Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Wachezaji saba wa Kitanzania wanaoshiriki Ligi Kuu soka Tanzania Bara wanaongoza kwa kufunga mabao ya mapema zaidi kuliko katika mechi za duru la kwanza za Ligi hiyo.
Ligi hiyo ya timu 16 tayari imemaliza raundi 15 za duru la kwanza hivi karibuni, na hivyo kuanza mechi za duru la pili la Ligi hiyo.
Nyota hao wazawa waliofunga mabao ya mapema katika mechi mbalimbali ni Mudathir Yahaya(Yanga), Sospeter Bajana(Azam FC), Yassin Mgaza(Dodoma Jiji), Awesu Awesu (KMC), Ibrahim Ajib (Coastal Union), Zidane Sereri(Dodoma Jiji) na Feisal Salum(Azam FC).
Mudathir Yahaya wa Yanga ndiye anayeongoza kwa kufunga bao la mapema zaidi kuliko wengine baada ya kufunga bao katika sekunde ya 44 kwenye mchezo wa Februari 17 dhidi ya KMC ambapo Yanga ilishinda 3-0 kwenye dimba la Jamhuri mjini Morogoro.
Sospeter Bajana wa Azam FC anafuatia kwa kufunga bao la mapema katika sekunde ya 54 dhidi ya JKT Tanzania, ambapo Azam ilishinda 2-1 siku ya Desemba 11 mwaka jana kwenye uwanja wa Azam Complex.
Awesu Awesu wa KMC alifunga bao katika dakika ya kwanza na sekunde 33 kwenye mchezo dhidi ya Mashujaa FC katika dimba la Uhuru jijini Dar es salaam, ambapo KMC ilishinda mabao 3-2 Desemba pili mwaka jana.
Ibrahim Ajib aliifungia Coastal Union bao la mapema kwa njia ya penati katika dakika ya kwanza na sekunde 42 na kuipa pointi zote tatu timu yake baada ya mchezo kumalizika kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye dimba la Mkwakwani jijini Tanga.
Penati hiyo pia imekuwa ya mapema zaidi kutokea kwenye Ligi hadi sasa, baada ya kutokea katika sekunde ya 15 tu, kabla ya Ajib kufunga kwenye dakika ya kwanza.
Mchezaji Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji alifunga bao katika dakika ya kwanza na sekunde 55 wakati walipocheza na wenyeji Tabora United kwenye dimba la Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora ambapo hata hivyo Dodoma ilipoteza mchezo huo kwa kufungwa 2-1.
Kiungo wa Dodoma jiji Zidane Sereri pia alifunga bao la mapema katika dakika ya pili dhidi ya KMC, huku Feisal Salum wa Azam FC akifunga bao katika dakika ya 3 dhidi ya Tabora United.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni waliofunga mabao ya mapema ni Zozuzoua Pacome na Kennedy Musonda, wote kutoka Yanga waliofunga katika dakika ya 3 kwenye mechi tofauti.

Viongozi wa Halmashauri ya Walei na Waamini wa Parokia ya Bikira Maria wa Mateso - Mbezi Msakuzi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Ekaristi Takatifu kwa watoto 90, iliyoadhimishwa parokiani hapo hivi karibuni.

Waamini wa Kanda ya Bethlehemu, Parokia ya Thomas More, Mbezi Beach, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakiwa katika maandamano ya kutembeza Msalaba wa Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogo Ndogo, baada ya kukabidhiwa kutoka kwa Paroko wa Parokia hiyo, Padri Ladislaus Kapinda (mwenye kanzu).

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Mikael Malaika Mkuu, Kawe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Bonus Ngoo, akiwapaka waamini Majivu wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jumatano ya Majivu, iliyoadhimishwa parokani hapo.

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Roho Mtakatifu, Segerea, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Amedeus Babu akiwapaka waamini Majivu wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jumatano ya Majivu iliyoadhimishwa parokani hapo.

Mwalimu na Mlezi wa Seminari Kuu ya Mtakatifu Antoni wa Padua – Ntungamo, Jimbo Katoliki la Bukoba, Padri Roland Kashaga (katikati kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa Komunio ya Kwanza baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya watoto 90 kupokea Ekaristi Takatifu, iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Mateso - Mbezi Msakuzi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. Kulia katikati ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Fregiel Massawe. (Picha na Yohana Kasosi)

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan akimpatia Baba Mtakatifu Fransisko zawadi wakati Rais na Ujumbe wake wa Tanzania ulipofanya ziara ya kitaifa, na kuzungumza na Baba Mtakatifu mjini Vatican. (Picha kwa Hisani ya Ikulu)

