Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

Kibamba: Parokia inayotoa Msaada Kisheria, huduma kiafya bila malipo

Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo- Kibamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. (Picha na Mathayo Kijazi) Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo- Kibamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. (Picha na Mathayo Kijazi)

DA ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Msemo wa ‘Mtoto umleavyo, ndivyo akuavyo,’ una maana kubwa katika familia na jamii kwa ujumla.
Licha ya kwamba wengi wanadhani kuwa hayo ni maneno ya wahenga tu hayana maana yoyote, lakini ukweli ni kwamba kuzingatia malezi kwa watoto, ni jambo la msingi sana.
Tukitazama katika Taifa la Tanzania na Mataifa mengine duniani, kila mtoto ana tabia yake, lakini kwa undani, utaona kwamba tabia hiyo imetokana na malezi aliyoyapata kutoka wazazi au walezi wake.
Hivi karibuni gazeti Tumaini Letu lilipiga hodi katika Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, kufanya mahojiano maalum na uongozi wa Parokia kuhusu mwenendo wa Parokia hiyo.
Pamoja na mambo mengine, wazazi wanaendelea kukumbushwa kutimiza wajibu wao katika suala zima la malezi, ili kuwajenga kimaadili watoto wao.
Padri Prijo Joseph, Paroko wa Parokia hiyo anasema kuwa wazazi wamepewa tunu au malaika, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kwamba malaika hao huko mbeleni hawabadiliki.
Wazazi kutokupata muda wa kutosha kukaa na watoto wao ili kupima tabia zao, imetajwa pia kwamba ni moja ya mambo makubwa yanayosababisha watoto kupoteza mwelekeo katika suala la maadili.
“Ni kutokana na changamoto za wazazi za kutokupata muda wa kukaa na watoto wao na kupima tabia zao, ndipo wengi hawafuatilii maedeleo ya kiroho ya watoto wao, badala yake, wanafuatilia tu maendeleo ya masomo ya shuleni, lakini mambo ya Mafundisho ya Kipaimara au Komunio, hawafuatilii.
“Kwa hiyo, tunaona vijana wengi wanakuja kanisani, lakini ukiwaambia wabaki kidogo kwa ajili ya semina au tafakari, unawaona wachache tu, wengine wanakimbia. Kwa hiyo, kama wazazi wangekuwa makini kuwahimiza watoto wao washiriki, basi wangeshiriki kwa wingi, kwa sababu mtoto akipata mafundisho ya imani, hawezi kuharibikiwa katika maisha yake, kwani atakuwa na hofu ya Mungu, atakuwa na moyo wa kutubu dhambi, na atakuwa msaada mkubwa kwa Parokia na Kanisa baadaye,”anasema Padri Prijo.
Padri huyo anaendelea kuwahimiza wazazi kwamba pamoja na jitihada zao za kuwasomesha watoto katika shule na vyuo, lakini pia ipo haja ya kuyaangalia maendeleo yao ya kiroho, kwani hata walioko vyuoni, baadhi yao hawaendi kanisani.
Licha ya changamoto hiyo katika malezi, Padri Prijo anawapongeza Waamini wa Kibamba kwa kuwa na mwitikio mzuri, kwani kunapokuwa na vikao, watu wengi hushiriki.
“Mwatikio wa Waamini katika Parokia hii ya Kibamba ni mzuri kwa kila jambo, kwani kukiwa na kikao au semina, watu wanajitahidi kuja kwa wingi;
“Lakini pia hata katika mafungo mwitikio ni mzuri sana. Sijawahi kupata shida na Waamini wa hapa, hasa katika masuala ya imani, hata katika mwitikio wa ibada za Misa na hasa kipindi cha Sikukuu wanajitahidi kuja kanisani,” anasema Padri Prijo.
