DAR ES SALAAM
Na Arone Mpanduka
Women Jazz Band ilikuwa bendi ya muziki wa dansi jijini Dar es Salaam, Tanzania. Bendi ilianzishwa mnamo 1965 ikiwa na wanawake tupu, lakini baadaye ilileta wanaume kwenye upande wa kupiga vyombo.
Mwaka 1965 kundi jipya la muziki la aina yake lilianzishwa Tanzania. Lilikuwa ni bendi ya akina mama watupu. Akina mama hawa, wengine wakiwa wafanyakazi wa Government Press, walijichagua na kuanza kuhudhuria mafunzo ya muziki chini ya yule mwanamuziki mahiri Mzee Mayagilo, aliyekuwa kiongozi wa shughuli za muziki katika Jeshi la Polisi.
Akina mama hawa wakawa chini ya kitengo cha Polisi Jazz Band, wakaanza kufanya mazoezi ya nguvu. Bendi hiyo ya akina mama ilikuwa chini ya ufadhili wa TANU Youth League.
Wakati wakianza shughuli hiyo, walikuwa hawana ujuzi wowote wa muziki. Kutokana na jitihada waliyofanya, taratibu wakaanza kufanya maonyesho yao, hasa kwenye hafla za Serikali na Chama tawala wakati huo.
Tarehe 31 Mei 1966, Women Jazz band iliingia katika studio za Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) na kurekodi nyimbo sita ambazo ni ‘Tumsifu Mheshimiwa’; ‘Leo Tunafuraha’, ‘Mwalimu Kasema’; ‘Women Jazz’; na ‘Sifa nyingi tuwasifu Viongozi na TANU yajenga nchi.’
Bendi hiyo iliundwa na Washiriki kama Mary Kilima (Mwimbaji); Juanita Mwegoha (Mwimbaji); Siwema Salum (Mwimbaji); Rukia Hassan (Mwimbaji); Kijakazi Mbegu (Solo Guitar); na Mwanjaa Ramadhan (Bass Guitar).
Wengine ni Chano Mohammed (Rhythm Guitar); Tatu Ally (Alto Sax); Mina Tumaini (Tenor Sax); Anna Stewart (Alto Sax); Rukia Mbaraka (Tenor Sax); Lea Samweli (Bongos, au Conga); Josephine James (Drums); Zainab Mbwana (Maracass); na Tale Mgongo (Timing).
Inaelezwa kuwa wazo la kuwa na bendi ya wanawake tupu lilianzia kwenye bendi ya wanawake ya Les Amazones De Guinee ya nchini Guinea kwa wakati huo.
Kipindi hicho, Rais wa Guinea ya Conakry, Sekou Toure alikuwa na tabia ya kuambatana na bendi yake hiyo katika ziara zake mbalimbali Barani Afrika, na nje ya Afrika.
Ndipo mwaka 1965, Rais huyo alipata fursa ya kufanya ziara nchini Tanzania na kuja na ndege iliyosheheni wasanii wengi wa kike kuliko wanasiasa, ambapo miongoni mwa bendi alizoambatana nazo kwenye msafara wake, ni ya Les Amazones.
Wakati walipowasili,baadhi ya mabinti wa TANU Youth League hapa nyumbani ndio walikuwa wenyeji wa wanamuziki hawa wa kike. Rais Sekou Toure na wasanii wake walipoondoka walikuwa wamepanda wazo la vikundi vya sanaa vya Taifa, na pia wazo la bendi ya wanawake.
Wanawake waliokuwa wakizunguka na wanamuziki wa kigeni, wengi wakiwa wanafanya kazi Government Press, waliazimia nao kuanzisha bendi ya wanawake, japo walikuwa hawana ujuzi wa chombo chochote cha muziki, lakini nia yao ilikuwa kuwa na bendi kama Les Amazones.
Women Jazz ilipata umaarufu kiasi cha kuanza kufanya safari nje ya Tanzania, na kuweza kufanya maonyesho Nairobi na Mombasa nchini Kenya, baada ya kutembelea miji kadhaa nchini Tanzania.
Wakati wa matayarisho ya kwenda China, kundi lilisambaratika. Kikubwa kilichosababisha hili ilikuwa ni wanamuziki kuona hawapati chochote kutokana na mapato yaliyotokana na muziki wanaoupiga.
Baada ya bendi kufa, TANU youth League ikachukua vyombo vyake na kuvihifadhi, hatimaye vyombo hivi vikawa ndivyo vyombo vilivyotumika kuanzisha Vijana Jazz Band chini ya Mzee John Ondolo, miaka kadhaa baadaye.
Vijana Jazz Orchestra ambayo ilikuwa inajulikana kama Vijana Jazz Band au Vijana Jazz) ilikuwa ni bendi ya muziki wa dansi ya Kitanzania iliyofikia kilele cha umaarufu katika miaka ya 1980.
Kama ilivyokuwa kwa bendi nyingi za dansi za enzi hizo, ilifadhiliwa na taasisi ya Serikali, yaani Umoja wa Vijana kupitia Tawi la Vijana la Chama Tawala cha Tanzania (TANU) kwa wakati huo.
Bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1971 na John Ondolo Chacha. Mnamo mwaka wa 1978, serikali ya Tanzania ilipitisha sheria iliyoruhusu bendi kununua ala za kigeni (jambo ambalo hapo awali lilikuwa limekatazwa na Baraza la Muziki la Taifa (BAMUTA), baraza la serikali linalohusika na udhibiti wa biashara ya muziki).
Vijana Jazz ilikuwa mojawapo ya bendi za kwanza kuchukua fursa hii, na katika miaka ya 1980, ilipata umaarufu mkubwa kwa sababu ya sauti yake ya ubunifu iliyotumia sanisi na mashine za ngoma.
Mitindo maarufu (styles) iliyobuniwa na Vijana Jazz include sindimba, heka heka, koka koka, watoto wa nyumbani, na pamba moto. Baadhi ya wanamuziki mashuhuri waliowahi kutamba katika Vijana Jazz ni Hamza Kalala, Hemedi Maneti, Issa Chikupele na Manitu Musa.