DAR ES SALAAM
Na Joseph Mihangwa
Mzungu hajakubali kuwa bin-Adam wote ni sawa, wala kwamba wote ni wa baba mmoja, Adam. Pamoja na kwamba alituletea Msahafu wa Dini, yaani Biblia wenye kusisitiza “upendo”, hiyo ni ghiliba tupu kwa sababu inawabagua wana-Adam kati ya walio wana wa Taifa teule la Mungu [Israeli] na wana wa Mataifa yasiyo teule. Huko ni kukweza ngozi nyeupe.
Kwa kutumia Mungu wa kujiundia [Yahweh] na Msahafu wa kibeberu, wanaidhinishwa kutugeuza watumwa wao, eti kwamba: “Na wageni watakuwa watumwa wa kulisha mifugo yenu; na wana wa Mataifa watawalimia na kutunza mashamba ya mizabibu yenu”. Huo ndio ubaguzi wa ubeberu wa kimataifa ambao umedumu hadi leo.
Ubaguzi huo kwa misingi ya rangi ulioasisiwa, kusimikwa na kukomazwa Kimataifa na Mjerumani Johann Friedrich Blumenbach [1752 – 1840], unawagawa bin-Adam kwa viwango vya ubora katika makundi sita ya Watu weupe [Coucassians] kama daraja la kwanza; Wamongolia [Mongoloid] daraja la pili; Watu weusi [Ethiopoid]; Wamarekani wenye asili ya Kihindi [Red Indians] na Wahimalaya [Malayans] kama daraja la mwisho kwa ubora.
Wamefika mbali kwa kudai kuwa Mwafrika si Mwana-Adam, yaani hakuzaliwa na Adam. Dhana hiyo mpya inayoitwa ‘Pre-Adamisma’, inadai kuwa Mwafrika alikuwepo kabla ya kuumbwa Adam, na alikuwa kiumbe asiye na roho.
Mwasisi na Mwenezi wa dhana hiyo inayoshika kasi kipindi hiki cha utandawazi, ni Mfaransa Isaac La Peyrere [1596 – 1676]. Dhana hiyo inapinga usahihi wa Biblia juu ya uumbaji, ikidai kuwa kulikuwa na watu kabla ya kuumbwa kwa Adam na Hawa.
Anadai kwamba kulikuwa na uumbaji mbili za watu: uumbaji wa kwanza ulikuwa wa dunia nzima na Mwafrika kama mtu wa kwanza; na uumbaji wa pili ulihusu Wayahudi kama Taifa ambalo Adam alikuwa mkuu wake.
Anadai kuwa, Mataifa yote hayatokani na Nuhu, kwamba watu wa Mataifa [wasio wa Taifa teule] hawakutenda wala hawahusiki na dhambi ya asili kwa sababu walikuwepo kabla ya Adam, na hivyo hawakupokea “Sheria” au Maagizo ya Mungu, bali ni Adam na uzao wake pekee. Chini ya dhana hiyo, Wazungu ni Wana-Adam, na Mwafrika, siye.
Dhana hii ina watetezi wengi miongoni mwa Mataifa ya Ulaya: Mathew Fleming Stephenson, katika kitabu chake “Adamic Race” anasema, “Mungu alitumia mamilioni ya miaka kuumba mtu duni [Mwafrika] kabla ya kuumba mtu bora aina ya Mzungu [Caucasian] juu yake”. Wengine, kwa kutaja wanataaluma wachache tu, ni pamoja na John Harris [The Pre-Adamite Race], Isabelle Duncan [Adamites and Pre-Adamites], na wengine.
Iwe ni kwa mtizamo wa dhana ya “Pre-Adamite”, “Uumbaji” au “Mageuko” [evolution], hakuna ubishi mpaka sasa, kwamba binadamu [mtu] wa kwanza aliishi Loliondo/Ngorongoro zaidi kabla ya mwaka 10,000, Kabla ya Vizazi [KV], ambao ndio mwaka unaosemekana Adam aliumbwa.
Ustaarabu wa mtu huyu ulianza na shughuli za kilimo, ufugaji, ibada na makazi, eneo ambalo sasa linajulikana kama Nubia, au Sudan Kaskazini. Utawala wa kwanza ulianzia Ta-Seti, eneo hilo watu hawa walijulikana kama “Anu”.
