Dar es Salaam
Na Arone Mpanduka
Kuimba ni kutamka maneno katika hali ya kimuziki, au pia twaweza kusema ni kutamka maneno moja baada ya jingine kwa sauti yenye lahani (sauti ya ala ya muziki,tyuni) au ghani (melodi).
Mwimbaji ni mtu yeyote mwenye uwezo wa kuimba kwa sauti yake bila kutumia vyombo vya muziki.
Ikumbukwe pia kuwa katika vikundi vya uimbaji, wapo wale wanaoongoza wengine katika uimbaji (lead singers), na wengine kazi yao ni kuitikia (backing singers).
Kuna mitindo mbalimbali ya uimbaji. Wengine wanaimba huku wamesimama wima, wengine wanaimba huku wamekaa, na wengine wanaimba huku wakionesha ishara mbalimbali kwa mikono, miguu yao,au vyote viwili.
Mitindo ya uimbaji ni mizuri iwapo tu inasaidia kufikisha ujumbe kwa wahusika. Huduma ya uimbaji siyo “show.”
JINSI YA KUPATA WIMBO/MADA MPYA
Watu wengi wanapenda vitu vipya,mathalan kiatu kipya, gauni jipya, nyumba mpya,vyombo vipya, n.k. Vivyo hivyo, watu wanapenda kusikia nyimbo mpya. Lakini je, ni rahisi kwaya au watunzi wa nyimbo kutunga nyimbo mpya kila mara?
Mambo yafuatayo yanaweza kukusaidia kupata nyimbo au mada mpya.Ukisikia sauti ya wimbo (melody) moyoni mwako, fanya haraka kuirekodi kwenye kanda (kama una radio cassette na microphone au simu).ili usisahau.
Njia nyingine ni kusoma sana vitabu mbalimbali vya kisiasa, kiuchumi na historia za ndani na nje ya nchi, ili vikupe uelewa mpana wa kuimba maudhui unayoyataka.
Pia, unaweza kuwa mdadisi wa mambo kwa kuuliza wajuzi mbalimbali, na kufuatilia vyombo vya habari kuhusiana na yale yanayoendelea kujitokeza kila siku.
Wimbo unaweza kuwa na mada (topic) moja au zaidi. Lakini wimbo wenye mada moja ni mzuri zaidi. Kwa nini?
Wimbo wenye mada moja mara nyingi unaanza kwa utangulizi,baadaye unaelezea mada yenyewe, na kisha unatoa hitimisho.Kwa hiyo ni rahisi kukumbuka ujumbe wa wimbo huo.
Pia, hakikisha unakuwa na ufafanuzi wa kutosha. Beti 3 au 4 zinaweza kuzungumzia mada moja tu kwa kuifafanua. Mada ya wimbo inaweza kumlenga mtu mmoja au watu kadhaa.
Nyimbo nyingi zinaangukia katika makundi mbalimbali, kama vile nyimbo za mafundisho/maonyo, Nyimbo za Faraja, Nyimbo za Mahubiri,
Nyimbo za siasa, nyimbo za uchumi na nyimbo za kuburudisha ambazo ndani yake zinaweza kukosa ujumbe sahihi, lakini zikaishia kuwa na midundo mizuri kwa lengo la kusherehesha.
VYAKULA NA VINYWAJI KWA MWIMBAJI
Vilaji na vinywaji visivyofaa kabla ya kuimba, ni muhimu ili kuepuka kuimba tumbo likiwa tupu kabisa. Kuimba ni kama riadha, inahitajika nguvu kwa ajili ya utendaji wako. Hata hivyo, ni muhimu pia kuepuka kuimba tumbo likiwa limeshiba sana.
Kumbuka kuimba ni kazi ngumu, unahitaji mafuta (you need fuel), hivyo inashauriwa kuwa na mlo wa kawaida wa saa moja au mbili kabla ya uimbaji.
Kulingana na mazoea yetu, vipo vyakula na vinywaji ambavyo ni vigumu kuachana navyo ghafla, mengine huchukua muda.
VYA KUZINGATIA UWAPO STUDIO YA MUZIKI
Mosi; Usikimbilie kwenye chumba cha kurekodia kabla hujawa tayari. Kusimama studio ili kurekodi inaweza kuwa ya kukatisha tamaa kwa waimbaji wapya. Hivyo, fanya mazoezi sana kabla ya kurekodi.
Pili; Jaribu kujirekodi mwenyewe kabla ya kuingia studio, na sikiliza kujua kile ulichokipenda, na kusahihisha usichokipenda. Chagua funguo sahihi ili kuweza kufikia nota za juu kwa wepesi, mbinu zako za kiuimbaji zinatakiwa kuwa nzuri kiasi cha kuzuia kupoteza muda katika studio kwa kurekodi mara nyingi, na kutumia tyuni nyingi.
Tatu; tumia vizuri microphone katika kuimba. Katika studio hakikisha kunakuwa na umbali fulani kutoka mdomoni mwako hadi kwenye microphone. Waimbaji wenye uzoefu mdogo kwenye microphones hujikuta wakiyumbisha vichwa vyao, kitu ambacho kinaweza kuharibu ubora wa sauti.Sogea karibu na microphone sauti inapokuwa ndogo, na mbali inapokuwa kubwa. Hii itakusaidia kuondoa tofauti ya kupanda na kushuka kwa sauti.
Nne; Epuka kusisitiza maneno yenye P na B ambayo mara nyingi huzalisha sauti yenye popp. Pia weka msisitizo kwenye maneno yenye F na S.
Tano; Dhibiti sauti za pumzi (kuhema kwa sauti). Kudhibiti sauti za pumzi wakati wa kurekodi itasaidia kuondoa usumbufu wakati wa kuhariri sauti.
Sita; Kabla hujaanza kurekodi, jaribisha aina tofauti za microphone kuona ni ipi inayofaa. Unaweza kurekodi ubeti mara kadhaa, na kusikiliza ipi inayofaa.