DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu
Diwani wa Kata ya Makurumla Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Mkoani Dar es Salaam, Bakari Kimwanga, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha wanakuwa na utulivu hasa kutokana na taharuki ya utekaji watoto kwenye shule.
Pamoja na hali hiyo, amesema kuwa mpaka sasa ndani ya Kata ya Makurumla, hakuna tukio la kutekwa kwa mtoto, huku akiweka wazi kuwa ni lazima kila mwana jamii ahakikishe anatoa ulinzi kwa mtoto, hasa wanapokuwa mitaani.
Kauli hiyo aliitoa hivi karibuni alipokuwa akizungumza na wazazi, walezi na waalimu katika shule za Msingi za Mianzini, Karume na Dk. Omari, ambapo juzi ilizuka taharuki ya kutekwa watoto kwenye shule hizo, na kuibua sintofamu kwa wazazi kulazimika kuvamia shule ili kuona usalama wa watoto wao.
“Tangu zilipoibuka taarifa hizi za taharuki Julai 22, 2024 (Jumatatu), tumefuatilia taarifa kwenye shule zetu, vyombo vya ulinzi na usalama, kwa maana ya Jeshi la Polisi, hali iko shwari wazazi wenzangu.
Aidha, aliwataka wazazi kutambua kuwa ni lazima kuweka mkazo kwenye suala la lishe kwa watoto kwa kuhakikisha wanachangia Shilingi 500 ya chakula kama walivyokubaliana kwenye mikutano ya wazazi, jambo ambalo litamsaidia mtoto kupata chakula shuleni badala ya kwenda mitaani wakati wa kipindi cha mapumziko.
Kwa upande wake Afisa Elimu Msingi, Manispaa ya Ubungo, Denis Nyoni aliwataka wazazi kuwa na utulivu kwani hadi kufikia jana hakuna taarifa za watoto kutekwa katika shule kwenye manispaa hiyo.
“Naomba waalimu msisahau wajibu wa kuandika mahudhurio ya watoto kila siku wawapo darasani, na hata wakati wanapomaliza masomo kwa siku, majina yaitwe. Hatua hii ndiyo njia ya kuendelea kudhibiti usalama wa watoto wetu,” amesema Nyoni
Naye Polisi Kata ya Makurumla, Insp Emmanuel Humba, alisema kuwa katika Kata ya Makurumla hali ni shwari, hakuna tukio la utekaji kwa watoto, huku akiwaomba wazazi wawe na utulivu wanapopata taarifa za taharuki.