DAR ES SALAAAM
Na Dk. Felician B. Kilahama
Mungu Mwenyezi alituumba binadamu kwa ‘sura na mfano wake’ (Kitabu cha Mwanzo, 1:26); akatuweka duniani na kutupa madaraka ya kumiliki na kutawala vyote alivyoviumba.
Akisema: binadamu “wakatawale samaki baharini, ndege angani, wanyama, nchi yote vile vile, kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi.” Vile vile, Mungu akahitimisha uumbaji akiwaagiza mwanamume na mwanamke: “zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuimiliki”.
Tangu kuumbwa Adamu na Eva/Hawa, ni miaka mingi imepita. Hata hivyo, takwimu zinaashiria kuongezeka idadi ya watu duniani, ikiwa takriban bilioni nane (8), hii leo.
Hiyo ni ishara kuwa dunia inazidi kujaa watu wakati mataifa kama ‘China’ na ‘India’ yakiongoza kwa takriban asilimia 40 ya idadi ya watu wote. Tanzania yenye ardhi kubwa (hekta 94.55 milioni), kwa takwimu za 2022, kuna watu 61,741,120.
Kwa uwiano wa ukubwa wa nchi, bado tunatakiwa kuzaa na kuijaza nchi. Tunatumiaje ‘vipawa’ tulivyopewa na Mungu Mwenyezi? Vijana vipaumbele vyenu ni nini kama siyo kwanza kuwa baba hodari wa familia bora na yenye kumcha Mungu. Je, vijana wetu wamekengeushwa na nini: utandawazi, mifumo-dijitali na kuiga yasiyofaa, au ni mifumo kijamii na kiutawala?
Hakuna shaka mataifa yaliyoendelea hayajali chochote wanafanya kulingana na matakwa yao, kwenda kinyume na agizo la Mungu wakichochea maovu, mfano, kuhamasisha ndoa kati ya mwanaume na mwanaume (ushoga); mwanamke na mwanamke (ulezibiani), ikiwemo kutunga Sheria ‘kuharibu na/au kutoa mimba, na kuchochea wanawake wasipate ujauzito’.
Masuala hayo ni machukizo kwa Mungu aliyetuumba, akatujalia neema tuzae na kuongezeka. Wakati nikiwa mdogo, nilikuwa nasikia watu vijijini wakisema, “kuzaa watoto wengi ni baraka” familia zilikuwa zinafurahia kuzaa watoto na kuishi kwa uelewano mkubwa kama jamii moja. Nyakati hizi hali imekuwa tofauti kiasi cha ‘vijana’ kuoa na kuzaa watoto ni dhiki kubwa au kama ni laana, wakati ni baraka/zawadi kwa familia.
Maisha ya babu/bibi zetu yalikuwa yameegamia kwenye misingi/mifumo ya kijadi, kiutamaduni wakiabudu miungu mingine (ingawa walifahamu yupo Mungu Muumbaji. Mtazamo huo hautofautiani na ilivyoandikwa katika Matendo ya Mitume kwamba Mtume Paulo wakati akipita huku na huko akiwa ‘Athene’ akaona ‘Madhabahu’ iliyoandikwa: “Kwa Mungu Asiyejulikana”.
Ikawa baada ya kuyaona hayo, akawahubiria habari njema kuhusu huyo Mungu wanayemwabudu bila kumjua (Mdo, 17:23). Hivyo na wahenga wengi wa kale yalifanya hivyo hadi Injili ilipowafikia, takribani miaka 100 iliyopita.
Tukumbuke kuwa maisha yetu yamejengwa kwenye misingi ya mifumo ya kiroho ,ambayo Mungu aliiweka kimpangilio. Hivyo vijana wetu wanapaswa kufahamu kuwa kukiuka kuyatekeleza maagizo ya Mungu; mafanikio yatakuwa haba kwa kukosa maarifa yatokayo kwa Mungu.
