MWANZA
Na Paul Mabuga
Joep Lange [1954 – 2014], raia wa Uholanzi na Mtafiti aliyejikita katika tiba za virusi vya ukimwi, aliwahi kuhoji, iweje karibu kiila mahali katika bara la Afrika unaweza kupata bia ama soda ya baridi bila changamoto, lakini linapokuja suala la usambazaji na upatikanaji wa dawa, linakuwa tatizo la kuzungumzwa kila wakati.
Lange alifariki akiwa miongoni mwa abiria kwenye ndege shirika la ndege la Malaysia iliyoshambuluwa kwa bomu kutoka ardhini Julai 17, 2014, wakati akisafiri kutoka Amsterdam Uholanzi, kwenda Kuala Lumpur, Malaysia, kwenye kongamano la kila mwaka la UKIMWI.
Na huo ndio ukweli, kwamba licha ya juhudi mbali mbali ambazo zimekuwa zikifanyika kwa miradi na mipango tofauti hapa nchini, lakini bado hilo limekuwa changamoto. Mathalani, wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi yasiyoambukiza, hususan kisukari na shinikizo la damu, wanaongezeka kutokana na mitindo yetu ya maisha, huduma zetu zinazidiwa na wingi wa watu, upatikanaji wa dawa kama inavyotakiwa unakuwa changamoto, umbali wa kufuata tiba nao unakuwa aghali, na uzingativu wa muda wa waganga kwa kila mgonjwa nao unakuwa mashakani. Lakini huko Zanzibar, kuna hatua imefikiwa
Mzee Omari Dadi Hamad, mkazi wa Shehia ya Bopwe Wete, Pemba, katika umri wake wa miaka 65, pamoja na kuwa changamoto ya shinikizo la juu la damu, leo hii anaweza kupiga jembe na ardhi ikaitika. Ni katika shamba lake la miwa, ambayo ni mali ghafi katika kiwanda chake kidogo cha sharubati kinachotegemewa na familia yake ya watu tisa. Asingeweza kufanya haya kabla ya mwezi Aprili, mwaka jana.
Mzee Hamad amekuwa akisumbuliwa na shinikizo la juu la damu kwa miaka kumi sasa, hali ambayo hapo awali, kama ilivyo kwake na wenzake wanaosumbuliwa na magonjwa yasiyoambukiza, yaani shinikizo la damu la juu ama la chini la damu, na kisukari, imekuwa kikwazo kama changamoto ya kiafya na hata kiuchumi katika ustawi wao.
“Nilianza kujisikia kuchoka, nikitembea kidogo nachoka sana. Nikifika msikitini nahema, nashindwa kusali na ndipo nikashauriwa na mke wangu, Madhari upo katika hali hiyo nenda hospitali kafanye vipimo. Nikaenda nikapima sukari, nikapima presha na nikapima vingine, nikaambiwa ni presha [shinikizo la juu la damu], na kwa sababu hali haikuwa chronic sana, nikashailiwa kuanza dawa,” anasema Mzee Hamad katika mahojiano kwa ajili ya makala haya.
Anasema kuwa kuambiwa juu ya tatizo hilo, kulimkumbusha juu ya kisa cha marehemu kaka yake ambaye wakati anafanya kazi Kigamboni jijini Dar es salaam, zaidi ya miaka kumi iliyopita, alianguka ghafla na kupoteza na alipopelekwa hospitalini ilibainika kuwa alikuwa na tatizo la shinikizo la juu la damu, na baadaye akapatwa na kiharusi.
“Kuanzia pale nilipopewa majibu kuwa nina presha , nikajua afanaleikh, kumbe na mimi niliishaanza presha na kuwa katika tishio la kuwa katika hali kama hiyo ya kaka yangu. Nikaanza dawa kidogo kidogo, lakini kwa sababu kulikuwa na usumbufu kidogo katika upatikanaji wa dawa. Uende hospitali ukaandkiwe dawa,ukienda dirishani hakuna.unaambiwa ukanunue. Basi ukimeza tembe mbili, unaweza kukaa hata wiki nzima humezi tena,” anasimulia Mzee Hamad.
