Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea Historia ya Dini ilivyokuwa wakati wa Mapinduzi ya Viwanda (Industrial Revolution) barani Ulaya. Leo tunawaletea Misingi na Haki ya Mafundisho ya Kijamii ya Kanisa. Sasa endelea…
Mwaka 1967 Papa Paulo VI (1963-1978: wa 262) alitoa barua yake ya Kichungaji “Populorum Progressio,” yaani ‘Maendeleo ya Binadamu’. Licha ya mengine, alisisitiza kwamba hakuna maendeleo ya kweli, kama siyo ya binadamu wote.
Anasisitiza juu ya wajibu wa mataifa tajiri kusaidia yale maskini. Wakati wa kuadhimisha miaka 80 tangu itolewe barua ya Rerum Novarum Mei mwaka 1891, Papa Paulo VI alitoa barua ya Kitume mwezi Mei 1971 “Octogesima Adveniens”, yaani ”Ujio wa Miaka Themanini”.
Katika barua hiyo, aliongelea hasa hali duni katika miji. Tarehe 26 Oktoba 1975 alitoa barua nyingine ya “Evangelii Nuntiandi”, yaani “Utangazaji wa Injili”, ikiadhimisha miaka 10 ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano (1962-1965), alisisitiza kwamba kazi ya Kanisa ni kupigana dhidi ya uonevu na udhalilishaji.
Papa Yohana Paulo II (1978-2005: wa 264) alitoa barua mbili kukazia mafundisho hayo ya Kanisa juu ya jamii. Mwaka 1981 ikiwa miaka 90 tangu barua ya Rerum Novarum, aliandika barua ya kitume ya “Laborem Exercens” akisisitiza kwamba haki binafsi ya kuwa na mali haipashwi kuathiri umma, yaani haki ya wote kuwa na mali au kukiuka haki za jamii.
Papa Yohana Paulo II alirudia mawazo hayo kwa mkazo zaidi, hasa akikosoa ubepari uliopindukia, na ujamaa hasi katika barua yake nyingine ya kitume “Centesimus Annus” ya mwaka 1991, akiadhimisha miaka 100 ya Rerum Novarum.
Kwa namna hii, unaonekana umuhimu wa barua ya Papa Leo XIII (1878-1903: 256) iliyolitoa Kanisa katika makucha ya mabepari bila kuiingiza katika utumwa wa wajamaa hasi, au ukomunisti. Kabla Papa Yohana Paulo II hajafariki mwaka 2005. ulitolewa muhtasari (Compendium) ya Mafundisho ya Kanisa juu ya jamii.
Papa Benedikto XVI (2005 -2013: wa 265) akifuata katika nyayo za watangulizi wake, mwaka 2009 alitoa barua ya Kitume “Caritas in Veritate”, yaani “Upendo katika Ukweli”.
Licha ya kusisitiza yale yaliyosemwa na watangulizi wake, pia aliisifu hasa barua ya kitume ya Papa Paulo VI ya mwaka 1967” Populorum Progressio” kwa kuongelea, siyo tu juu ya maslahi ya wafanyakazi, bali pia juu ya maendeleo ya binadamu mzima (Integral Developoment).
Papa Benedikto XVI alikosoa sana ubepari, akiuona kukosa utu na kuwa na ubinafsi wa kujitafutia faida kutoka kwa wengine bila kuona wajibu wa kurudisha vilevile kwa jamii. Alisisitiza juu ya haki za jamii kuzidi haki za mtu binafsi kupata faida. Alilaumu ubepari kwa madhara ya siki hizi, yakiwemo vilevile balaa la madawa ya kulevya.
Papa Fransisko (wa sasa: 2013: wa 266), mafundisho yake yote ni juu ya upendo na kujali. Mwaka 2016 alitangaza mwaka wa Huruma ya Mungu na Upatanisho. Mafundisho yote ya wakati huo yalikuwa Mungu atakuhurumia, nawe ukiwahurumia wengine.
“Kuweni na Huruma kama Baba yenu wa Mbunguni alivyo na Huruma.” Katika barua yake ya Kitume “Evangelium Gauduim” au “Furaha ya Injili” ya mwaka 2013, anasihi serikali mbalimbali na vyombo vya kimataifa vya fedha kuhakikisha kuwa watu wanapata haki za msingi, yaani kazi, afya na elimu.
Anakubali haki ya serikali kuingilia uchumi kwa wema wa umma. Anapinga utamaduni wa kuabudu fedha na kuacha soko huria kwa faida ya wachache, wakati wengi wanakuwa fukara. Analaami utofauti unaoongezeka kati ya walionacho na wasionacho.
Katika barua nyingine ya Kitume ya mwaka 2015 “Laudato Si”, ambayo ilipokelewa vizuri sana na watu wa rika na Imani mbalimbali, anaongelea siyo tu juu ya haki ya wanyonge, bali na ulazima wa kutunza mazingira, na kulaani matumizi mabaya ya nyenzo za dunia kwa sababu ya ulafi.
Aliongeza barua nyingine mbili akisisitiza juu ya upendo na kujali; “Gaudete et Exultate” yaani “Furahini na Kushangilia” ya mwaka 2018 na “Fratelli Tutti”, yaani “Sote ni Ndugu”, ya mwaka 2020.
Kanisa katika mafundisho yake ya kijamii katika miaka hii yote, imesisitiza juu ya mambo yafuatayo:
1. Haki ya Uhai:
Maisha ya binadamu ni matakatifu tangu kutungwa mimba hadi kifo. Kila binadamu siyo tu ana haki ya kuishi, bali pia ana haki ya kupata heshima. Katika mafundisho yake yote, Kanisa linasisitiza kwamba kila binadamu ameumbwa katika sura ya Mungu, na watu wote wana haki sawa mbele ya Mungu, na hivyo wanastahili heshima.
2. Auni (Subsidiarity):
Hii ilisisitizwa hasa kuanzia na barua ya Papa Pio XI ya Quadragesimo Anno mwaka 1931. Madaraka ya juu yasichukue kile ambacho madaraka ya chini yanaweza, na yana haki nacho. Mkubwa asaidie kile ambacho mdogo hawezi peke yake kufanya, la sivyo unamnyang’anya heshima na juhudi zake.
3. Mshikamamno na kufanya juhudi kwa wema wa wote (Common Good):
Watu hatuko kisiwa, hivyo lazima kusaidiana kama binafsi, kama junuiya, na kama mataifa.
4. Upendo ndio upeo wa yote:
Hapa siyo upendo wa kihisia, bali ni upendo wa kweli wa kujitoa kwa ajili ya wengine.
Hayo maagizo manne yanakuwa msingi wa haki na wajibu katika Mafundisho ya Kanisa juu ya jamii kama haki ya kupata kazi; haki ya familia; haki ya uhuru wa kuabudu na kuwasiliana; utunzaji wa mazingira; haki ya kuwa na mali binafsi; kujali maskini; na wasiojiweza.