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Wakati Mfungo wa Kwaresma ukiwa umeanza, Wakristo wametakiwa kujikita katika toba, sala, kufanya matendo ya huruma na upendo katika kipindi chote cha mfungo huo wa siku 40.
Wito huo ulitolewa na Maaskofu, na Mapadri wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam wakati wakitoa homilia katika Maadhimisho ya Misa Takatifu zilizoadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu; Parokia ya Mtakatifu Petro – Oysterbay; Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja – Boko; na Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, aliyeadhimisha Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, alisema kuwa ni vyema kujikita katika matendo ya huruma na upendo, huku wakimrudia Mungu.
“Ndugu zangu, Neno la Mungu kwa msisitizo mkubwa, litatualika na kutuasa kujikita katika toba, kujikita katika sala, kujikita katika huruma na upendo tukimrudia Mungu. Hizi ni zama za mtandao. Kishawishi kikubwa, ni kule watu kutaka kufanya mambo yaonekane mtandaoni,” alisema Askofu Mkuu.
Askofu Mkuu alisema kuwa toba ya kweli siyo mambo ya mtandao, bali ni mabadiliko ya ndani, kuongoka rohoni, kumrudia Mungu kwa dhati, pamoja na kuanza upya, kwani hilo ndilo waliloaswa katika masomo waliyoyapitia katika Misa hiyo.
Pia, aliwasisitiza Waamini kufahamu kwamba majivu ni kielelezo cha toba, akisema kuwa watu wa kale walipofanya toba, walijipaka majivu, wakajivika magunia, na wakatembea katika unyofu na uadilifu.
Aliongeza kuwa Wakristo wanapopakwa majivu na kufanya toba, hawatakiwi kufanya maonyesho, bali wamwombe Mungu kwa mioyo radhi ili awahurumie dhambi zao, awajaze neema yake, na awajalie wajikite katika safari ya kipindi cha Kwaresma, huku wakimrudia Mungu.
“Sisi tunapojipaka majivu tukifanya toba, hatutaki kufanya maonyesho, bali tunataka kumwomba Mungu kwa mioyo radhi, atuhurumie dhambi zetu, atujaze neema yake, atujalie tujikite katika safari ya kipindi cha Kwaresma, tumrudie Mungu tukimwomba toba kwa ajili ya dhambi zetu, kwa ajili ya dhambi za ulimwengu, na yote yale yaliyo machukizo kwake.
Kwa upande wake Askofu Msaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Stephano Musomba wakati wa homilia yake katika Parokia ya Mtakatifu Petro – Oysterbay jimboni humo, aliwataka Wakristo kuwa wanyenyekevu, huku wakitambua mipaka yao, udhaifu wao, na kufahamu kwamba Mungu ni muhimu katika maisha yao.
Katika homilia yake, Askofu Msaidizi Musomba aliwataka Waamini katika kipindi hiki cha Kwaresma, kuombana msamaha pale wanapokoseana, na pale wanapomkosea Mungu, ili waanze upya na waendelee vizuri na maisha yao.
Naye Paroko wa Parokia ya Mwenyeheri Isdori Bakanja – Boko, jimboni humo, Padri Emmanuel Makusaro aliwaalika Waamini kufunga matendo ya dhambi pamoja na kuwasaidia wahitaji, kwani hapo Kwaresma ndipo itakuwa na nguvu zaidi.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimboni humo, Padri Cornelius Mashare alitoa wito kwa Waamini kutafakari, huku wakiishi maisha ya unyenyekevu na yenye kumpendeza Mungu katika kipindi hiki cha Kwaresma.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Tanzania na Vatican zimeridhika na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili kwa mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.
Katika mazungumzo ya faragha kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Fransisko yaliyodumu kwa takribani dakika 25, Viongozi hao waliridhika na mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, licha ya changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.
Aidha, Viongozi hao katika mazungumzo yao walijikita zaidi katika masuala ya kijamii, Kikanda, Kimataifa na umuhimu kudumisha amani miongoni mwa jamii.
Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa Aprili 19 mwaka 1968 na Askofu Mkuu Pierluigi Sartorelli aliyeteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi Desemba 22 mwaka 1970.
Uhusiano huo kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto XVI (2005-2013: wa 265, aliyefariki mwaka 2023), wakati akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Ali Abeid Aman Karume wa Tanzania mjini Vatican, unasimikwa katika tunu msingi za Amani, haki, mshikamano na uhuru, kwani haya ni mambo yanayopata asili yake kutoka katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, yakipewa msukumo wa pekee.
Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania, na katika mchakato wa kudumisha amani ulimwenguni.
Takwimu zinaonesha kwamba Kanisa Katoliki nchini Tanzania linamiliki na kuendesha Shule za Awali 240, Shule za Msingi 147, Shule za Sekondari 244, Vyuo vya ufundi, vyuo vikuu vitano; taasisi za elimu ya juu 5, na vituo viwili ambavyo viko chini ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino, (St. Augustine University of Tanzania: SAUT), Mwanza.
