Dar es Salaam
Na Mwandishi wetu
Dekano wa Dekani ya Mtakatifu Thomas More, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Romwald Mukandala, amewataka waamini kuwa na upendo kwa majirani zao.
Padri Mukandala ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Kizito, Kilongawima, jimboni Dar es Salaam, alisema hayo hivi karibuni wakati wa Misa Takatifu ya Alhamisi Kuu iliyofanyika parokiani hapo.
Alisema kuwa waamini inabidi muoneshane upendo, hasa kwa majirani zetu…mkitambua kwamba sisi sote ni Watoto wa Baba Mmoja, ambaye ni Mungu Mwenyezi,” alisema Padri Mukandala.
Alisema kuwa jambo lingine ambalo waamini hao wanatakiwa kulisimamia ni kuwa na Imani na Mapadri wao wanaowaongoza katika Imani.
Padri Mukandala alisema kuwa Mapadri ni watumishi wa Mungu, ambao hawapaswi kutetwa na kusemwa kama inavyofanyika kwa baadhi ya waamini, akiwasihi waendelee kuwaombea Mapadri ili waweze kutekeleza vyema utume wao.
Akizungumzia Alhamisi Kuu, Padri Mukandala alisema kuwa hiyo ni Siku ya Mapadri, kwani ndiyo siku ambayo Bwana Yesu Kristo alisimika rasmi Misa Takatifu kwa njia ya karamu ya mwisho, alipokula pamoja na wanafunzi wake.
“Sisi ni wafuasi wa Kristo. Je tunapomfuata yeye, tunayaishi hayo? Mungu atusaidie tuache tabia ya ubinafsi, uchoyo, tujitoe kwa wenzetu,”alisema Padri Mukandala.
Ahimiza utunzaji wa mazingira
Kwa mujibu wa Padri Mukandala, waamini wote wanatakiwa kuhakikisha wanatunza mazingira katika maeneo yao kwa kupanda miti katika kutekeleza Waraka wa Baba Mtakatifu Fransisko wa ‘Laudato Si’ unaohitimiza utunzaji wa mazingira.
Alisema kuwa kuna kila sababu kwa waamini kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anatimiza wajibu wa kupanda miti kwa wingi katika maeneo yake, na hata katika Maparokia ili kutunza mazingira ili yawe katika hali bora.
Naye Mlezi wa Seminari Kuu ya Segerea, Padri Siegried Ntare aliwataka Wakristo kuishi Ukristo wao kwa kumpenda Mungu kwa kusali na kuyashika Maandiko Matakatifu.