Kilichonisukuma kuyasema hayo ni hali ya vijana wetu hususan wa kiume; kujisahau kuwa wao ni wanaume wanaotegemewa kujenga familia zilizo bora na endelevu. Nimekuwa nikisia msemo “dunia inawayawaya” ukimaanisha binadamu kukosa utulivu/umakini kwa kuhangaika huku na huko mpaka kupayapaya bila kujua mustakabali wa maisha kwa ujumla.
Ukitafakari hali hiyo kwa umakini mkubwa, utagundua kuwa hali ya sasa tunayoishuhudia kwa vijana wetu wa kiume, hakika ni matokeo ya kuhangaika kidunia zaidi, kuliko kusimama imara kwa msingi na maagizo ya Mungu Mwenyezi.
Moja ya athari kubwa kwa vijana Tanzania; ni ‘unywaji pombe’ uliokithiri. Kawaida Watanzania wengi vijijini/mijini wapo wanaokunywa pombe aina mbalimbali. Wakati nikiwa kijana kabla na baada ya kuanza shule; nilikuwa naona wanaokunywa pombe walikuwa watu wazima (wenye familia), hakuna kijana aliyekuwa hajaoa angeweza kuruhusiwa kujumuika nao.
Hata kama angekuwa ameoa, lakini bado hajawa na uzoefu wa kutosha kimaisha, haikuwa rahisi ajumuike na watu wazima. Mifumo kijadi au kimila ilikuwa imezuia vijana kutojitosa kwenye unywaji pombe bila ya kujijengea msingi imara wa kuweza kuyamudu maisha yake na familia.
Nyakati hizi maisha ni kidijitali, kisiasa, kisaikolojia, kiteknolojia, kimaendeleo hadi kusema kila mtu yuko huru kufanya anavyotaka ili mradi amefikisha umri wa miaka 18 au zaidi. Hali hiyo inakinzana na Sheria, Kanuni pamoja na Mifumo ya Kiroho aliyoiweka Mungu. Kadhalika, Serikali kwa dhamira ya kupata mapato zaidi, ikapunguza bei ya pombe.
Kimsingi, mapato ya Serikali yanapoongezeka, kwa namna moja au nyingine, tunatarajia huduma za kijamii kuboreshwa na kuimarisha miundombinu kwa maendeleo endelevu. Kuna pombe ambazo vijana wanachangamkia, mfano, “sungura” na “konyagi.” kadhalika, usambazaji pombe kwa kutumia vifungashio vyenye ujazo mdogo mdogo, unahamasisha vijana wengi wanywe pombe zaidi kwa bei poa.
Kuwepo vyanzo vya mapato kwa Serikali hasa ambavyo haviumizi walipa kodi na wananchi kwa ujumla ni jambo jema; lakini tunapotafakari suala la unywaji pombe ee-vijana wengi wanaathirika sana kwa kiwango cha taifa kuelekea pabaya. Mbali na pombe, changamoto nyingine ni “dawa za kulevya”; zikiwa kama ‘pacha’ wa pombe, kwa kutumiwa na vijana wengi.
Uzoefu unaonyesha kuwa kijana akishazoea dawa zinazolewesha, kuacha inakuwa kizaazaa. Kuna wakati Serikali ilijitahidi kudhibiti kwa kiasi kukubwa, matumizi ya dawa zinazolewesha kwa kuhakikisha haziingizwi nchi hovyo.
Hata hivyo, “operesheni iliyofanywa na Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za kulevya; iliyofanyika kati ya Agosti 24 na Septemba 2, 2024”; imedhihirisha kuwa sasa-upo udhaifu mkubwa katika mifumo husika ya kudhibiti uagizaji na uingizaji dawa zinazolewesha. Ripoti iliyotolewa na Mamlaka Septemba 10, ilionyesha kuwa kiasi kikubwa cha dawa hizo zilizoingizwa nchini, zikamatiwa Manispaa za Kinondoni na Ubungo kwa kuwanasa watuhumiwa kadhaa.
