NEKEMTE, Ethiopia
Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ethiopia (Catholic Bishops’ Conference of Ethiopia: CBCE), Mwadhama Abune Kardinali Berhaneyesus, amesema kuwa wajibu mtakatifu wa kupitisha cheo cha ukuhani kutoka kizazi hadi kizazi, ni utamaduni unaowezeshwa na Roho Mtakatifu uliopokelewa kutoka kwa Yesu Kristo.
Kardinali Berhaneyesus aliyasema hayo katika mahubiri yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu na kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu Getahun Fanta Shikune, aliyeteuliwa kuwa Askofu wa Vicariate ya Nekemte, nchini Ethiopia.
Aidha, katika mwendelezo muhimu wa baraka za kuadhimisha Mwaka Mpya wa Ethiopia, Kanisa Katoliki nchini humo lilisherehekea kuwekwa wakfu kwa Askofu huyo Mteule.
Miongoni mwa waliohudhuria katika Adhimisho hilo, ni Askofu wa zamani Varghese Thottamkara, C.M., Askofu wa sasa wa Balasore, India, pamoja na Maaskofu mbalimbali, Mapadri, waalikwa maalum, vikundi vya kidini, familia, na Waamini waliojitolea kutoka kote nchini.
Kardinali Berhaneyesus alimkabidhi Askofu huyo jukumu la kuongoza huduma hiyo mpya iliyowekwa na Mungu, akiwahimiza Wakatoliki wote kumuunga mkono mchungaji wao mpya kwa subira pamoja na sala.
Ikumbukwe kwamba Baba Mtakatifu Fransisko alifanya uamuzi wa kihistoria kwa kuwateua Maaskofu watatu wapya wa Kanisa Katoliki nchini Ethiopia, ili kutimiza sala na matarajio ya muda mrefu ya Waamini katika majimbo matatu nchini humo.
Maendeleo hayo yaliyosubiriwa kwa muda mrefu yanaashiria hatua kubwa kwa Kanisa Katoliki la Ethiopia, ambalo lilikuwa likitafuta kwa dhati uongozi wa mtaa kwa ajili ya utume wake wa kiroho na kichungaji.
Matukio hayo yalihudhuriwa na idadi kubwa ya Waamini kutoka kote Ethiopia na nchi jirani, wakiwemo Maaskofu, Mapadre, Masista wa Kidini, na Walei kutoka Eritrea, Association of Member Episcopla Cenference in Eastern Africa: AMECEA (Chama cha Mabaraza ya Maaskofu Wanachama Afrika Mashariki), na Symposium of Episcopal Conference of Africa and Madagascar: SECAM (Kongamano la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika na Madagaska).
Pia, Mkutano huo uliakisi umoja mpana wa Kanisa Katoliki Barani Afrika na nafasi yake katika Ukatoliki wa Kimataifa, na kwamba Sherehe za kuwekwa wakfu hazikuwa za kiroho tu, bali pia za kijumuiya, zilisherehekewa kwa furaha na ushiriki mkubwa kutoka sekta zote za jamii, zikiwemo jumuiya za mitaa, vikundi vya vijana, viongozi wa serikali, na wawakilishi kutoka mashirika mbalimbali ya kidini.
Kardinali Berhaneyesus alisema kwamba ushiriki huo mkubwa na wa aina mbalimbali, ulionyesha uhusiano thabiti kati ya Kanisa na watu wa Ethiopia, pamoja na nafasi muhimu ya Kanisa katika maisha ya kiroho na kijamii ya taifa.
Aliongeza kwamba uwepo wa Wawakilishi wa Kiekumene na Serikali pia ulionyesha dhamira ya Kanisa Katoliki katika ushirikiano wa dini na majadiliano kati ya dini mbalimbali, jambo ambalo ni la muhimu ambalo Maaskofu wapya wanatarajiwa kuendeleza na kuimarisha zaidi.
Alibainisha pia kuwa kuzingatia mizozo ya sasa ya Ethiopia, machafuko ya kijamii, na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu, Kanisa Katoliki linaonekana kama mhusika mkuu katika juhudi zinazoendelea za nchi kuelekea ujenzi wa amani na upatanisho.
Alisema kwamba mchanganyiko huo wa desturi za Kikatoliki na za kimaeneo uliashiria dhamira ya Kanisa ya kuishi pamoja na mshikamano kati ya jumuiya mbalimbali za kikabila na kidini nchini Ethiopia.