Morogoro
Na Modest Msangi
Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Augustino – Mzumbe, Jimbo Katoliki la Morogoro, Padri Dk. Romanus Dimoso amewataka Waamini kutafakari maisha yao na kutambua kwamba wao ni Viongozi bora.
Padri Dimoso alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika ya 16 ya Mwaka ‘B’ wa Kanisa iliyoadhimishwa parokiani hapo.
Padri Dimoso ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema kuwa katika familia, kaya, na jamii, Viongozi wameweka kipaumbele kutafuna mali za familia, na kuwaacha watu wakiteseka kwa kukosa huduma za kijamii.
“Ukiona maendeleo katika familia au jamii fulani, ujue kiongozi wao anawajibika vyema, lakini baadhi yao wamekuwa panya wa maendeleo ya watu, baba au mama katika familia anakuwa panya, huwezi kuona maendeleo katika familia au kaya yao,”alisema Padri Dimoso.
Padri Dimoso alisema kuwa Yesu Kristo ni mfano bora wa kuigwa alipowatuma Wafuasi wake waliporudi kutoa ripoti ya kazi waliyotumwa, aliwapongeza na kuwaambia waende mahali pasipo na watu, wakapumzike.
Azungumzia uchaguzi Mkuu
Aliongeza kusema kwamba huu ni mwaka wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, na mwakani ni Uchaguzi Mkuu, hivyo Waamini kama sehemu ya wananchi, wanapaswa kutafakari kwanza kabla ya kuamua wamchague nani.
Alisema kwamba kwa Miaka 60 ya Uhuru, maendeleo yamekuwa ni ya kupapasa, kwani baadhi yao wamekuwa na tabia zisizofaa katika jamii yao.
Padri Dimoso alibainisha kwamba ili kupata viongozi ambao hawatakuwa kama panya, kabla ya kuwachagua, wananchi wanapaswa kutafakari kwanza hali ya changamoto zilizopo katika jamii, na kuona kama anayechaguliwa, anaweza kuzitatua.