DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Baadhi ya Wawakilishi wa Mpango wa Nia Njema wameomba kuwahishwa kupewa kadi zao za bima na kuongezewa hospitali za kwenda kutibiwa wanapopatwa na matatizo ya kiafya, kwani wanazoruhusiwa kwenda ni chache.
Waliyasema hayo wakati wakieleza changamoto zilizojitokeza tangu baada ya Semina Elekezi katika Mkutano wa Kazi wa Wasimamizi wa Mpango wa Nia Njema uliofanyika katika Viwanja vya Kituo cha Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.
Katika changamoto walizozitoa kwenye mkutano huo, waliomba pia kufanyiwa kazi kwa suala la baadhi ya magonjwa kutokutibiwa na kadi za bima hiyo, ili kuweza kumsaidia kila mgonjwa anayekwenda kufuata huduma.
Waliomba elimu na semina mbalimbali ziendelee kutolewa kwa wazee na wajane, ili nao waone kwamba Kanisa limewatambua.
Aidha, baadhi ya Wawakilishi wa mpango huo wa Nia Njema waliomba kupatiwa sare ili kujenga imani ya kusikilizwa pale wanapotoa elimu kwa wenigine.
Waliushauri Uongozi wa mpango huo, kuwaongezea timu ya Wawakilishi, ili kuongeza kasi ya uhamasishaji pamoja na utoaji wa elimu juu ya Nia Njema.
Miongoni mwa changangamoto walizobainisha Wawakilishi hao, ni pamoja na kutokupatiwa huduma kutokana na kutokupokelewa simu kwa wakati pale mtu anapohitaji huduma.
Wakati huo huo pia walipendekeza kutolewa mipaka suala la umri wa kupatiwa huduma hiyo, kwani kila rika lina haki ya kupatiwa matibabu pale mtu anapopatwa na magonjwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ACCLAVIA, Nindiu Mpangile alisema kuwa ili kupunguza baadhi ya changamoto za kupatiwa matibabu, watahakikisha baadhi ya Hospitali za Wilaya ziingie katika mpango huo.
Nindiu alitumia nafasi hiyo kusema kwamba wao kama ofisi, wanaomba radhi kwa ucheleweshwaji wa kupata kadi, akisema kuwa watajitahidi kuongeza kasi ya utendaji ili watu wapatiwe kadi zao kwa wakati.
Aliongeza kuwa wakati mwingine wanawaambia watu wasubiri kwa muda kabla ya kuwapatia kadi hizo, ili kuepusha udanganyifu unaoweza kujitokeza.
Pia, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema kuwa lengo siyo tu kuziingiza Hospitali zote za Kanisa katika mpango huo, bali ni zile tu ambazo zimekidhi vigezo katika suala zima la utoaji wa matibabu.
Alisema kuwa wameandaa utaratibu wa kuwa na vipindi mbalimbali katika vyombo vya habari vya Kanisa, ikiwemo Tumaini Media, ili kuwafanya wengi wawe na ufahamu juu ya mpango huo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa ACCLAVIA, Dk. Anselmi Anselmi alisema kuwa hakuna bima ambayo ni ya lazima, bali wao wapo kwa ajili ya kutoa bima yenye kusaidia watu, hasa wenye kipato cha chini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mpango wa Nia Njema, Emmanuel Tibaijuka aliwasisitiza Wakristo kutambua kwamba mpango wa Nia Njema una faida kubwa kwao, hivyo ni vizuri wakafanya maamuzi ya kujiunga na mpango huo.
Akihitimisha katika Mkutano huo, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu aliwashukuru Wawakilishi kwa kukubali kupokea utume huo, akiwataka kuendelea kufanya kazi bila kukata tamaa.
Askofu Mchamungu aliwasihi Maparoko kutoa nafasi kwa Wawakilishi parokiani, ili waendelee kutoa elimu na uhamasishaji, akiwataka Wakristo kufahamu kwamba huo si utapeli, bali ni mpango wenye manufaa makubwa kwao.