DAR ES SALAAM
Na Pd. Dkt. Clement Kihiyo (TEC)
Mwaka wa Liturujia Leo ya Wokovu
1. Utangulizi:
Ishara na matendo yanayofanywa kwa wakati huwa njia ya wokovu kwetu. Mwaka wa Liturujia ambao pia huitwa mwaka wa Kanisa ni fumbo la Kristo. Ni kwa njia ya maadhimisho ya kumbukumbu takatifu ndani ya Mwaka wa Liturujia, ndipo tunapata wokovu. Katika Mwaka wa Liturujia, Fumbo zima la Kristo linafunuliwa; yaani, kutoka Umwilisho na kuzaliwa, na kutoka Kupaa hadi Pentekoste
Mama Kanisa Takatifu huchukulia wajibu wake kuadhimisha kwa kumbukumbu takatifu kazi ya ukombozi ya Bwanaarusi wake aliye Mungu, katika siku zilizopangwa katika mwenendo wa mwaka mzima. Kila juma, Kanisa katika siku aliyoiita “Dominika”, yaani “Siku ya Bwana”, linaadhimisha kumbukumbu ya ufufuko wa Bwana. Kwa namna ya pekee, linauadhimisha ufufuko huo pamoja na mateso yake yenye heri mara moja kwa mwaka katika Sikukuu ya Pasaka, iliyo kubwa kuliko maadhimisho yoyote (SC 102).
Katika mzunguko wa mwaka mzima, Mama Kanisa analikunjua fumbo la Kristo, tangu umwilisho na kuzaliwa, hadi kupaa mbinguni, mpaka siku ya Pentekoste na kungojea kwa tumaini lenye heri kurudi kwake Bwana. Anapokumbuka namna hii mafumbo ya ukombozi, Kanisa huwafungulia waamini utajiri wa uweza na mastahili ya Bwana wake. Kwa njia hii, uwepo wa mafumbo haya unakuwapo kwa nyakati zote, ili kutoka humo waamini waweze kuchota na kujazwa neema ya wokovu.
Mwaka wa Liturujia pia unawakilisha na kueneza tena imani, maisha ya Kikristo na uwepo wa ukombozi wa Kristo na utajiri wa wokovu (SC. 102c). Mwaka wa Liturujia ni safari ya wokovu wa Kristo Mwenyewe na Kanisa lake (Lk, 24:15). Mwaka wa Liturujia sio mfuatano wa jumla wa siku na miezi, lakini unakuwa alama/ishara ya mfuatano ambao matukio ya neema yanatokea kama matukio ya wokovu kwetu hapa leo. Mwaka wa Liturujia ni wakati wa wokovu, ‘epifania’ ‘hic et nunc’ (hapa na sasa) kwetu.
2. Baadhi ya Mambo Makuu ya Mwaka wa Liturujia
2.1 Mwaka wa Liturujia ni Maadhimisho:
Matukio ya Mwaka wa Liturujia sio tu mifano ya kutafakari au kuiga uungu, lakini ni ishara zenye ufanisi za wokovu, ambao Kristo katika Utatu Mtakatifu, wamekamilisha kwa wokovu wa wanadamu. Mambo makuu ya ukombozi ni sisi kuadhimisha na kurithisha kwa kizazi kingine. Mwaka wa Liturujia una nguvu maalum ya kisakramenti na ufanisi wa kuimarisha maisha ya Kikristo.
2.2 Mwaka wa Liturujia Kuanzia Ufufuko:
Tukianzia na habari ya wanafunzi wa Emao (Lk 24:25-26); Yesu alieleza kisa chote kuanzia Ufufuko hadi Manabii. Ina maana kila kitu kinamhusu Kristo. “Bila ufufuko imani yetu haina maana” (1Kor. 15:13-17). Ufufuko ni chanzo na kitovu cha Mwaka wa Liturujia. Ufufuko ni siku ya Adamu Mpya (Rum. 11:5, Efe 2:5,8).
2.3 Siku ya Kwanza ya Juma-Dominika- Siku ya Bwana
Tangazo la ufufuko lilianza siku hii kwa amri ya Bwana (Mk.16.7, Mt. 28.7, Lk. 24.9). Ndipo wale wanawake wakatangaza ufufuko siku ile ile. Kwa hiyo, Dominika ni mwendelezo wa tangazo la Ufufuko. “Tunasherehekea Dominika kwa sababu ya Ufufuko Mtukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo, na tunafanya hivyo sio tu wakati wa Pasaka bali pia kila mzunguko wa juma, yaani kila Siku ya Kwanza ya Juma. Mtakatifu Augustino anaiita Dominika kwa usahihi kama Sakramenti ya Pasaka (Taz . In Io. Tract . XX, 202: CCL 36,203), (SC 26, 184). Kwa Kanisa la Mashariki Dominika ni ‘Anastasimos hemera’, yaani, siku ya ufufuko.
Matendo ya kiliturujia si matendo ya kila mmoja peke yake, bali ni maadhimisho ya Kanisa, ambalo ni “sakramenti ya umoja”, yaani taifa takatifu linalokusanywa na kuratibishwa chini ya uongozi wa Maaskofu SC 26.
