MWANZA
Na Paul Mabuga
Wakati huko wanafunzi wakiandika matusi kwenye mitihani yao, kule watoto wameiba simu janja yenye thamani ya zaidi ya Shilingi 300,000/-, baada ya kumhadaa mama muuza barafu.
Kwenye daladala, konda kavaa fulana yenye maandishi ya Kiingereza, yenye tafsiri kuwa amefurahia uzinzi, na kwenye mtaa jirani Askari Polisi kaibiwa kuku wanne. Lakini, wenyewe tukikutana, tunasalimiana, ‘Mambo poa’.
Yaani kwamba, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani, Dk. Saidi anatuambia wanafunzi 17, watatu wakiwa watahiniwa wa darasa la nne na 12 wakiwa ni wa kidato cha pili, wamefutiwa matokeo baada ya kuandika matusi katika mitihani waliyoifanya mwaka jana.
Yaani, watoto hawa wametukana, ila tu ni kwamba walikuwa wanatukana nini na wanamtukana nani hatujui.
Hii si mara ya kwanza kwa tukio kama hili, kwani kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2018 jumla ya watoto 33 nao walifutiwa matokeo kwa kuandika matusi katika mitihani yao.
Yaani mwaka huu ni hao 17, lakini mwaka 2022 watahiniwa 14 wa kidato cha pili walifutiwa matokeo pia, na wengine wawili wa kidato cha nne, nao walikumbwa na dhahama kama hiyo mwaka 2022.
Angalia, mtoto mwenye umri wa miaka tisa ama 10 akiwa darasa la nne, anaandika matusi, ama tusema anatukana, na kulifanya taifa kusimama kujadili kishindo chake.
Unadhani akifikisha umri wa miaka 22 na akiwa amehitimu Chuo Kikuu kama atafanikiwa, na ikiwa hakurekebishwa, hali itakuwaje katika muktadha wa kujenga kizazi chenye maadili?
Katika mahojiana kwa ajili ya makala haya, Mwalimu John Ndama kutoka Manispaa ya Shinyanga, anasema, “Haya ni mambo yanayotokea katika miaka ya hivi karibuni,” na katika uzoefu wake wa kufundisha kwa karibu miaka 30 kwenye shule za sekondari, hakuwahi kuona mambo kama hayo.
“Hawa ni watoto watukutu, na kwa bahati mbaya wanazidi kuongezeka kadri miaka inavyozidi kwenda. Inawezekana chanzo kikubwa ni wazazi kushindwa kupata muda wa kuwalea kutokana na kubanwa na harakati za kutafuta fedha, baada ya changamoto za kiuchumi kuongezeka, na badala yake, vijana wanalelewa na runinga na mitandao ya kijamii,” anasema Mwalimu Ndama.
Anasema kwamba yaani watoto wanaona vitendo vyenye maudhui magumu yenye mwelekeo wa matusi kwenye runinga, lakini pia wanaona maandiko na sauti za matusi kwenye mitandao ya kijamii. Lakini baadhi ya familia zinaona haya ni mambo ya kawaida, na hivyo kuyaruhusu yaendelee bia udhibiti! Tunajenge kizazi cha viumbe kisicho na utamaduni, ‘uncultured creatures’.
Katika hali kama hii inakuwaje? Unasafiri kwenda Mtwara kikazi, lakini basi ulilopanda linaharibika njiani katika moja ya vijiji vya mkoa wa Lindi.
Anakuja kijana anauza mahindi ya kuchoma akiwa amevaa fulana yenye maandishi, “Girls for Sex, No offer Rejected,” (yaani Warembo kwa ajili ya ngono, wapo tayari kwa pesa yoyote). Ukimuuliza maana yake anajifanya kufahamu, lakini anakuambia ni zawadi aliyoletewa na baba yake anayeisha jijini Dar es Salaam.
Kijana anadai anafahamu maadishi, na katika umri wake wa miaka 12, bila shaka ubonge wake ulivyo kama sponji, unamnyinya kila kitu, na kuona kuwa haya ni maisha ya kawaida. Kwa nini huyu asione kuwa kuandika matusi kwenye mitihani, siyo ‘jambo mzungu, [la kustaajabisha]?’.