Kulingana na simulizi ya Mzee Hamad, ukiacha changamoto hiyo ya upatikanaji wa dawa kama inavyotakiwa miongoni mwa wagonjwa wa shinikizo la damu na kisukari, lakini pia wingi wa wagonjwa katika vituo vya huduma uliosababisha yeye na wenzake kuchukua muda mrefu kwenye mistari kabla ya kupata huduma na hata kufuata huduma hizo mbali zaidi.
“Dokta akahangaika, akaniambia wende Makunduchi [hospitali ya wilaya kwa ajili ya rufaa], mmh, wende wapi? Makunduchi sikai, Makunduchi, Upo! Sasa tulivyokwenda kule. Hapana hehee! Swalaa hiyo [Niliondoka alfajiri wakati wa adhana]. Natafuta gari kwa pesa [nauli] mpaka wap:?
Makunduchi! Makunduchi nateremka nenda hotel, hotel [Kula na baadaye napata matibabu] mpaka narudi kwetu saa nane au saa tisa, Upo! Yanakuijia [unaelewa]!” Anasimulia Bibi Nali Kombo, mwenye umri wa miaka zaidi ya 70 na mkazi wa Mtende, Unguja, ikiwa ni uzoefu wake kuhusu matibabu kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Hali hii ya huduma pia ilikuwa ni changamoto hata kwa watoa huduma kama Dk. Fatmah Mohamed Amour, Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya cha Jadida, Pemba, anavyosema, “ licha ya kuwepo wagonjwa wengi lakini pia utunzaji kumbukumbu ulikuwa tatizo kutuwezesha kufuatilia wagonjwa.
Pia, wagonjwa wengine wa kisukari walikuwa wanashindwa kuvumilia kusubiria vipimo, hivyo wanakwenda kula na kutufanya tusipate vipimo sahihi ambavyo vinahitaji sampuli kuchukuliwa kabla ya kula chochote.”
Kutokana na changamoto hizi ambazo zilitokana na ingezeko la wagonjwa wa kisukari na presha, Mraribu Msaidizi wa Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza Zuhura Saleh Amour, anasema Wizara ya Afya Zanzibar kwa ushirikiano na PharmAccess na udhamini wa Sanofi, Aprili 2023, walianzishwa mradi wa huduma kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na maradhi yasiyombukiza katika ngazi ya jamii.
Anasema kwamba chini ya mradi, zahanati zinawasaidia wagonjwa wanaotoka eneo moja kuunda vikundi vya kijamii katika makazi yao na kupata huduma ya matibabu na dawa wanazopelekewa na muuguzi kila mwezi bila kuhitajika kwenda mbali.
Pia kuna wahudumu wa ngazi ya jamii katika kila kikundi ambao wamepata mafunzo ya kuchukua vipimo muhimu kuangalia mwenendo wa afya za wagonjwa kwa karibu na kuwashauri. Vipimo hivi huingizwa katika mfumo wa kidigitali, ambao unamwezesha daktari kufuatilia wagonjwa wote ambao wamepimwa katika siku husika. Pamoja na kuchukua vipimo, wahudumu wa ngazi ya jamii wamepewa mafunzo ya kutoa elimu ya namna bora ya kuishi na magonjwa yasiyoambukiza
“Kwa sasa, tunapata huduma kama inavyotakikana, dawa tunapata, siku ya kliniki, wauguzi wanakuja kwenye jamii yetu. Wahudumu nao wanatupima na kutufuatililia. Sasa tunaweza kufanya hata kazi zetu,’’ anasema Mzee Hamad baada ya kuanza kunufaika na kupitia mradi huo , wakati, Bibi Nali anashuhudia, “Dawa tunapata na maungoni zinaingia, na afya zinatengemaa. Hili begi hili [analioesha], ni la madawa.”
