Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Kanisa katika Zambia huru

Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea historia ya kuanza kwa Uinjilishaji nchini Zambia.  Leo tunaendelea na Uinjilishaji nchini humo, hususan Kanisa katika Zambia huru na kuanza kwa uinjilishaji nchini Malawi. Sasa endelea…

Mwaka 1923, Kampuni ya Cecil Rhodes iliachia utawala wake Zimbabwe na Zambia na Nchi hizi zikawekwa moja kwa moja chini ya ulinzi wa Serikali ya Uingereza. Mwaka 1953 Zimbabwe, Zambia na Malawi ziliunganishwa katika ‘Muungano wa Rhodesia na Nyasaland’.

Muungano huu ulipingwa sana na Waafrika wa Zambia na Malawi. Upinzani ulizidi sana mwaka 1960 na 1961 ukiongozwa na Harry Mwaanga Nkumbula wa African National Congress (ANC), na baadaye Kenneth Kaunda aambaye aliunda chama chake cha United National Independent Party (UNIP).

Kama sehemu nyingine, Waprotestanti wa Presbiteri na Methodisti ndio waliongoza katika kuchochea siasa ya kudai Uhuru. Kwa namna ya pekee, Kanisa la Methodisti la Kiafrika la Kiaskofu lililotokea Afrika ya Kusini na Zimbawe na mhubiri wake mkuu akiwa John Lester Membe, liliongoza.

Membe alihubiri hata katika mikutano ya chama cha siasa cha ANC cha Zambia. Hata Kenneth Kaunda kabla ya kuingia siasa, alijiunga na Kanisa hilo na kusaidia kama mhubiri na kiongozi wa Kwaya.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1962, vyama hivyo viwili vya ANC na UNIP viliungana katika Bunge, na kwa wingi wao wa kura, vikapinga muungano na kuuvunja. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1963, chama cha Kenneth Kaunda cha UNIP kilishinda na kuunda Serikali ya Zambia huru (1963-1991).

Katika miaka iliyofuata, Kaunda alishirikiana sana na Mwalimu Nyerere wa Tanzania kupigania Uhuru wa Afrika, hasa sehemu ya Kusini mwa Afrika, yaani Rhodesia, Afrika ya Kusini na Namibia, zikiwa chini ya ubaguzi wa rangi wa Makaburu; na Angola na Msumbiji zikiwa chini ya ukoloni wa Wareno.

Katika uhuru wa kuabudu na shughuli za kidini, Serikali zote baada ya Uhuru, hazikuwa na shida. Dosari ilikuwa mwaka 1962 ambapo Kaunda ilibidi apigane vita na dhehebu la Lenshina lililohubiri watu wasishiriki katika siasa na Serikali, na wakataka kufanya serikali yao ndani ya Nchi.

Katika vita hivyo, zaidi ya watu elfu moja waliuawa. Baadaye hata wafuasi wa dhehebu la Mashahidi wa Yehova wa Watchtower, walishambuliwa lakini siyo rasmi. Serikali ya Frederick Chiluba (1991-2001) aliyemshinda Kaunda katika uchaguzi wa mwaka 1991, akiwa mlokole, kidini alijaribu kuifanya Zambia iwe rasmi nchi ya Kikristo, lakini alipingwa na Viongozi wa Dini.

Vile vile Chiluba alifadhili na kuhamasisha madhehebu ya kilokole ya Kipentekoste. Chiluba alirithiwa na Levy Mwanawasa. Wakati huu, Kanisa Zambia liko msitari wa mbele katika kupigania haki za binadamu, na kuhamasisha watu katika siasa ya demokrasia shirikishi.

Waamini wengi wa Kanisa Katoliki mwanzoni walikuwa Kaskazini, katika sehemu ya Wamisionari wa Afrika (zamani White Fathers) au kabila la Wabemba. Mwaka 1950, walikuwa zaidi ya laki mbli wakati Kusini kwa Wajezuiti na Wafransiskani, Waamini walikuwa hawafiki elfu sitini.

Mwaka 1990, Kaskazini ilikuwa na Waamini kama laki tisa, ambapo Kusini walikaribia milioni moja na nusu. Hivyo uwingi wa Waamini ulikuwa umehamia Kusini, lakini hata hivyo, kati yao wengi walikuwa Wabemba waliohamia Kusini, hasa katika machimbo.

Mwaka 2005 kati ya wakazi 11,600,000, Wakristo walikuwa asilimia 75, ingawa kati ya hao Madhehebu mengi yalikuwa ya Kipentekoste yaliyoshamiri hasa wakati wa Chiluba, ambayo huchanganya Ukristo na tamaduni za Kiafrika.

Wakatoliki walikuwa asilimia 26 ya wakazi wote nchini humo, ingawa Wakatoliki si wengi sana kwa hesabu, nguvu zao za ushawishi wa watu ni kubwa sana.

Kanisa nchini Malawi
Nchi ya Malawi au Nyasaland, kama ilivyoitwa na wakoloni, wakifuatia jina ambalo Livingstone alilipa Ziwa la Nyasa, inakaliwa na makabila matatu. Wakazi asilia ni Wachewa, na hadi sasa ndilo kabila lenye watu wengi, na lugha yao ni lugha ya taifa, pamoja na Kiingereza.

Wachewa katika karne ya 15, waliongoza ufalme wa Maravi. Wakiwa na Makao yao Makuu Kusini ya Ziwa Nyasa, walishamiri na walitanuka hadi sehemu za Msumbiji na Zambia.
 
Ufalme huu uliangushwa na makundi mawili, la kwanza ni lile la Wangoni waliokimbia kutokana na mashambulizi ya Wazulu, wakiongozwa na Shaka. Wangoni kwa ukatili, waliteka falme walizokutana nazo njiani.

Kundi la pili lilikuwa la Wayao, ambao walishirikiana na Waarabu kwa kuteka watu na kuwauza utumwani. Wayao kwa sababu ya kushirikiana na Waarabu walishashika dini ya Kiislamu kama dini yao ya jadi.

Walianzisha vituo vya watumwa kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa, kituo kikubwa kikiwa Nkhotakota, ambacho kiliweza kusafirisha watumwa kati ya 5,000 hadi 20,000 kwa mwaka. Huu ndio unyama aliouona Livingstone na kuomba msaada wa ulimwengu kwa wenye mapenzi mema. Ni juhudi za Dkt. David Livingstone, Wamisionari wengi walimiminika Afrika ya Mashariki na Kati.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.