Padri Prijo anasema kwamba Waamini wanatakiwa  kuendelea kujikita katika imani kama wanavyojipanga katika maisha ya kimwili, kwani imani ya mtu ndiyo inayomfanya asonge mbele.
Mwenendo wa Vyama vya Kitume:
Padri Prijo anasema kwamba ni mzuri, na mara kwa mara hukutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusu vyama vyao ikiwemo kuvifanya viendelee kuwa hai.
“Lakini Viongozi kwa upande wao wanajitahidi, na vile vile chama cha Vincent wa Paulo, VIWAWA, na Utoto Mtakatifu. Chama cha Vincent wa Paulo mara kwa mara hapa wana utaratibu wa kugawa misaada kwa wahitaji,” anasema Padri.
Kutokana na idadi ndogo ya wanaume wanaoshiriki katika mambo mbalimbali ya Kanisa, Padri huyo anawasisitiza wanaume hao kwamba pamoja jitihada za kutafuta riziki kwa familia zao, bali pia wajitahidi kutenga muda kwa ajili ya kumkumbuka Mungu katika maisha yao.
Mambo ya kuwainua watu kimwili:
Akizungumzia mambo waliyoyafanya ya kuwainua watu kimwili tangu Parokia kuanzishwa, Katibu wa Parokia hiyo, Victor Rweyongeza anasema kuwa wameanzisha Msaada wa Kisheria bure, huduma za afya bila malipo, Semina za Afya ya Akili, uokoaji katika majanga ya moto, ambapo yote yanaratibiwa na Christian Professionals of Tanzania (CPT), yaani Wanataaluma Wakristo Tanzania ambao ni Waamini wa Parokia hiyo.
Katibu huyo anasema kwamba wamefanikiwa pia kuanzisha misaada kwa wahitaji kupitia Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo kila mwezi, Pasaka, Noel, pamoja na Sherehe ya Parokia.
Pia, Katibu anasema kuwa Parokia hiyo hufanya semina za ujasiriamali na kujitambua kupitia tafakari za vijana siku za Dominika.
Kuhusu mambo waliyoyafanya ya kuwainua watu kiroho tangu Parokia imeanzishwa, Katibu huyo anasema kuwa Misa siku za Dominika zimeongezeka kutoka moja hadi tatu, Kuabudu Ekaristi Takatifu kila siku ya Alhamisi, pamoja na kujenga moyo wa Ibada, Liturujia.
Pamoja na hayo, anasema kuwa ushiriki katika Mafungo, Semina na Makongamano, ni mzuri, hasa kwa vijana na watoto Kiparokia, Kidekania, Kijimbo, na hata Kitaifa.
Kwa mujibu wa Katibu, Parokia hiyo imepiga hatua katika mafundisho ya watoto, kuanzia chekechea hadi darasa la nne kupitia mpango wa MADIDO (yaani Mafundiho ya Dini Dominika), huku darasa la tano na la sita wakifanya mafundisho ya Komunyo na Kipaimara, na baada ya Kipamimara, watoto hao huingia katika mpango mwingine wa MADIBAKI (Mafundisho ya Dini Baada ya Kipaimara)
Katibu huyo alizungumzia pia kuhusu Logos, ambapo anabainisha kwamba Masomo ya Biblia kila mwaka yanachaguliwa, huku Waamini wakisoma, na kisha baadaye kufanya mitihani, na washindi katika mitihani hiyo hupewa zawadi siku ya Kipaimara.
Katika jitihada hizo za kuwainua watu kiroho, Parokia iliweka mikakati ya kupunguza uchumba sugu, huku ndoa zaidi ya 80 zikiwa zimefungwa ndani ya miaka miwili, yaani 2022 na 2023.
Aidha, Katibu Rweyongeza anasema kuwa Mapadre wanajitahidi kuzitembelea Jumuiya, ambapo kila wiki kuna Misa za Watakatifu Waombezi wa Jumuiya, huku Waamini katika Jumuiya hushiriki kwa pamoja.
Mipango ya kiuchumi, kijamii:
