Dar es Salaam
Na Mathayo Kijazi
Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Mtume, Stakishari, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wametakiwa kuishi maisha ya utakatifu, wakitambua kamba wamebatizwa ili kuishi kitakatifu.
Hayo yalisemwa hivi karibuni na Paroko wa Parokia hiyo, Padri Laurent Lelo wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyokwenda sanjari na kuapishwa kwa Viongozi wa Utume wa Wanaume Katoliki (UWAKA), Taifa, iliyofanyika parokiani hapo.
Katika homilia yake, Padri Lelo aliwasisitiza Waamini kupendana kutoka ndani ya mioyo yao, wakisaidiana pale inapohitajika, kwani hiyo ni moja ya sifa za Mkristo.
Alisema kuwa kila mmoja anatakiwa kumkimbilia Mungu zaidi, na kuwakumbusha kwamba mtu anapoutafuta utakatifu, ndipo shetani anapozidi kumnyemelea.
Wakati huo huo, Wakristo wameaswa kutambua kwamba nguvu ya Mungu ni kubwa kuliko ya mwanadamu, kwani ndiye mkombozi, na anayewatoa katika majaribu kila wanapokutana nayo.
Kwa mujibu wa Padri Lelo, waamini hao wanapaswa kuendelea kumwomba Mungu ili familia, Jumuiya, na hata Parokia zao ziwe katika muungano, huku wakiikimbilia huruma ya Mungu, kwani itawasaidia pale wanapotawanyika, hivyo Yeye aweze kuwarudisha katika misingi iliyo bora.
Aidha, wao kama wabatizwa, walikumbushwa pia kusaidia kuwarudisha kundini wale waliosambaratika, huku wakiaswa kuwa kwa kufanya hivyo, watakuwa wametimiza wajibu wao.
Padri Lelo aliwasisitiza Wakristo kulihubiri Neno la Mungu, na kuongeza kuwa hata katika shamba la Bwana, mavuno ni mengi, bali watenda kazi ni wachache.
Viongozi wa UWAKA Taifa, walioapishwa katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu, ni Mwenyekiti Cassian Njowoka, Mwenyekiti Msaidizi Salvatory Mrema, Katibu Silvester Musumi, na Katibu Msaidizi, Seraphin Mvungi.