Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kuwa Wachungaji wema ni wale wenye kutenga muda wao kwa ajili ya kuwafahamu kondoo wao kwa majina, ili wasisambaratike.
Hayo yalisemwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu la Upadri kwa Mashemasi saba wa OSA, katika Parokia ya Mtakatifu Ambrosi – Tagaste, jimboni humo.
Aliwataka Mapadri hao wapya kutambua kwamba wanatakiwa kujitosa bila kujibakiza, kwani ndiyo sifa ya uchungaji mwema, kuwakusanya kondoo wanaowachunga.
“Sifa ya uchungaji mwema ni kujitosa bila kujibakiza. Wachungaji wema ni wale wenye kuwafahamu kondoo wao, tena kwa majina, ili wasisambaratike. Mumwombe Mungu awape nguvu ya kuifanya kazi yake ili muwe vyombo vya neema yake,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kila mbatizwa alizawadiwa wito wa kumtambua na kumfuata Kristo, akiwasisitizia Wakristo kuitambua fursa hiyo.
Aliwasihi Wakristo kuthubutu kumkimbilia Mungu, kwani kwa kufanya hivyo, watapata faraja na kusamehewa dhambi zao.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa Mungu ndiye chimbuko la kila jema, na pia ndiye anayetoa kila wito ulio sahihi katika maisha ya mwanadamu.
“Ndugu zangu, Mungu ndiye chimbuko la kila jema, na pia ndiye anayetoa kila wito ulio sahihi. Wapo baadhi ya watu wanaolala na kuamka, kisha kujitangaza kuwa wana wito. Mtu anaamka asubuhi anamwambia mke wake kwamba ‘usiku nimeoteshwa’. Huo siyo wito ulio sahihi, kwani wito ulio sahihi hutoka kwa Mungu Mwenyezi,” Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliongeza kuwa Mungu ni mwenye huruma, ndiyo maana licha ya mapungufu ya wanadamu juu ya dhambi zao, yeye huwahurumia.
Aliwasisitiza Mashamasi hao kuwa wakawe Mapadri wenye kujituma bila kulaza damu, bali watumie kila muda wao kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu.
Aidha, aliwataka pia Wakristo kutambua kwamba Yesu Kristo hashabikii dhambi, bali humwokoa mdhambi na kumzawadia wokovu maishani mwake.
Wakati huo huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa kama Kanisa, wanamshukuru Mungu kwa kupata Mapadri wapya watakaosaidiana nao kufanya utume kwa ajili ya kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Kwa upande wake Padri Laurent Temanya- OSA, mmoja wa waliopokea Daraja hilo Takatifu, alisema kwamba wao kama Mapadri, wanamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Upadri.
Alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kuongoza Adhimisho hilo, huku wakiwashukuru wazazi wao kwa kuwaleta duniani pamoja na kuwaruhusu kuuitikia wito huo.
Waliwashukuru walezi wao katika maeneo yote waliyopita kwa mchango mkubwa katika safari yao hiyo, huku wakiwashukuru pia wote waliowaombea, na kusema kwamba bado wanahitaji sala zao.
Aliwaasa wazazi kuendelea kuziombea familia zao, hasa zenye watoto wanaowiwa kuufuata wito, ili katika shamba la Bwana, watendakazi wawe wengi.