Dodoma
Na Mwandishi wetu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amekemea vitendo vya mateso na unyanyasaji kijinsia vinavyofanyika dhidi ya mabiinti wa shule kwa kukeketwa, kuwaajiri kama wafanyakazi wa ndani, na kuwaozesha.
Chongolo alitoa onyo hilo mjini Dodoma baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa katika Shule ya Sekondari Chilonwa, iliyopo wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Alisema kuwa tabia ya ukeketaji dhidi ya watoto wa kike haivumiliki na haikubaliki, akiitaka Jamii kubadili mtazamo na kuwafichua wote wenye kujihusisha na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Katika hatua nyingine, Chongolo alitoa maelekezo kwa Wizara ya Maji pamoja na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa- TAMISEMI, kuweka mkakati maalum utakaowezesha kujengwa kwa miundombinu ya maji shuleni hapo na maeneo mengine yanayotoa huduma za jamii.
Chongolo alitembelea Wilaya ya Chamwino baada ya kuhitimisha ziara yake katika Wilaya za Kongwa na Mpwapwa, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku nane mkoani Dodoma kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Wakati huo huo, Chongolo aliitaka Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), kuwawezesha zaidi wafugaji wadogo ili watoke katika ufugaji wa kawaida, na wafikie daraja la ufugaji wa kibiashara.
Alitoa agizo hilo wakati alipotembelea NARCO Ranchi ya Kongwa Mkaoni Dodoma, katika mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM.
Akizungumza katika Ranchi hiyo, Chongolo alisema kuwa kuna wafugaji ambao wana mifugo mingi, lakini haiwafaidishi kutokana na kukosa elimu ya ufugaji kibiashara, na hivyo kutumia mazao ya Ng’ombe kama ngozi na Pembe katika matumizi yasiyo na tija kwao.
Aidha, aliagiza kupelekwa mbegu katika maeneo ya malisho ya wakulima wa kawaida ili kulima mazao ya ng’ombe yatakayosaidia katika malisho, hasa katika kipindi cha kiangazi ambacho kuna changamoto ya malisho.
Kwa upende wake, Mkurugenzi wa NARCO Peter Msofe ameiomba Serikali kuwawezesha katika miradi miwili yenye thamani ya Shilingi bilioni 84 yenye lengo la kutoa Elimu kwa Wanawake na Vijana kuhusu ufugaji, pamoja na mradi wa unenepeshaji ng’ombe.
Ranchi hiyo ya Kongwa ina hekta 38,000 ambapo ndani yake kuna mifugo 30000, huku hekta 18,000 wakipewa wawekezaji, wakiwemo wananchi.