Wiki iliyopita tuliwaletea historia ya mchango wa Kanisa wakati wa kupambana na athari ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1939-1945). Leo tunawaletea mrithi wa Papa Pio X11 (1939-1958: wa 260) ambaye ni Papa Yohana XX111, aliyepigiwa kura mara 12 kumpata. Sasa endelea.
Papa Yohana XXIII (1958 - 1963: wa 261), zilipigwa kura mara 12 kabla ya kumpata. Uchaguzi wa Papa wa kumrithi Papa Pio XII, haukuwa rahisi kama uchaguzi wake. Inasemekana kwamba kura zilipigwa mara 12 ili kumpata. Kulikuwepo na wengi ambao walidhaniwa wangemrithi, lakini sasa dunia ilihitaji zaidi Mchungaji kuliko Mtawala.
Papa Pio XII alikuwa labda Papa wa mwisho wa mapokeo ya kifalme. Katika hali ngumu ya kumpata mtu wa kukidhi mategemeo ya wote, walimchagua mtu wa mpito wakiwa wanajipanga vizuri.
Walimchagua mtu ambaye hisia zake zilikuwa za mkulima, mtu rahisi kuongea naye na kufikiwa. Umri wake, miaka 76, ulikuwa umekwenda, hivyo hakutegemewa kukaa muda mrefu.
Alichaguliwa Kardinali Angelo Ronccali ambaye alichukua jina la Papa Yohana XXIII. Kardinali Ronccali alikuwa na uzoefu wa kukutana na watu wa aina mbalimbali wa kutoka nchi mbalimbali.
Ni vema na haki kujua vizuri maisha ya Papa huyu aliyebadili mwelekeo wa Kanisa katika Ulimwengu wa sasa. Kinyume na mategemeo ya wote, alifanya kazi ambayo ilikuwa haijafanyika tangu Mtaguso Mkuu wa Trento katika karne ya 16.
Angelo Giuseppe Roncalli, mtoto wa tatu kati ya watoto kumi na watatu, alizaliwa tarehe 25 Novemba 1881 huko Sotto il Monte (Bergamo), kwenye familia ya wakulima. Alipadrishwa mwaka 1904, na akaendelea na masomo na kupata Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa.
Akiwa Katibu wa Askofu mpya wa Bergamo, Giacomo Radini –Tedeschi, Angelo alipigania haki za jamii, na baadaye alifundisha Seminarini Historia ya Kanisa, na masomo mengine. Wakati wa Vita Kuu vya Kwanza (1914-1918), mwaka 1915 alijitolea kama mhudumu wa kiroho (Chaplain) wa wanajeshi. Baada ya vita, alikuwa mlezi wa kiroho wa Seminari.
Mwaka 1921 aliitwa Roma na Papa Benedikto XV (1914-1922: wa 258) kusaidia kupanga upya Idara ya Uinjilishaji (Propaganda Fide). Mwaka 1925 alitumwa Bulgaria kama Mwakilishi wa Papa, na huko alijishughulisha na Makanisa ya Mashariki (Waortodosi). Mwaka 1934 alitumwa Uturuki na Ugriki, makao yake yakiwa Istanbul (Konstantinople ya zamani).
Huko, licha ya Wakristu Waortodosi, alikutana kwa karibu na Waislamu. Mwaka 1944 alitumwa kumwakilisha Papa huko Paris, Ufaransa, ili kusaidia Kanisa hilo kubwa kujiunda upya baada ya vita.
Hii haikuwa kazi rahisi kwa sababu Balozi aliyetangulia alishirikiana na Wajerumani. Hivyo serikali ya Rais De Gaule na Wafaransa, walimchukia pamoja na Maaskofu waliofuta, nyayo zake. Sasa Askofu Mkuu Roncalli, ilibidi afanye kazi ya ziada kutuliza hali.
Wakati huo alikuwa vile vile Mwakilishi wa Papa katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Kushughulikia Watoto (United Nations International Children’s Emergency Fund: UNICEF). Baada ya kazi nzuri akiwa na umri wa miaka 71, mwaka 1953 aliteuliwa kuwa Kardinali na Patriarka wa Venezia.
