DAR ES SALAAM
Viongozi wa Halmashauri ya Walei wa Parokia za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wametakiwa kuacha kuingia kwenye mizozo na malumbano na Maparoko, ili kazi ya Mungu isonge mbele.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 34, katika Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mungu – Mbopo Madale, jimboni Dar es Salaam.
“Viongozi mhakikishe mnadumisha mshikamano na Maparoko wenu, kwani kwa kufanya hivyo, kazi ya Mungu itasonga mbele,”alisema Askofu Mchamungu.
Akitoa nasaha kwa Wasimamizi, Askofu Mchamungu alisema kuwa: “Wasimamizi nawaomba sana mshikamane na wazazi au walezi wa vijana hawa kuwalea kiimani, maana wewe umepewa jukumu hili umsaidie mlezi au mzazi kumsimamia huyu kijana…
“Sasa jukumu ni lako, umuongoze ili aweze kuiishi vizuri imani yake ya Ukristo, maana wasimamizi wengi wakimsimamia kijana wakafurahi siku hiyo, basi hana muda naye tena, hamfuatilii wala kuwajulia hali, inakuwa imetoka,” alisema Askofu Mchamungu.
Aliwasisitiza Waimarishwa kutoacha kwenda kusali, kujifuza, pamoja na kushiriki shughuli mbalimbali za Kanisa, kwani wakifanya hivyo, watakuwa vijana wema na wenye nguvu ya Roho Mtakatifu waliyempokea.
Aidha, aliwaasa vijana hao kutodanganywa na manabii wa uongo katika maeneo wanayoishi.
Padri Luwena asimikwa rasmi:
Katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, Askofu Mchamungu alimsimika rasmi Paroko wa Parokia hiyo, Padri Joseph Luwena akiwaomba Waamini kushirikiana naye vizuri katika kazi zake za Kitume.
Aidha, aliwasihi Waamini wa Parokia hiyo kuongeza jitihada juu ya ujezi wa nyumba ya Mapadri, ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati, na Paroko aweze kuishi sehemu bora.
“Hakikisheni Paroko wenu anakaa mahali pazuri, kwa sababu anawahudumia kiroho. Mmpende, mmjali, mthamini, kwa kuwa Paroko huyu mmekabidhiwa na Askofu Mkuu wa Jimbo, kwa hiyo msipomjali, sio vizuri…
Kwa upande wake, Padri Joseph Luwena aliwaomba Waamini wa Parokia hiyo kumpa ushirikiano, ili aweze kufanya kazi kwa amani, akimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuwapatia sakramenti vijana hao.