Na Pd. Raymond Sangu, OCD
SWALI LIMEULIZWA: Je, Ni sahihi kwa Wakristo kuadhimisha/kusherehekea VALENTINE’S DAY, yaani Siku ya Wapendanao? – Evelyne, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam – TANZANIA, anauliza.
MAJIBU, mpendwa Evelyne, kulingana na swali lako, nitakupa maelezo kuhusu mambo manne kama ifuatavyo: Jina VALENTINE, kwa nini ni tarehe 14 FEBRUARI, rangi NYEKUNDU na mwisho MAANA YA SIKU HII KWA MKRISTO.
HISTORIA YA JINA VALENTINE Valentine alikuwa Padre Mkatoliki wakati mtawala wa Kirumi aliyeitwa Klaudio alipokuwa akilitesa Kanisa. Padre huyo alizaliwa mwaka 226 BK huko Terni nchini Italia, na kufariki Februari 14 mwaka 269 BK huko Roma, Italia. Valentine ndiye mtakatifu msimamizi wa wapendanao.
KWA NINI FEBRUARI 14 INAITWA SIKU YA VALENTINE? Mtawala wa Kirumi Klaudio alikuwa ametoa amri/agizo lililokataza vijana wasifunge ndoa. Hii ilitokana na dhana kwamba askari ambao hawajaoa, walipigana vizuri zaidi kuliko askari waliooa.
Hii ni kwa sababu askari waliooa wangeweza kuogopa nini kingetokea kwa wake zao na familia zao ikiwa askari hao wangekufa. Valentine aliwafungisha ndoa vijana kwa siri, kinyume na amri/agizo/katazo la Mfalme Klaudio. Hatimaye alikamatwa, akateswa na kufungwa kwa kukiuka amri ya Mfalme.
Mnamo Februari 14 mwaka 269 BK, Valentine alihukumiwa kifo kwa hatua tatu, kwanza kipigo, pili kupigwa mawe, na hatimaye kukatwa kichwa. Yote haya yalisababishwa na msimamo wake kuhusu ndoa ya Kikristo.
KWA NINI RANGI NYEKUNDU? Kadri ya vyanzo mbalimbali, rangi nyekundu inaashiria sadaka, hisia na upendo wa kina, kwa wale wanaopendana, au walio katika uhusiano, au wale wanaotarajia hilo. Ni rangi inayohusishwa na kuamsha hisia au upendo. Ndiyo maana rangi hii hutumika katika ya Siku ya Wapendanao.
VALENTINE YA KWELI: Februari 14 ni siku ya kusherehekea upendo. Lakini sio tu ule wenye uelekeo wa uhusiano wa kimapenzi. Ikiwa huna valentine katika maana inayoshabikiwa na watu wengi, wala usifadhaike. Kuna mazuri mengi yanayoweza kutokana na kuwa ‘single’.
Kuwa ‘single’ hukupa fursa ya kuwa huru, kujitambua wewe ni nani, unapenda nini, nini hupendi, na ni kitu gani kinachofaa zaidi kwako. Usiruhusu tarehe 14 Februari kuwa ukumbusho wa jinsi ulivyoshindwa kupata upendo. Ikiwa uko kwenye uhusiano, Februari 14 siyo siku ya kuthibitisha upendo, badala yake ni siku ya kuendelea kuondoa matabaka na makandokando yanayozuia upendo kushamiri katika uhusiano wako.
HITIMISHO: Februari 14 ni siku ya kusherehekea upendo. Kujipenda mwenyewe, kupenda maisha yako, kupenda mapambano ya maisha, kumpenda kila mtu maishani, aliyeko katika maisha yako, na vile vile kumpenda hata yule ambaye yuko nje ya maisha yako. Ikiwa hujaoa au kuolewa, tarehe 14 Februari ni siku nzuri ya kusherehekea uhuru wako na kukumbatia ujasiri wa kuwa radhi ya kuwapokea watu wote, kupenda zaidi na kujifunza zaidi kuhusu upendo.
Baada ya maelezo marefu, nihitimishe kwa kusema kwamba hata Wakristo pia wanapaswa kuadhimisha na kusherehekea SIKUKUU YA WAPENDANAO, al maarufu kama VALENTINE’S DAY, ambayo mwaka huu imeangukia katika siku nzuri sana ya TOBA, yaani JUMATANO YA MAJIVU! Happy Valentine’s Day in Advance, Kheri ya Siku ya Wapendanao, lakini zaidi sana KHERI YA SIKU YA JUMATANO YA MAJIVU – Februari 14 mwaka 2024! -----------------------
“Upendo huvumilia, upendo hufadhili, upendo hauoni wivu, hauna majivuno, hauna kiburi. Haukosi kuwa na adabu, hautafuti mambo yake, haukasiriki upesi, hauweki kumbukumbu ya mabaya. Upendo haufurahii matendo mabaya, bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote.” – 1 Wakorintho, 13:4-7 ----------------------
Rev. Fr. Raymond Sangu, OCD, Shirika la Wakarmeli Tanzania ambaye yuko Roma, Italia: Maoni WhatsApp +255 755 223 657