Swali linabaki. Je, dawa hizo zimepitia wapi bila kugundulika mpaka zikawa mitaani kiasi-hicho? Kadhalika, matumizi ya “bangi” (Cannabis sativa) pia yamekuwa yakiongezeka kila kukicha. Je, tunakwama wapi hadi taifa kushindwa kudhibiti matumizi ya dawa zinazolevya?
Tujitathimini kwa kina miaka michache ijayo nguvukazi nchini itakuwa ya namna gani Iwapo vijana wengi wa umri kati ya miaka 20 hadi 40 inakuwa katika hali hii isiyoridhisha, na huenda vijana wanaoinukia nao wakatumbukia kwenye janga hili. Nini hatima ya Tanzania? Kwanza, viongozi wajao watakuwa wa namna gani, wenye mwelekeo gani je, watakuwa na maarifa gani?
Je, Vijana wataishi maisha ya namna gani kama mwelekeo wao kwa sasa ni kunywa/kulewa kupindukia? Agosti, 2024 mtaa mmoja Jijini-Kati Dar-es-Salaam, karibu na Posta ya Zamani, niliona vijana wanne wamejibanza mahali akiwepo binti mmoja.
Kwa kuwa nilikwa nikitembea kwa miguu, nikapunguza mwenda taratibu kuona nini kinachoendelea. Nilichokishuhudia walikuwa wakinywa, lakini kwa kutunia chupa moja wakipokezana. Vile vile, walikuwa wanavuta kitu kama sigara pia kwa kupokezana: niliduwaa kwa hali niliyoiona bila kuwakaribia.
Mbele yangu alikuwa mama, mtu-mzima akielekea nilikokuwa natoka; baada ya kusalimiana. Nikamuuliza hiyo ni ishara gani kwa vijana wetu. Mama alisema hiyo ndiyo ‘hali halisi’ kwa vijana wa Tanzania. Tukaishia kusema: “Mwenyezi Mungu uwarehemu vijana hawa na wengine wa aina hiyo, maana wanaangamia kwa kukosa maarifa (akili zao zimepinda)”.
Tutamwomba Mungu, lakini kwa utashi aliotupa kuweza kufanya uchaguzi sahihi, mathalani, ufanye nini, ule nini, unywe nini, uvaeje au uishi maisha gani! Hivyo, inabidi tuwajibike kwa maisha tunayoishi. Dunia moja, ‘binadamu wote sawa’ lakini tunatofautiana katika uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuishi, vizuri bila kukengeuka hadi kupoteza ‘afya ya akili’ zetu.
Vijana kutumbukia kwenye unvwaji pombe na matumizi dawa zinazolevya, Mungu hahusiki hata kidogo, maana Mungu anatupenda na anatuwazia mema, pia huzibariki kazi za mikono yetu. Kadhalika, ili tubarikiwe, lazima ‘vigezo na masharti’kuzingatiwa ipasvyo. Kinyume cha hapo, ni laana mpaka huruma ya Mungu ipatikane kupitia toba ya kweli; pia kwa kufunga vile vile kuomba bila kukata-tamaa.
Ombi langu kwa Serikali, unywaji ‘pombe kupindukia’ ikiwemo ‘dawa-zinazolevya,’ hatua madhubuti zichukuliwe kwa kupandisha bei za ‘vileo’ vyote, pia kuhakikisha dawa-zinazolevya, zinadhibitiwa kwa hali ya juu sana kwa dhamira njema ili kuokoa nguvukazi ya taifa.
Vile vile, atakaye thibitishwa Kisheria kufanya biashara haramu, adhabukali zichukue mkondo wake bila kuoneana haya wala huruma, ili tusiendelee kuliangamiza taifa kwa maslahi binafsi. Taifa bora linahitaji ‘vijana’ imara, wenye nguvu, afya na akili timamu pamoja na maarifa ya kimbingu.
Kumbuka ‘kumcha Mungu’ ndiyo chanzo cha maarifa, na taifa lenye hofu ya Mungu hutenda haki kwa wote na kuuchukia ‘uovu’ kwa sababu ‘uovu’ ni janga kwa taifa, husababisha watu walaaniwe. Hivyo, tuwe makini tujiepushe na hali hiyo.