Mwanza
Na Paul Mabuga
Wimbi la watu kuwa na maarifa kutokana na usomi lakini matendo yao yakawa tofauti, wengi wao ni malezi ya wazazi yanayozaa raia magarasa.
Utakuwaje na maarifa na hata fedha lakini maneno yako hayaendani na matendo? Jamii yetu ipo katika madhila ya tatizo hili, na makala haya yanatafuta majibu ni kwa nini tunakuwa na hali hii.
Anakufuata jamaa mwenye ukwasi, elimu na maarifa ya kutosha anakufuata akilalamika kwamba wenyeji katika eneo ulilotembelea, siyo nje ya mji mmoja kanda ya Ziwa, ni wema kwa kuwa wamemloga mke wake. Ndiyo maana analewa kupita kiasi na binti yake anayesoma Kidato cha Nne, hadi amekataa kwenda shule.
Anakuambia kisa ni kwamba yeye ana fedha na wanamuona kuwa ni tajiri, na hivyo ulozi anaousema unatokana na kuonewa wivu. Ni kweli anamiliki nyumba mbili ambazo hazijaisha wala kukamilika, ila watu wanaziishi kibishibishi, na baiskeli moja ambayo ina kitako ambacho hakifunikwi.
Kimsingi binti yake ni kweli ana kawaida ya siku kadhaa haendi shule, ama anakwenda kwa kuchelewa, na ni wazi kuwa hakuna anayefuatilia kwa vile mama yake muda mrefu anakuwa amelewa, ama kazima data, kama wanavyosema watu wa karne hii.
Inafikirisha sana kupata kauli kama hizi kwa mtu ambaye amekwenda shule na kusoma kwenye vyuo vya uhakika na hata kuwa na uwezo wa kifedha, anakuwa katika hali hiyo. Tena kukuongezea mshangao, ila anakuelezea mambo mengi ya kielimu akikumbuka mambo wakati wa enzi zake akiwa shuleni.
Wakati unashangaa hili, unapanda bajaji kwenda kituo cha basi ili kupata usafiri wa kurudi unakoishi, na abiria wenzako ni familia ya mke na mume ambayo inatoka shamba kulima.
Unawauliza maswali, lakini muhimu wanakuambia, wote ni wahitimu wa Kidato cha Nne na kwamba chanzo chao ni mbegu za mahindi kuziokota zile zilizodondoka mashineni! Unachoka.
Unajiuliza hivi ni kwa nini watu wanashindwa kutumia kiwango bora cha maarifa waliyopata kutokana na elimu waliyopata? Je ni malezi ya helikopta ya kutafutiwa kila kitu katika malezi na elimu yao?
Je, ni kukosa muda wa kufanya kwa uhalisia juu ya kila wanachokisoma na kile ambacho watakutana nacho katika maisha, au tu tumeamua kuwa kizazi cha hovyo?
Je, tunaugua ugonjwa wa akili hadi kufikia hatua hii? Unashangaa nini kama tulitegemea kikombe cha babu wa Loliondo kutibu kila ugonjwa, lakini bado tukajiona tuna maarifa?
Jiulize tu kama kikombe hicho kingekuwepo hadi leo, ni misiba mingapi ingekuwepo! Hivi ukiambiwa ukila ndizi iliyooshwa kwa maji maalum utapata mchumba, shahada yako ama cheti cha Kidato cha Sita huwa unakuwa umekificha wapi, kama siyo maliwatoni!
Mjini kisomo! Mtaani katika jiji la Mwanza napo unakutana na kijana mwenyeji wa moja ya jamii zinazopatikana katika mkoa wa Arusha, anakupa kikaratasi chenye orodha ya magonjwa 63 ambayo anadai kuyatibu, lakini mikebe ya dawa haizidi mitano, na anakuhakikishia kuwa anapata wateja wa kutosha - majirani.
Cha kushangaza, ukiuliza unataka mchumba, presha ya kupanda, ya kushuka, kisukari na kutafuta kazi, anakupa chupa moja kwa magonjwa yote hayo. Anaongeza kuwa dawa hiyo pia inatibu Uric Acidi iliyozidi mwilini na magonjwa sugu ya njia ya mkojo! Unapata jibu ni kwa nini ana orodha ya magonjwa mengi, lakini mzigo wa dawa kiduchu.
Dk. Nkwabi Sabasaba anasema kwamba kuwa na maarifa na kutenda wakati mwingine vinaweza kuwa tofauti, kwani uwezo wa kufanya mambo huongozwa na ubongo wa mbele ambao pamoja na mambo mengine, una jukumu la kutafsiri kile ulicho nacho katika maarifa, na kukiweka kwenye matendo. Anasema kwamba ubongo unaposhindwa kufanya kazi hiyo kikamilifu, hali tunayoizungumzia hujitokeza.
“Hali hii ya ubongo kushindwa kutafsiri maarifa na ujuzi na kuviweka katika vitendo, inaweza kuwa imesababishwa na mazingira ya malezi ya mteremko, kudekezwa na kushindwa kutenda, na hivyo ubongo unashindwa kupata hamasa ya kujishughulisha, anasema Dk. Nkwabi Sabasaba.
Na anaongeza, “Ukiwafuatilia watu wa namna hii, wengi ni waongeaji sana! Hii inaletwa na mzazi kuona kuwa mtoto hawezi kuhangaika, hawezi kufua, yaani anamlea ki helikopta kwa kujali kuwa mtoto hawezi kuhangaika, na hivyo ubongo wa mbele unakuwa ‘inactive’ [unadumaa].”
Pia, uwezo wa akili kwa maana ya ‘Intelligent quotient [IQ],’ ni tofauti na ule mhemko wa kutenda, ‘emotion quotient [EQ],’ kwamba mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa maarifa, lakini hawezi kutenda kutoka na uwezo mdogo wa mhemko.
Dk. Nkwabi anafafanua kuwa katika mwili wa binadamu kuna sehemu ya ubongo ambayo inachochea hamasa ya mhemko wa kutenda, yaani binadamu mathalani anapoona mkufu na akautamani, basi sehemu hii inamhamasisha ili kufanya juhudi aupate, na anapata nguvu zote kuusaka, hii ni EQ.
“Kimsingi EQ ni bora kuliko IQ! Mnaweza mkaingia kazini kwenye ajira wote mkiwa na IQ nzuri ambazo zimeoneshwa kwenye vyeti vyenu, lakini baada ya muda mwingine akawa na EQ nzuri na akasifiwa kwa utendaji,” anasema Dk. Nkwabi.
Lakini pia anazungumzia kitu kingine katika hali hii kwamba mtu anaweza akawa na IQ kubwa, lakni ule uwezo wake wa kumudu watu wengine [Social Quotient] unakuwa wa chini, na hivyo wakati mwingine kulazimika kutumia fedha kuwamudu.
“Unakuta mtu anaajiri watu wengine kwa kuwalipa fedha ili kumudu familia yake, anaagiza ‘naomba unisaidie kumdhibiti huyu mtoto ama mke ili waondokane na tabia hii ama ile.’ Hii ni dosari ambayo kama mtu anayo, basi hafai kuwa kiongozi,” anaonya Dk. Nkwabi na kusema kuwa mtu anaweza kuwa na uwezo mkubwa wa fedha ‘Financial Quetient’, lakini akakosa EQ na uwezo wa kuwamudu watu wengine.