Papa Pio XII alipofariki (Oktoba 1958), Makardinali walikuwa na wakati mgumu kukubaliana juu ya nani amrithi. Ilikuwa vigumu kupata theluthi mbili za kura kwa mtu mmoja. Hivyo, baada ya kupiga kura mara 11, waliona wampate Papa wa mpito atakayekubalika kwa wote wakati hali inaendela kuwa shwari.
Tarehe 9 Oktoba 1958 katika kura ya 12, walimchagua Kardinali Angelo Roncalli, mwenye umri wa miaka 76, mtu asiyekuwa na misimamo mikali, lakini mtu wa watu na Mwanadiplomasia mzuri katika kuleta mahusiano na watu.
Alichagua jina la Yohana XXIII. Mfano wa maisha yake na mtu ambaye alitaka kufuata nyayo zake alikuwa Mtakatifu Papa Pio X (1903-1914: wa 257) ambaye alizaliwa akiwa maskini, na kufa akiwa maskini. Naye kabla ya kuchaguliwa kuwa Papa, alikuwa Patriarka wa Venezia.
Katika hotuba zake za mwanzo, mara moja Papa Yohana XXIII aligusia mambo makuu mawili ambayo alitamani kuyatekeleza. Kwanza kuhuisha Kanisa ili lioane na nyakati, yaani kusoma alama za nyakati kama alivyoiita (Aggionamento).
Alitaka kulihuisha Kanisa kiroho. Pili aligusia kuita Mtaguso Mkuu wa Kanisa kufanya kazi hiyo muhimu. Papa Yohana XXIII alihisi kwamba amevuviwa na Roho Mtakatifu kutengeneza Kanisa na kulihuisha.
Wakati akiamini juu ya Neno la Mungu na Mapokeo rasmi ya Kanisa ambayo ni msingi wa Imani na hayawezi kugeuka, aliona mazoea mengine yaliyoingia kufuatana na utamaduni na mwenendo wa watu wa mahali, au wakati fulani yanaweza na mara nyingine yanapashwa kugeuka kukidhi mahitaji ya wakati na mahali.
Kwanza alianza na desturi za maisha ya Papa. Tofauti na watangulizi wake waliokaa ndani Vatikano, yeye alitoka nje mjini Rona na kwenda kuwatembelea watoto wagonjwa hospitalini, na hata wafungwa.
Alisisitiza kuwaona hata wafungwa sugu na hatari. Aliwaambia wafungwa: “Kwa sababu ninyi hamuwezi kuja kunitembelea, imebidi mimi nije kwenu.” Vile vile alikutana na watu ambao kabla haikufikirika kukutana na Papa kama mpwa wa Rais wa Urusi Nikta Khrushchev, Askofu Mkuu wa Kantebury, yaani Mkuu wa Kanisa la Anglikana, kasisi mkuu wa dini ya Shinto kutoka Japan, na wengine.
Kwa mara ya kwanza katika karne moja, alisafiri nje ya Roma na kwenda Asizi. Alipokutana na watu, hakujiona au kujionyesha kama Kiongozi Mkuu wa Vatikano, bali kama mchungaji au kama alivyosema “Mtumishi wa watumishi” (Servus Servorum), akiwa na sura ya Mchungaji kuliko ya Mtawala.
Papa Yohana XXIII aliliona Kanisa kama chombo cha kiroho kilicho juu ya madaraka yote ya siasa, na chenye jukumu la kuwapatanisha, mathalani wakati wa mzozo wa silaha za nuklia wa Cuba mwaka 1962, ambapo ilikuwepo hatari ya vita vikuu vya mabomu ya nuklia kati ya Urusi na Marekani kutokea.
Papa Yohana XXIII aliingilia kati baina ya John Kennedy wa Marekani na Khrushchev wa Urusi kwa kuzungumza nao, na hivyo akapunguza munkari. Mambo yalipotulia, wote wawili walimshukuru.
