuu cha mabadiliko ya ulimwengu wako. Ijulikane kwamba mchango wa msaada wa watu kwako, ni kwa sababu ya juhudi zako. Watu hujitokeza zaidi kukusaidia kama umewakaribisha wakusaidie, au iwapo wameona juhudi zako. Pia, kitendo cha kuwakaribisha wakusaidie, hiyo ni juhudi yako. Juhudi yoyote huzaa matunda. Msemo ‘mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe’ , una maana kwamba wewe ndiye mtaji. Mtaji hauko pale wala huko, ila ni wewe mwenyewe. Jipe moyo mwenyewe, moyo ukiwa na hamasa, utafanikiwa.
Franklin D. Roosevelt alisema, ”Kipingamizi pekee cha mafanikio yetu ya kesho, ni ile hofu tuliyo nayo leo.”
Kila mtu kabla hajaanza kutenda, mafanikio yake ni 100%. Anapoanza kutenda, mafanikio yanaanza kupungua hadi 90% na kushuka chini, lakini hutegemea kila hatua ya utendaji wako unaambatanisha hofu kiasi gani.
2. KUTEGEMEA KUWAZA TU, NA KUPUUZA SAUTI YA NDANI:
Watu wengi hawatilii maanani hisia na sauti za ndani au kutoziamini. Kuna aina mbili za kuwaza. Kuwaza kwa akili ya ufahamu. Hii huwaza taratibu sana na inatumia nguvu nyingi. Na kuwaza kwa kutumia akili ya kina, hii huwaza kwa haraka sana. Akili ya fahamu hukuletea majibu yaliyofikiriwa kwa makini kisha, kuamriwa. Majibu hayo yapo katika mpangilio mahsusi, wakati akili ya kina hutumia imani, na majibu yake ni ya haraka.
Mfano, kuna familia moja ilikuwa inauza nyumba. Jirani yao akasema ataleta mteja. Siku moja kweli jirani akaleta mteja, familia ikakubaliana na mteja kuwa nyumba iuzwe kwa shilingi milioni 70.
Itaendelea wiki ijayo.