Vyuo vyote hivyo vina jumla ya wanafunzi 31, 000 pamoja na taasisi 473 za afya, kwa lengo la kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya shule zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki, pamoja na dhamana ya Uinjilishaji wa kina inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Uinjilishaji nchini Tanzania.
Shule na taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki nchini, vimekuwa ni vituo vya majiundo makini ya vijana, kiakili, kimaadili, kiroho na kiutu, kwa kuzingatia ubora na viwango vya kitaifa na kimataifa, ukweli ambao kamwe hauwezi kufumbiwa macho nchini Tanzania.
Elimu bora inayotolewa na Kanisa, inalenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na Kimataifa kwa kuwapatia: elimu, ujuzi na uwezo wa kushiriki katika ujenzi wa Tanzania, katika ujumla wake.
Historia inaonesha kuwa wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanzania mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII (1958-1963: wa 261), alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanzania ili uhuru wake uwawezeshe Watanzania kuishi maisha mema zaidi kadri iwastahilivyo watoto wa Mungu.
Imepita takribani miaka 12 tangu Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania alipotembelea mjini Vatican na kukutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Januari 19 mwaka 2012.
Katika ziara hiyo, Rais Samia aliambatana na Mama Evaline Malisa Ntenga, Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani na Rais wa World Union of Catholic Women’s Organisations (WUCWO) Afrika, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Taifa, nchini Tanzania.
Wengine ni Profesa Deogratius Rutatora, Mwenyekiti Halmashauri ya Walei, Taifa; Leonard Mapolu, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Wafanyakazi Tanzania, Taifa, VIWAWA; Dalmas Gregory, Mwenyekiti Halmashauri Walei, Jimbo Katoliki la Zanzibar, na Theresia Seda, Mwenyekiti wa Utoto Mtakatifu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ameiagiza Taasisi zote za ununuzi nchini (Serikali na Binafsi) kuhakikisha zinatoa kipaumbele katika manunuzi ya bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi ili kukuza uchumi wa Watanzania, na wazingatie kutoa kipaumbele kwa wafanyabiashara wadogo na makundi maalum.
Dk. Biteko alisema hayo Jijini Dodoma katika hafla ya utiaji saini hati ya makubaliano kati ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (Public Procurement Regulatory Authority: PPRA) na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Economic Empowerment Council: NEEC) ili kujenga ushirikiano unaolenga kuchochea ushiriki wa Wafanyabishara Wadogo, wa kati na Makundi Maalum, katika masuala ya ununuzi wa umma.
“Kusainiwa kwa hati hii leo, kunazidi kuboresha mazingira ya Watanzania kushiriki kwenye uchumi wa nchi yao, hasa watu kutoka makundi maalum. Haya ni  maelekezo ya Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wote wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, hivyo NEEC, PPRA, Taasisi nyingine za Serikali na Binafsi, wawezesheni Watanzania kushika uchumi wa nchi na muone fahari katika hili,” alisema Dk. Biteko.
Kupitia hafla hiyo, Dk. Biteko aliitaka PPRA kuzidi kuboresha huduma zake kwa Watanzania, ikiwa ni pamoja na kuharakisha mchakato wa rufaa zinazowasilishwa kwenye mamlaka hiyo, hususan zile zinazohusisha waombaji wa zabuni kutoka makundi maalum ili kuchochea kasi ya ukuaji wa Uchumi wa mtu mmoja mmoja, na hatimaye Uchumi wa Taifa.
Alizitaka mamlaka hizo kujikita zaidi katika uwezeshaji wa wananchi kwa kutoa elimu, badala ya kubaki kuwa wadhibiti pekee.
Dk. BIteko aliongeza kusema kwamba NEEC na PPRA kufanya tathmini na kutoa tuzo kwa watoa huduma wanaofanya vizuri katika uwezeshaji wa makundi maalum suala litakalochagiza ushindani miongoni mwa watoa huduma, na hatmaye kukuza uchumi.
Alisema kuwa makubaliano hayo yatatumika kama jukwaa la kuwahamasisha watu wa kundi hilo kushiriki na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja, kuimarisha wigo wa walipa kodi, na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Aliipongeza PPRA kwa kuweka kanuni ya ushirikishaji makundi maalum kwenye manunuzi ambayo imeelekeza kuwa asilimia 30 ya zabuni zote zitolewe kwa washiriki kutoka makundi maalum, ambao ni wanawake,vijana, wazee na wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Jenista Mhagama, alisema kusainiwa kwa hati ya makubaliano kati ya PPRA na NEEC ni ushahidi wa namna Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoamua kwa dhati kushikirisha makundi ya watu maalum kwenye uchumi na ujenzi wa Taifa.
Alisema kuwa makubalinao hayo yataongeza ushiriki wa makundi maalum kwenye manunuzi ya umma, na hii itaongeza uwezo wa Watanzania katika uzalishaji malighafi na bidhaa pamoja na utoaji wa huduma ndani ya nchi.