DAR ES SALAAM
Na Arone Mpanduka
Raha za michuano ya soka ya Mataifa ya Afrika (Africa Cup of Nations: AFCON) zitarejea tena kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 mwakani, huku Tanzania Ikiwa miongoni mwa washiriki tunaotarajiwa, ukiwa ni ushiriki wetu wa tatu tangu fainali hizo zilipoanzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1957.
Tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo, kumekuwa na matukio kadhaa ya kukumbukwa kuwahi kutokea.
Yapo matukio ya huzuni, furaha na ya kustaajabisha ambayo yamewahi kutokea katika fainali hizo tangu kuanzishwa kwake.
AJALI YA CHIPOLOPOLO MWAKA 1993
Aprili 27 mwaka 1993 timu ya taifa ya Zambia, maarufu kama Chipolopolo, ilikuwa safarini kwenda nchini Senegal kucheza mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia. Ndege iliyowabeba ilianguka na kutumbukia katika bahari ya Atlantic mita 500 tu iliporuka kutoka mji wa Libreville, Gabon. Wachezaji wote waliokuwa kwenye ndege hiyo, walifariki dunia.
Mwaka mmoja baadaye, Zambia ilijijenga vyema kwa kuunda wachezaji wengine na kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Mataifa Huru ya Afrika ya mwaka 1994. Walifika fainali ingawa walifungwa na Nigeria kwa mabao 2-1. Yalikuwa ni mafanikio makubwa licha ya changamoto iliyowakumba mwaka mmoja uliotangulia.
JEZI ZA CAMEROON
Mwaka 2002 katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyofanyika nchini Mali, timu ya taifa ya Cameroon ilichukua Kombe la AFCON kwa kuifunga Senegal katika fainali kwa mikwaju ya penati 3-2, baada ya timu hizo kutoka suluhu ya kutokufungana.
Lakini habari kubwa ya Cameroon ilikuwa ni kuhusu jezi zao.Timu hiyo ilienda katika mashindano na jezi zilizokuwa katika mtindo wa ‘singlets (vests)’, jezi ambazo baada ya mashindano, Shirikisho la Soka la Kimataifa (Federation of International Football Association: FIFA) walizipiga marufuku.
Mwaka 2004 tena, Cameroon ilitinga katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Tunisia ikiwa na jezi za ajabu zaidi zikiwa kwenye mtindo wa ‘Jump Suti’, yaani fulana na bukta zimeshikana. Fifa hawakukubali, wakawakataza mara moja kuacha kutumia jezi hizo, na kuwapiga faini ya dola 154,000 za Kimarekani, ambazo zililipwa na watengenezaji wa jezi hizo - kampuni ya Puma.
BASI LA TOGO KUSHAMBULIWA MWAKA 2010
Basi la timu ya taifa ya Togo lilishambuliwa na watu wenye silaha wakati timu hiyo ilipokuwa ikielekea mashindanoni nchini Angola.
Tukio hilo lilitokea Januari 8 mwaka 2010 wakati basi la timu ya Togo likisafiri kutoka Togo kwenda Angola ambako fainali hizo zilifanyika, watu watatu waliuawa, akiwemo mchezaji mmoja.
Nyota wa Arsenal kwa wakati huo, Emmanuel Adebayor, alikuwa ni miongoni mwa waliokuwa kwenye basi hilo, na kwa hasira akatangaza kutoichezea tena timu hiyo akishutumu uzembe wa Chama chake cha Soka kuwasafirisha kwa basi, badala ya ndege.
DROGBA ASULUHISHA AMANI
Mshambuliaji wa Ivory Coast, Didier Drogba alikuwa mahiri sana uwanjani kwa timu yake ya taifa ya Ivory Coast, na klabu wakati huo akiicheza timu ya Chelsea ya Uingereza, na pia alitumia hadhi yake kufanikisha amani nchini mwake.
Wakati wa vita kati ya 2002 na 2007, alipiga magoti moja kwa moja kwenye luninga akiwa na wachezaji wenzake kuwahimiza waliokuwa wanapigana kuweka silaha chini.
Amani ilitawala, na mwaka 2008 alisisitiza mechi ya kufuzu Kombe la Afrika ichezewe kwenye ngome ya zamani ya waasi, Bouake, kama wito kwa raia kuungana.
Mwaka 2006 na 2012, Drogba alisaidia taifa lake kufika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, lakini wakashindwa kwa mikwaju ya penati.
EBOLA MWAKA 2015
Mwaka 2015 kupitia msemaji wao, Mohamed Ouzzine, Morocco walisema kuwa kutokana na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (World Health Organization: WHO), hawataweza kuandaa mashindano hayo kutokana na kuenea kwa kasi virusi vya ebola, ugonjwa uliokuwa unasambaa kwa kasi huko Afrika Magharibi.
Baada ya Morocco kujitoa kuandaa, mashindano hayo yalihamishiwa nchi ya Equatorial Guinea.
AFCON 2021 BADALA YA 2022
Fainali hizo za Cameroon ambazo zilifanyika mwaka jana na Senegal kuwa bingwa, zilikuwa zikiitwa AFCON 2021 licha ya kufanyika mwaka 2022 kwa sababu maandalizi yake yalilenga mashindano kufanyika mwaka 2021.
Ilishindikana kufanyika katikati ya mwaka 2021 kwa sababu katika kipindi hicho, Cameroon ilikuwa na majira ya mvua kubwa na mafuriko, hivyo Shirikisho la Soka Afrika (Confederation of African Football: CAF), likasogeza mbele.