DAR ES SALAAM
Na Alone Mpanduka
Mbio rasmi za kwanza za baiskeli zilifanyika mnamo 1868 huko Ufaransa. Mnamo mwaka 1885, baiskeli za usalama zilitengenezwa huko Coventry, Uingereza, binamu wa karibu wa baiskeli ya leo. Uendeshaji baiskeli ulianzishwa katika Olimpiki ya kwanza ya kisasa mwaka wa 1896. Mnamo 1903, Maurice Garin alishinda Tour de France ya kwanza, ambayo ilijumuisha maili 1,450 katika hatua sita. 1 Mei 2024.
Kulingana na rekodi za kihistoria, asili ya baiskeli ina mizizi yake katika bustani ya Palais Royal huko Paris, Ufaransa. Mnamo mwaka wa 1791, mtu mmoja aitwaye Comte de Sivrac alionekana akiwa amepanda kitu chenye magurudumu mawili kilichofahamika kama ‘celerifere’.Ikumbukwe kuwa usafiri mkuu wa miaka hiyo ulikuwa ni farasi.
Lakini, ikumbukwe pia kwamba mashindano ya kwanza kabisa ya baiskeli yenye mvuto duniani yalianzia nchini Ufaransa, yakifahamika kama Tour de France.
Ilikuwa ni Novemba mwaka 1902, ambapo Mkurugenzi wa gazeti la michezo la L’Auto, Henri Desgrange, alikuwa akitafuta njia ya kulishinda gazeti la Le Vélo kwa mauzo. Géo Lefèvre, mwandishi chipukizi wa gazeti la L’Auto alitoa pendekezo hili: “Kwa nini tusianzishe mashindano ya baiskeli kote nchini Ufaransa?”
Mwanzoni, wazo hilo lilionekana kuwa lisilowezekana. Hata hivyo, punde si punde likaanza kupamba moto. Alasiri ya Julai 1, 1903, saa 9:16 kamili, jijini Paris, waendeshaji 60 stadi na wengine, wakaanza mashindano yanayoitwa Tour de France ya majuma matatu yenye umbali wa kilometa 2,428.
Mara moja mashindano hayo yakawavutia watu wengi. Mashabiki wengi walikuja kutoka sehemu zote za Ufaransa ili kuwatazama na kuwashangilia washindanaji hao ambao Albert Londres, mwandishi wa habari wa Ufaransa, aliwaita “watumwa wa barabara.” Kwa kweli, katika miaka michache ya kwanza, mashindano hayo hayakuwa rahisi kwa sababu vifaa vilikuwa duni, barabara zilikuwa na mashimo, mikondo ilikuwa mirefu sana, na mara nyingi mikondo hiyo ilianza usiku.
Hatua kubwa ilipigwa kufikia mwaka wa 1919, wakati ambapo mshindi wa jumla wa kila siku alitunukiwa jezi la pekee la rangi ile ile ya kurasa za manjano za gazeti la L’Auto, yaani lile jezi la manjano ambalo hupendwa sana.
Mnamo mwaka wa 1931, Desgrange alibuni gari la matangazo ambalo liliwatangulia washindanaji kwa saa moja likiwachochea mashabiki barabarani, ili kulipia gharama za mashindano hayo.
Mauzo ya Gazeti la L’Auto, ambalo sasa linaitwa L’Équipe, yakapanda. Mwaka wa 1903, nakala 130,000 za toleo la pekee lililochapishwa dakika saba baada ya kufika kwa Maurice Garin, mshindi wa mashindano ya kwanza ya baiskeli nchini Ufaransa, zilinunuliwa mara moja kutoka kwenye vibanda vya kuuzia magazeti.
Siku hizi, kwa sababu mashindano hayo huonyeshwa kwenye televisheni katika nchi zaidi ya 150, mashindano hayo ya Ufaransa yanashikilia nafasi ya tatu kati ya mashindano ya michezo, ambayo husambazwa sana na vyombo vya habari, nafasi za kwanza mbili zikichukuliwa na Michezo ya Olimpiki, na Kombe la Dunia la Soka.
Mashindano hayo yamewavutia watu wengi sana hivi kwamba mwaka wa 1987 wabunge wa Hispania walikatiza mjadala wao ili kutazama ushindi wa mwananchi mwenzao Pedro Delgado akipiga zile kona kali 21 katika mkondo mgumu wa kupanda milima ya Alpe d’Huez.