DAR ES SALAAM
Na Arone Mpanduka
Mwaka 2024 umeingia, huku wasanii wa muziki wa kizazi kipya wakiwa wanakimbizana na wingi wa wasikilizaji na watazamaji kupitia mitandao ya kijamii.
Kwa mwaka jana 2023, zipo nyimbo nyingi zilizokuwa mstari wa mbele kwa kusikilizwa zaidi na watu pamoja na kutazamwa zaidi kwenye televisheni na mitandao ya kijamii.
Tumaini Letu linakuletea orodha ya baadhi ya nyimbo zilizofanya vizuri kwa mwaka jana.Ninasema baadhi kwa sababu zipo zingine nyingi zilizotikisa kwa mwaka jana.
JUX FT DIAMOND PLATNUMZ - ENJOY
Wimbo huu umevunja rekodi zake zote, kuanzia audio, video mpaka mapokezi ya mtaa, Enjoy ime-takeover kila mahali. Ikiwa na uchanga wa mwezi mmoja YouTube, Video ya Enjoy imekusanya watazamaji milioni 20 huku audio yake ikisikilizwa zaidi ya mara milioni 11 kwenye mtandao huo.
Enjoy ambayo ni kolabo na Diamond Platnumz, inavunja rekodi ya kuwa video na audio kubwa za Jux tangu aanze kuachia muziki kidigitali.
MBOSSO - AMEPOTEA
Mei 11, 2023 ndiyo tarehe ambayo Mbosso aliiachia video ya wimbo huo YouTube. Video ya Amepotea ilitosheleza kuwepo kwenye YouTube chaneli ya Mbosso bila kusindikizwa na audio wala lyrics video.
Video pekee iliyoachiwa YouTube imetazamwa kwa zaidi ya mara milioni 9.6 huku audio yake Boomplay ikiwa na wasikilizaji milioni 13.8 sambamba na milioni 3.25 Audiomack. Jumla ya streams za Amepotea ni milioni 26.75.
DARASA - NO BODY
Darassa aliziachia Mind Your Business, Dead Zone na moja kati ya nyimbo zake zilizofanikiwa kuwafikia watu wengi zaidi hata tuweze kusema kuwa Nobody ni miongoni mwa nyimbo zilizofanya vizuri mno mwaka huu.
Nobody iliyoachiwa Februari 24, ndio wimbo pekee wa msanii wa Hip Hop/Rap ulioweza kukusanya zaidi ya streams nyingi mwaka huu.
Kupitia Nobody peke yake, Darassa ameweza kukusanya zaidi ya wasikilizaji milioni 26.37. Video ya Nobody ambayo YouTube ina watazamaji zaidi ya milioni 1.5, haijafanya vizuri kama audio yake ambayo YouTube imesikilizwa zaidi ya mara milioni 7 na zaidi ya mara milioni 14.2 Boomplay na milioni 3.17 Audiomack.
JAY MELODY - SAWA
wimbo wake ‘Nakupenda’ na chorus yake kwenye ‘Puuh’ ya Billnass.
Baada ya matokeo chanya ya kazi hizo mbili, Jay aliufanya ‘Sawa’ kuwa wimbo wake wa pili kwa mwaka huo. Mpaka hivi sasa audio na video za Sawa zimekusanya watazamaji milioni 17.5 YouTube. Kwa upande wa Boomplay wimbo huu ulioachiwa Februari 27, umewafikia zaidi ya wasikilizaji milioni 36.9 na milioni 3.58 ‘Audiomack’.
Namba zinazoifanya jumla ya wasikilizaji wa wimbo huu kufikia milioni 57.98
ZUCHU - NANI
Ndani ya wimbo huu Zuchu ameshirikiana na mama yake mzazi, Khadija Kopa na msanii Innoss B kutoka nchini Congo, na hadi mwaka 2023 unamalizika, wimbo huo ulikuwa na zaidi ya watazamaji milioni 10.
Wimbo huu umejizolea umaarufu hasa kwa watoto wadogo ambao wengi walipenda staili yake ya uimbaji ambayo inaendana na nyimbo za watoto.
DIAMOND PLATNUMZ - YATAPITA
Diamond aliazimia kuumiliki mwaka 2023 kwa kufanya maajabu mengi na aliuanza mwaka na Yatapita. Wimbo ambao umekusanya zaidi ya streams milioni 44 YouTube video na audio, milioni 22.9 Boomplay na milioni 2.7 Audiomack. Streams za Diamond Platnumz kwenye orodha hii zinahesabika kuwa milioni 69.67.
Yatapita ni wimbo wa Diamond ambao umekusanya namba za wasikilizaji wengi kuliko nyimbo nyingine ambazo mkali huyo amefanya mwaka huo.
ALI KIBA FT MARIOO - MKE WA MTU SUMU
Akishirikiana na Marioo, Ali Kiba alitoa wimbo huo Julai mwaka jana, na kushika hatamu katika maeneo mbalimbali ya starehe bila kusahau vituo vya redio na televisheni. Kwa mfano kwenye youtube, wimbo huo umemaliza mwaka 2023 ukiwa na zaidi ya watazamaji milioni 6.
HARMONIZE - SINGLE AGAIN
Wimbo huu ulioachiwa siku ya wapendanao, umekusanya zaidi ya streams milioni 72.86, kwa mujibu wa namba za video na audio ya YouTube, ‘Audiomack’ na BoomPlay, Harmonize ndiye msanii mwenye wimbo unaokusanya wasikilizaji wengi zaidi ukiwa unachangia asilimia 15.7 ya streams zote kwenye orodha hii.
RAYVANNY FT MISSO MISONDO - KITU KIZITO
Mnamo mwezi Desemba 2023, video ya wimbo huu ilitoka. Rayvanny alijizolea mashabiki wengi kupitia wimbo huo kwa kipindi kifupi tu cha mwezi mmoja kabla yam waka kuisha hasa baada ya kuwashirikisha vijana machachari walioibuka na ubunifu kutoka Mtwara.
Misso Missondo ni jina la kimuziki la kijana mmoja DJ wa mtaani aliyeamua kubuni kundi lake maarufu kama ‘wazee wa makoti’ ambao huko kijijini walikuwa wakijipatia umaarufu kwa kucheza kwenye sherehe mbalimbali.
Staili yao ni ya singeli ingawa wameweka ubunifu wa kurudia beats za nyimbo za kawaida zilizowahi kuchezwa na wasanii wengine na kisha wao huingiza maneno yao na kucheza kwa staili yao tofauti. Singali zao zinasifika kwa ustaarabu bila kutumia lugha za matusi.