Akizungumzia mipango ya baadaye waliyo nayo kijamii na kiuchumi katika Parokia hiyo, Katibu Rweyongeza, anasema kuwa ni kuendeleza juhudi za kutoa huduma kupitia Vyama vya Kitume mbalimbali kwa kuzingatia karama zao, pamoja na kuanzisha shule na vyuo ili kutoa elimu bora.
Akizungumzia kiini cha eneo hilo kuanzishwa ujenzi wa kanisa, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia hiyo, Leonard Masige anasema kuwa ni kutokana na ongezeko la watu katika eneo la Kibamba lililoleta wito wa uinjilishaji, ndicho kikawa chanzo cha kuanzishwa kwa Parokia hiyo.
Mwenyekiti huyo anabainisha kuwa shauku ya kuwaleta watu karibu na Kristu, ndiyo ikawa sababu ya uwepo wa Parokia hiyo ambayo ilizaliwa kutoka Parokia ya Kibaha, kwani ilikuwa mbali kwa Waamini kuweza kupata huduma za kiroho.
Asili uasisi jina la Kibamba:
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Leonard Masige, neno Kibamba ni neno la Kizaramo lenye maana ya mmea unaofanana na mkonge ambao pia huitwa mkonge, pori. Mmea huo hupatikana mahali penye dalili za kichaka na bondeni kidogo.
“Chanzo cha Kibamba tulipo inaanzia eneo la Kibamba kwa Mangi ukitokea Kibaha upande wa kushoto, ukielekea bondeni kidogo kulikuwa na kichaka kidogo na kisima kidogo cha maji. Ilikuwa mtu akichota maji, akiulizwa amechota wapi, anasema ni pale kwenye Kibamba, na hapo ndipo ikawa chanzo cha jina Kibamba, lakini kabla ya hapo, inasemekana eneo lote hili la Kibamba lilijulikana Kibwegere,” anasema Mwenyekiti wa Parokia hiyo, Leonard Masige.
Changamoto zinazoikabili
“Sisi kwa kweli tunamshukuru Mungu, kwani hatuna tatizo la kurudi nyuma hadi sasa. Hii inatokana na mikakati mbalimbali tunayoifanya, hususani ushirikiano katika sala, kupitia Jumuiya Ndogo Ndogo, Kanda, na hata Parokia. Waamini wanashirikishwa katika kila kinachofanyika katika Parokia yao, na kweli wanayaona matunda ya kazi yao,”anasema Masige
Shughuli za kiuchumi Kibamba:
Kuhusu shughuli kubwa za kuwaingizia kipato chao Waamini wa Kibamba, Masige anabainisha kwamba Waamini hao wana shughuli nyingi za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kufanya biashara ndogo ndogo na kubwa, wakulima, wafugaji, waajiriwa wa taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, pamoja na wajasiriamali.
Anasema kuwa ushirikiano wao pamoja na watu wa imani nyingine, ni mkubwa, akiongeza kwamba wanatoa huduma mbalimbali kupitia Waamini ambazo zinatolewa kwa watu wote bila kujali imani zao, ikiwemo huduma ya afya bila malipo, pamoja na msaada wa kisheria.
“Kwa ujumla, ushirikiano ni mzuri sana. Tunashirikiana vizuri, mfano mzuri ni wiki hii tulikwenda kufanya uinjilishaji kwenye Kanisa la SDA Kwembe, ambapo kwaya yetu ya Mtakatifu Vincent wa Paulo ilialikwa kwenye ujirani mwema na kushiriki vizuri,” alisema Mwenyekiti.
Parokia ya Mtakatifu Vincent wa Paulo – Kibamba, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, inapatikana katika Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam, huku ikiwa na Waamini takribani 6,000, Jumuiya 103, Kanda 15, pamoja na Kigango kimoja cha Mtakatifu Fransisko Ksaveri.

Rate this item
(0 votes)

Leave a comment

Make sure you enter all the required information, indicated by an asterisk (*). HTML code is not allowed.