Nchi waliyokalia ilijulikana kwa majina mengi, kama vile, Nubia, Kermet, Kush, Ethiopia au Egypt [Misri], na Mji Mkuu ulikuwa Kerma. Nubia imetajwa kwenye Biblia, Kitabu cha Mwanzo 2:11 kama nchi ya Havillah.
Ni Ufalme ulioundwa na watu weusi kutoka eneo la Maziwa Makuu [ANU] miaka ya 5900 Kabla ya Vizazi [KV], na maelfu ya miaka kabla ya Kisto [KK]. Hapa ndipo Gharika [la Nuhu] lilipowakuta watu hawa, wakaangamia, isipokuwa mtu mmoja – Nuhu na wanae watatu – Yafeti, Shem na Hamu. Hiyo ilikuwa Mwaka 5000 KK.
Wakati ardhi ilipoonekana kutotosheleza familia za ukoo huu ulioendelea kupanuka, Nuhu akawagawia wanawe maeneo ya kutawala: Yafeti alipewa eneo lote la nchi ya Kaskazini ya Dunia, yaani Ulaya yote; Shem maeneo yote ya Mashariki ya Kati na Asia, wakati Ham aligawiwa eneo lote la Bara la Afrika na Marekani Kusini. Ifahamike kuwa wote hawa walikuwa watu weusi kipindi hicho kabla ya koo zao kubadilika rangi maelfu ya miaka baada ya kuhamia nchi mpya.
Ham na ukoo wake alijijengea himaya ya Kikemeti yenye nguvu kiuchumi, Kijeshi na Kitheolojia kwa imani ya Kikemeti iliyotambua uwepo wa Mungu mmoja [Baba].
Mkanganyiko wa kidini na kitheolojia kati ya Mwafrika na Mzungu, unaanza na mtu mmoja aliyeitwa Abraham kutoka Mesopotamia [Ur], aliyeoteshwa ndoto na Mungu wake akielekezwa kwenda [kutafuta makazi] Kanaani, nchi ya Mwafrika aliyeitwa Kanaani, mwana wa Ham na mjukuu wa Nuhu.
Kutoka Kanaani, akaenda Misri Mwaka 1871 KK wakati mtu mweusi alikuwa mtawala na kurejea tena Kanaani, akanunua shamba kutoka [Ephron] ukoo wa Hiti [Wahiti], mwana wa pili wa Kanaani, na kufanya makazi [Mwanzo 23:1-20; 25: 7-10].
Wakati Abraham akiondoka Ur [kwa kukosana na mtawala wa eneo lake] Mesopotamia, ilikuwa chini ya himaya ya utawala wa Mwafrika aliyeitwa Nimrodi, mwana wa Kush na mjukuu wa Ham. Dini na theolojia iliyoongoza huko ilikuwa ya Kikemeti/Kiafrika kutoka Nubia/Afrika. Abraham alikuwa wa uzao wa Nmrod, kwa hiyo alikuwa Mwafrika na alikimbilia Kanaani na Misri kwa watu weusi wenzake.
Musa alikuwa mtu mweusi, la sivyo asingelelewa kwa Farao mweusi, na hatimaye kupewa madaraka ya kitawala kabla ya kukimbilia Nubia/Ethiopia kwa tuhuma za kuua raia. Huko alioa mke wa Kikushi aliyeitwa Tharbis, mweusi tii, wakapata watoto.
Kutoka ukimbizini Nubia/Ethiopia akaenda Midiani, akafikia kwa Kingozi wa eneo hilo, Mzee Yethro aliyepata kuwa Mshauri wa Farao miaka ya nyuma. Akamuoa Ziporah, binti wa Yethro, mweusi tii kama alivyokuwa Tharbis wa Nubia. Akawa na wake wawili wakiishi mbali mbali. Hawa aliwakusanya na kwenda nao Kanaani.
Yethro alikuwa mtu mweusi wa ukoo wa Abraham kwa mke wa mjomba wake, Keturah. Na Musa angekuwa Mwisraeli [wa Taifa teule] asingeoa wake wa Kiafrika – Tharbis na Ziporah.
Wanaofikiriwa kuwa “Waisraeli” aliwaongoza kutoka Misri kwenda kuvamia Kanaani ya Wakanaani, hawakuwa Waisraeli kwa maana halisia, wengi walikuwa weusi hasa wale wa uzao wa wake za Yakobo, Leah, Raheli, Zilpha na Bilha ambao walikuwa Wakush/Wanubia kwa asili.