Nyendo Hassan Haji mkazi wa Mtende, Makunduchi na mnufaika wa mradi huu anasema umekuwa na manufaa anasema maana kabla yake walikuwa kama wananyanyasika vile kwani “Ilikuwa usumbufu sana. Unafika kule unakuta watu wametia mabuku yao [daftari za kumbukumbu ya matibabu kwa wagonjwa], ukitaka kuweka lako wanakuambia, wenzako wamewahi, ilikuwa usumbufu mpaka wengine walikuwa wanaona heri wabaki nyumbani wajifie basi!”
Hawa ni miongoni mwa wananchi zaidi ya 800 wanaosumbuliwa na maradhi ya kisukari na sdhinikizo la damu, ambao wapo katika vikundi 25, ambavyo vimefikiwa na huduma chini ya mradi huo, na wanafikiwa kila mwezi katika vikundi vyao vilivyopo mahala wanakoishi na kupatikiwa huduma za dawa na matibabu.
Mganga Mfawidhi katika Kituo cha Jongowe Tumbatu, Dk Tumaini Zaidu anasema kuwa kutokana na mradi huo, hata uhusiano wao na wagonjwa umeimarika, kumbukumbu zimekuwa sawa, kazi imekuwa rahisi, na ufanisi umeongezeka na hata wamepungukiwa na wagonjwa kwa kuwa wengi wanapata huduma katika vikundi vya kijamii katika mitaa yao, na kwamba wanaofika kwao ni wale ambao wanachangamoto za kirufaa. “kwa hawa ambao wanalazimika kuja hapa kliniki, tunapata muda wa kutosha wa kuwasikiliza matatizo yao, mienendo yao ya kimaisha na muda wa kutosha kuwapa elimu ya namna nzuri ya kuishi na magonjwa haya.
Meneja wa Programu wa Pharmaccess Zanzibar, Faiza Abbas, anasema katika kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, kuwa taasisi yao iliona kuna haja ya kuwa na program bunifu, na kwa msaada wa teknolojia, ambao itaondoa matatizo katika utoaji huduma ili kupunguza tatizo la msongamano wa wagonjwa wa maradhi yasiyoambukiza katika vituo vya huduma, lakini pia kuboresha huduma kwa wagonjwa.
Katika moja ya matumizi ya teknolojia, vipimo vya kila mgonjwa kwenye vikundi huchukuliwa na kutumwa kwenye kituo cha mawasiliano ya afya, ambapo madaktari na wataalam wengine huwa na utaratibu wa kufuatilia mienendo ya wagonjwa hao, na kuwatambua wale wenye changamoto na kuwasiliana nao kwa hatua zaidi za kitabibu.
“Mimi mwenyewe binafsi mwanzo sikuwa sanasana na tamaa kama tunaweza kufika hatua hii. Lakini baada ya kwenda kuangalia, sasa nimeona kwa muda mfupi tumepata mafanikio makubwa sana. Baada ya kufanya evaluation tumegundua kuwa mafanikio ni makubwa sana,” anasema Nassor Ahmed Mazrui, Waziri wa Afya, Zanzibar, na kuongeza, ‘’ PharmAccess wametusaidia sana kwa mambo mengi na mafanikio haya ni lazima kuyafikisha katika wilaya zote, na manufaa ya mradi lazima yaendelezwa hata baada ya mfadhili kumaliza muda wake.”
Kwa Mzee Hamad, mafanikio katika mradi huu ni jambo muhimu katika maisha yao, kwani anasema, “Walahi mie nasema Mungu ajalie hawa wenye kuonesha mpango huu. Awape nguvu, awape kila hali uendelee na utanuke zaidi uwafikie wagonjwa wengi zaidi, kwa sababu bado wapo.”