Papa Yohana XXIII aliongeza Jopo la Makardinali kiasi kwamba kufikia mwaka 1962, lilikuwa na Makardiali 89, ikiwa 19 zaidi ya wale 70 wa Kanuni iliyowekwa na Papa Sisto IV (1471-1484: wa 212) katika karne ya 15.
Kati ya Makardinali hao, aliwateua wengine kutoka Afrika, Filipino na Japan, licha ya Marekani na nchi nyingine. Kati ya Makardinali alimteua Mwafrika wa kwanza na mtu mweusi wa kwanza kuwa katika jopo hili, Mwadhama Laurean Kardinali Rugambwa, Mtanzania kutoka Jimbo la Rutabo, Bukoba, Kagera, Tanganyika wakati huo, mwaka 1959.
Kuna watu ambao hawakuamini kwamba mtu mweusi angelikuwa Kardinali. Ikumbukwe kwamba wakati huo karibu nchi zote za Afrika zilikuwa bado koloni na Marekani mtu mweusi hakuweza kupiga kura na hata kukaa sehemu moja na wazungu, kwani alitengwa kama mkoma. Katika uongozi wake, aliwateua Makardinali 54.
Kama Baba Watakatifu waliomtangulia, naye alitoa barua mbalimbali za kichungaji. Tofauti na wengine, barua zake hazikuwa za kulaumu, au za kutoa fasili ngumu za teolojia, bali mambo ya kawaida yenye ladha ya kichungaji yaliyowahusu na kuwagusa watu, bila ubaguzi.
Papa Yohana XXIII aliandika barua nane za kichungaji, na kati ya barua hizo alizoziandika, mbili zilikuwa na msukumo mkubwa. Mater et Magistra (Kanisa kama Mama na Mwalimu), hii ilikuwa barua ya tano iliyotolewa tarehe 15 Mei 1961 ikiwa ni miaka 70 tangu barua ya Papa Leo XIII (1878-1903: wa 256) Rerum Novarum, na miaka 30 tangu barua ya Papa Pio XI (1922-1939: wa 259) “Quadragesimo Anno.”
Katika barua hiyo iliyosifiwa na kukubalika Ulimwengu mzima, ilijadili masuala ya jamii kama walivyofanya watangulizi wake kwa mtazamo chanya, huria na wa kujenga. Barua maarufu kuliko zote ni ile ya “Pacem in Terris“ (Amani Ulimwenguni) aliyoiandika tarehe 11 Aprili 1963, miezi miwili kabla ya kifo chake Papa Yohana XXIII.
Tofauti na barua nyingine za Baba Watakatifu wengine, Papa Yohanne XX111, aliwaadikia watu wote wenye mapenzi mema. Kweli ilikuwa inawafundisha na kuwaasa watu wa Ulimwengu mzima. Ulikuwa kama wosia wake wa mwisho kwa Ulimwengu.
Barua hii imechambua hali halisi ya kijamii Duniani. Papa Yohana XXIII anatutaka kuheshimu utu wa watu, na anadai kwamba kuheshimu haki za binadamu wote, ndio msingi wa haki na amani ya kweli.
Anaandika “Mwanadamu ana haki ya kuishi. Ana haki ya uadilifu wa mwili na njia zinazohitajika kwa maendeleo sahihi ya maisha, haswa chakula, mavazi, malazi, matibabu, mapumziko na, mwishowe, huduma muhimu za kijamii. Ana haki ya kutunzwa katika hali mbaya ya afya; ulemavu unaotokana na kazi yake; mjane, uzee; kulazimishwa kukosa kazi; au wakati wowote bila kosa lake mwenyewe, ananyimwa njia ya kujikimu.”
Licha ya kusisitiza juu ya utu na usawa wa binadamu, anaasa juu ya haki za wanawake, anawasihi kutoenezwa kwa silaha za nyuklia. Anafundisha juu ya umuhimu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuwaleta watu wote pamoja, kujadili na kuleta muafaka juu ya kutatua mafarakano na kuleta maendeleo ya kweli kwa watu wote.
Bahati nzuri, tafsiri ya barua hii iko katika Kiswhili, na inapatikana kwenye mtandao wa Vatikano.