Unapanda moja ya daladala katika Jiji la Mwanza, konda analifunga kiunoni koti lenye nembo kuonesha kuwa hiyo ni sare ya kazi. Hali hii inaifanya fulani aliyoivaa na maandishi yake yanayosomeka, “We ejoyed sex overnight!” Hakuna anayemsemesha na kumuonya miongoni mwa abiria, na zaidi wanasalimiana miongoni mwao kuwa ‘mambo poa.’ Fikiria kijana aliyemo ndani ya dalada hiyo, hali hiyo anaichukuliaje?
Katika mtaa mmoja jijini Mwanza, wakati Askari Polisi anamsimulia mama jirani yake juu ya kuibwa kwa kuku wake na vibaka, mama huyo naye anaelezea juu ya watoto wawili wenye umri kati ya miaka tisa na 10, walivyofika kwake na kumuibia simu janja kwa namna ambayo hakuweza kuamini.
Mama huyo, Grace Kezla [43], anasema kwamba alipokuwa ameketi kiambazani nje, walifika watoto wawili na kutaka kununua barafu mbili, na wakatoa shilingi 200.
Mama huyo akaingia ndani kwenda kuchukua hiyo bidhaa kwenye jokofu, kwa bahati mbaya akaacha simu janja kwenye mkeka aliokuwa amekalia. Wale watoto bila kuchelewa walichukua ile simu na kuondoka, na alipotoka nje, hakuona kitu.
“Ni kama vile niliuza simu ya Shilingi 300,000/- kwa Shilingi 200.” Anasema Grace ambaye anapoulizwa kuhusu watoto kuandika matusi kwenye mitahani anasema, “Kwenye jamii yetu kuna vitu haviko sawa, wazazi wameelemewa, na waalimu nao wamezidiwa! Hapo panahitajika juhudi nyingine za ziada, vingenevyo tutapata tabu.”
Anasema, “Wazazi wapo na shida ya kutumia muda mwingi kutafuta fedha kwa ajili ya mahitaji ya familia. Waalimu nao wanataabika na mzigo mkubwa wa wingi wa wanafunzi kuliko uwezo wao, na hivyo kufanya ‘bora liende’. Wakati hali ikiwa hivyo, bado kwa kila hali, inatakiwa kadri iwezekanavyo, kila kijana amalize elimu ya sekondari.
Anashauri kuwa ingawa mtaala mpya wa elimu una msisitizo juu ya maadili, lakini kuna haja ya jambo hili kuwa mtambuka likihusisha wadau na sekta mbalimbali ili kukikomboa kizazi hiki.
“Kama Waunguja wanaona kuwa kwa mwanamke kukaa kwenye boda, ama kipando kama mwanaume ni sawa na kutukana, badala yake anapaswa kukaa upande, inashindikanaje katika maadili yetu?”
Uzoefu mwingine ni kuhitajika umakini juu ya kusimamia maadili ya kijamii, ni maelezo ya Msese Mwanzalima [80], mkazi wa Shinyanga ambaye anasema kwamba kutokana na waalimu kuzingatia kazi zao enzi hizo, alifukuzwa akiwa darasa ka pili mwaka 1958, enzi za Mkoloni kwa kosa ambalo anadhani pengine leo hii lingevumilika.
“Kwenye madawati, enzi hizo kulikuwa na kitundu kwa jiuu, sasa hapo paliwekwa kidau ambapo kilijazwa wino kwa ajili ya kuchovya ‘pen’ iliyokuwa na ‘nib’, na kuandika.
“Mimi badala yake nilikuwa nachovya kidole katika kidau na kujipaka usoni, ila mchezo huo ulitosha kunifukuzisha shule,” anasema Mzee Mwanzalima akikumbukia hali ilivyokuwa wakati huo, huku akidai kwamba hawa waalimu wa siku hizi, ni wapole sana.