Na hii inajieleza wazi kuwa walioongoza maasi jangwani dhidi ya Musa walikuwa wenye asili ya Nubia/Afrika, akiwamo On [Anu] mwana wa Paleth na mmoja wa Wakuu wa kabila la Reuben, mtoto wa kwanza wa Yakobo kwa Leah.
Wengine walikuwa ni Korah [mtoto wa tatu wa Esau kwa mke wa Kikanaani, Aholibamah]; Dathan na Abiram, wote wana wa Eliab, waliendesha mgomo kupinga uvamizi wa Kanaani uliokusudiwa na Musa na washirika wao wachache wenye nia ovu.
Mazungumzo ya Musa na Mungu wa jamii ya Kiyuda yenye lengo la kujikweza ambapo inadaiwa alipewa amri kumi, ndicho chanzo cha ubaguzi wa kikabila na kitheolojia uliojenga ubeberu wa Taifa moja dhidi ya mengine. Ni nani mwenye uhakika juu ya usahihi wa dhana ya “Mungu wa Israeli” dhidi ya Mataifa mengine sawa tu na dhana ya “Pre-Adamism?”
Wanaakeolojia wanatuambia kuwa, dunia iliumbwa miaka bilioni 13 iliyopita; Adamu aliumbwa Mwaka 10,000 KV, na Wanahistoria wanasema mwaka huo [10,000], tayari Mwafrika alikuwa ameenea sehemu zote za Ulaya, Asia, Australia na Marekani Kusini.
Waafrika hao walisambaa kutoka Loliondo/Ngorongoro hadi Nubia na kuenea duniani kama ifuatavyo: Miaka 100,000 iliyopita, walijaza Palestina, Israeli na Yemen; Miaka 65,000 iliyopita wengine walitumia mkondo wa Bahari ya Atlantiki, wakaingia Amerika ya Kusini.
Miaka 50,000 iliyopita, wengine walitokea Kusini Mashariki ya Bara la Asia wakawasili Australia, wakajaza Visiwa vya Pasifiki mpaka Hawaii. Na Miaka 40,000 iliyopita wakaingia nchi za Skandinavia na Uingereza.
Wanahistoria na Wanafalsafa nguli wa kale, Flavius Josephus [37 – 86 BK], Lucius Plutarchus [46 – 119 BK], Publius Tacitus [56 – 120 BK], Eusebius Pamphilus [260 – 339 BK] na Diodurus Siculus [90 – 20 KK] walioishi kabla ya Torati [Diodurus] na Kabla ya Biblia ya Agano Jipya kuandikwa [78 BK], wanakiri kuwa Waebrania asilia walikuwa ni kikundi cha Wanubi/Wakush waliolazimika kuhama Nubia/Kush/Ethiopia kwa miguu kwenda nchi ya Kanaani, aliyotawala Kanaan, mwana wa Ham na mjukuu wa Nuhu. Ilikuwa nchi ya Waafrika eneo la Afrika Kaskazini Mashariki.
Hii ndiyo nchi ambayo Abraham aliishi kwa miaka 100 na kumuoa Hajir, Mkushi [Mwanzo 15:3]. Mipaka ya nchi hiyo Kanaani na ukoo wake waliishi na kutawala, kwa mujibu wa Mwanzo 10:19] ilikuwa “kutoka Sidoni hadi Gerari hata Gaza; Sodoma na Gomora, na Adma, na Seboimu hadi Lasha na Afrika Mashariki yote.”
Ham ni Mwafrika kwa mujibu wa Biblia. Mwanae [Kanaani] hawezi kuwa mtu mweupe. Kush, mwana mwingine wa Ham, alitawala Sudani ambayo imo Afrika – ikijulikana wakati huo kama nchi ya Kush.
Misraim, mwana mwingine wa Ham, alitawala Misri ambayo imo Afrika [Zaburi 105:23 – 27]. Uzao wake ni wa Waafrika, si wa watu weupe.
Phut, mwana mwingine wa Ham, alitawala nchi yote inayoitwa leo Libya. Kwa hiyo, ni wazi kuwa nchi na Mataifa yote yanayotajwa katika Biblia ni mali ya Afrika na Waafrika, na si ya Ulaya na Wazungu.
Mungu aliwekeza Loliondo/Ngorongoro siri na madhumuni ya uumbaji kwa utukufu wake. Uwekezaji mwingine hapo kwa uchu wa mali na wenye kufifisha kazi yake ni kufuru kubwa kwa wakfu.