DAR ES SALAAM
Na Ibrahim Mkamba
Tanzania ina wawakilishi wanne kwenye mashindano makubwa ya soka Afrika. Young Africans, (nitakaowataja baadaye Yanga), na Azam FC watatuwakilisha kwenye ligi ya mabingwa Afrika, huku Simba na Coastal Union wakituwakilisha kwenye mashindano ya kugombea ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Makala hii inaongelea hatari ya timu kujiamini kupita kiasi au kuelezewa ubora wao kupita kiasi dhidi ya wapinzani wao, tena kwa kauli zinazowafikia wapinzani hao. Hii ipo kwa Yanga na Simba, na si kwa Azam FC na Coastal Union, na ndiyo sababu makala hii itaziongelea tu timu hizo za Kariakoo, Dar es Salaam.
Ukweli haupaswi kupingika kwamba, ukisahau kucheza nusu fainali ya mashindano ya kugombea ubingwa wa Afrika mwaka 1974 kwa mfumo wa mtoano mwanzo mwisho, sahau kucheza fainali ya mashindano ya CAF mwaka 1993 na potezea kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek ya Misri na kutinga makundi kuwania ubingwa wa Afrika mwaka 2003, tangu mwaka 2018 mpaka sasa, Simba imekuwa moja ya timu za Afrika ya kufika hatua ya robo fainali katika mashindano makubwa ya soka ya Afrika kwa mfululizo.
Ukiiondoa Al Ahly ambayo kwao kubeba ubingwa wa Afrika si habari tena, timu nyingi kubwa za bara hili zimeshindwa kufikia hatua hiyo mfululizo miaka hii. Kuna zilizopotea kipindi fulani kama Zamalek, Esperance de Tunis, Raja Athletic Club, TP Mazembe na nyinginezo kubwa. Kwa hiyo walichofanya Simba si kidogo bali ni kikubwa kinachofanya wastahili sifa. Timu kuwa na uimara ule ule kwa misimu mitano mfululizo, ni jambo kubwa.
Yanga wamekuwa na historia ya kusifika kwenye mashindano ya Afrika tangu 1969 walipotolewa kwenye hatua ya robo fainali kwa kura ya shilingi jijini Dar es Salaam na Asante Kotoko ya Ghana ya kipa wao Robert Mensah, na mkali wa mabao Ibrahim Sunday.
Ni Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kucheza hatua ya makundi mashindano ya ligi ya mabingwa Afrika mwaka ule ule 1998 utaratibu huo ulipoanzishwa. Wakafika fainali Shirikisho Afrika msimu wa 2023/2024 na msimu uliomalizika waliishia robo fainali Afrika. Kwa sasa Yanga ni moja ya timu tishio Afrika. Hili si la kubishaniwa.
Pamoja na ukubwa walionao Yanga na Simba kwa sasa, hiyo haimaanishi watazishinda timu zote, za hadhi zozote, nyakati zote. Kama Simba walivyoifunga Al Ahly Dar es Salaam mechi mbili miaka hii ya karibuni kwa ushindi wa 1-0 kila mechi, magoli ya Meddy Kagere na Luis Miquissone ya mechi hizo tofauti, ndivyo Uhamiaji Zanzibar au wawakilishi wa Libya wanavyoweza kuitupa Simba nje ya mashindano ya Kombe la Shirikisho hatua ya awali.
Kama Yanga ilivyoipiga CR Belouizdad 4-0 jijini Dar es Salaam, ndivyo Vital’O inavyoweza kuishinda Yanga na kuitupa nje ya mashindano kwenye hatua ya awali. Yanga inaweza kupenya hapo kisha kukwama kwa SC Villa ya Uganda, au Commercial Bank ya Ethiopia.
Natoa tahadhari hizo kutokana na kauli ya kujirudiarudia ya Afisa Habari wa Yanga na ya wachambuzi kadhaa wa soka kwamba Yanga itabeba ubingwa wa soka wa Afrika msimu huu. Kwa upande mwingine, kuna baadhi ya wachambuzi wa soka husema Simba itabeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho. Angalau kwa upande huo, Afisa Habari wa Simba hajawahi kutamba hivyo. Afadhali kwa Yanga iliyo kamili tangu msimu wa 2023/2024, lakini Simba iko kwenye matengenezo.
Madhara ya kauli za kuzipaisha Yanga na Simba kwenye ushiriki wao wa mashindano ya Afrika ni, kwanza, zinawafanya wachezaji wao wawe kwenye shinikizo kubwa wakutanapo na timu wanazoaminishwa kuwa dhaifu. Vichwani mwao hujiuliza itakuwaje wakishindwa kuwashinda wadogo hao? Kucheza kwa shinikizo, si jambo salama kwenye soka.
Pili, timu zetu zitaziendea mechi hizo katika hali ya kama kwamba zimeshashinda kwa jinsi zinavyopotoshwa. Hivyo, watabweteka, na wakishtuka tu, mambo tayari yameshakuwa magumu. Zaidi soma Tumaini Letu