Kwa sababu hiyo matendo hayo ni ya mwili wote kabisa wa Kanisa, nayo huudhihirisha na kuuimarisha. Aidha, kila mmoja wa wanakanisa anahusika kwa namna tofauti, kadiri ya utofauti wa daraja, wa majukumu, na wa ushiriki kiutendaji
Matukio maalum ya kimungu siku ya Dominika pia yanaipa siku hii umaalumu wake. Maana yake:
i. Roho Mtakatifu alitolewa kwa Wanafunzi siku ya Dominika (Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa),
ii. Pentekoste ilikuwa siku ya Dominika,
iii. Dominika ni siku ya Amani, siku ya Yubilei ya Roho Mtakatifu (Lk 4:18-19, Isa 61:1-3).
iv. Kwa namna ya pekee, Dominika ni siku ya uumbaji mpya, siku ya Jua Jipya (Mal, 4:2).
2.4 Dominika ni Kitovu na Kiini cha Mwaka wa Liturujia:
Dominika ni Kitovu na Kiini cha Mwaka wa Liturujia kwa muktadha ufuatao:
Dominika ni siku ya Bwana. Wayunani wanaiita, “Kyriake Hemera”, ambapo kivumishi ‘Kyriake’ kinarejelea Kyrios, yaani Bwana aliyefufuka pamoja na Roho (1 Kor. 16:2, Mdo, 20:7, Ufu.1.10).
Dominika ni siku ya kimungu ya kumwadhimisha Bwana, siku kwa ajili ya kumega mkate na Neno, siku kwa ajili ya karamu na kwa ajili ya kukusanya sadaka kwa ajili ya maskini (2 Kor, 9:12, Rum. 15:27).
Dominika ni siku ya mwanzo wa uumbaji, ni siku ya nane baada ya ufufuko. Ni siku ya nane kwa sababu ni nje ya muda unaopimwa katika wiki. Siku ya nane ni siku ya Ekaristi. Hivyo, Dominika hugusa fumbo zima la wokovu. Inaleta pamoja na yenyewe ulimwengu wote wa mfano wa Kikristo. Inaangazia siku ya mwisho, siku ya Parousia.
Kwa hiyo, Dominika ni siku maalum na siku pekee ya Bwana. Inaunda mwendelezo halisi wa adhimisho wa Kanisa kutoka Pentekoste hadi kurudi kwa Bwana. Maadhimisho mengine, isipokuwa kama yana umuhimu mkubwa, hayatapewa kipaumbele kuliko Dominika ambayo ndiyo msingi wa kweli na kiini cha Mwaka mzima wa Liturujia.
Kadri ya mapokeo ya Mitume, yanayopata asili yake katika siku ya ufufuko wa Kristo, Kanisa huadhimisha fumbo la Pasaka kila siku ya nane, katika siku ile iitwayo kwa haki kabisa Siku ya Bwana au Dominika. Katika siku hii Waamini wanapaswa kujumuika pamoja ili, wanaposikiliza Neno la Mungu na kushiriki Ekaristi, wafanye ukumbusho wa mateso, ufufuko na utukufu wa Bwana Yesu. Na pia watoe shukrani kwa Mungu “aliyewazaa upya katika tumaini lenye uhai kwa njia ya ufufuko wa Yesu Kristo katika wafu” (1Pet, 1:3). Kwa hiyo, siku ya Dominika ni Sikukuu ya kwanza ambayo ni lazima ielezwe vizuri na kuingizwa, kwa kadri inavyowezekana, katika maisha ya kidini ya Wakristo, ili iweze kuwa pia siku ya furaha na ya kuacha kazi. Maadhimisho mengine yasitiliwe mkazo sana, isipokuwa yale yenye umuhimu zaidi, kwa sababu siku ya Dominika ni msingi na kiini cha mwaka mzima wa Liturujia (SC. 106).
3. Fumbo na Mafumbo ya Kristo:
Imani ya Kikristo inaadhimisha Fumbo Kuu Moja la Pasaka, nalo ni Fumbo la Kristo, aliyeteswa, akafa, akazikwa na kufufuka. Kanisa linaendelea kuadhimisha Fumbo hili kwa njia tofauti. Fumbo hili lilianza kufunuliwa katika Agano la Kale; na linatimizwa kihistoria katika maisha ya kidunia ya Kristo, na lipo katika mafumbo ya kisakramenti.
Fumbo la Pasaka huadhimishwa katika mwaka kwa njia tofauti, lakini katika utaratibu ule ule wa Neno, mwili na kikombe cha Yesu Kristo. Awamu tofauti za maadhimisho zinalenga kutufanya tuelewe vizuri Fumbo hilo. Katika uwezo wetu mdogo wa kibinadamu na kisaikolojia, hatuwezi kulielewa na kuliadhimisha hilo Fumbo kwa wakati mmoja na kuchota utajiri wa neema ya Fumbo hilo la Kristo”, kwa hivyo, Mwaka wa Liturujia unatupa muda wa kutosha wa kuliadhimisha na kuchota neema zake.
Kwa muktadha huu, katika kila Misa kuna Majilio, Noeli, Epifania, Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu, Pentekoste, Pasaka, Kupaa, na Watakatifu wote. Kwa hiyo, Mwaka mzima wa Kanisa ni Fumbo Moja, “ Sakramenti Paschale ” ambalo huadhimishwa kila Dominika.
Kutoka hili Fumbo Kubwa la Pasaka, linajigawa katika mafumbo kadhaa yanayorejelea matukio tofauti katika maisha ya Kristo, na ni ushiriki na ukuzaji wa Fumbo moja pekee la Pasaka, ambalo huanza kutoka Usiku Mtakatifu wa Ufufuo hadi wakati wa Pasaka hadi Pentekoste, Wiki Takatifu, Kwaresima, Wakati wa Kawaida, Majilio, Noeli hadi Epifania na Sikukuu mbalimbali.
Itaendelea toleo lijalo.