Dar es Salaam
Na Mathayo Kijazi
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu amewapongeza wazazi waliowalea vyema watoto wao tangu walipobatizwa hadi kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, akiwataka wengine kuiga mfano huo.
Pongezi hizo alizitoa wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Nicholaus wa Tolentino, Msingwa, jimboni humo.
“Kwa hiyo, tunawashukuru sana wazazi ambao walikuwa pamoja na hawa watoto, wakawalea kiroho, kwa sababu wale ambao waliachwa katikati humo, baada ya kupata Ubatizo, wazazi hawakuhangaika nao;
“Kwa hiyo watoto hao inawezekana waliishilia huko, wakaendelea kukua bila kupata Ekaristi, bila kupata Kipaimara. Kwa hiyo, wako watu wa namna hiyo ambao wazazi hawahangaiki na watoto katika makuzi yao ya kiroho…. Walioko hapa mbele yetu inaonekana wazazi waliwajali, waliyajali maisha yao ya kiroho, wakawaongoza, hadi kupokea Sakramenti hii,” alisema Askofu Mchamungu.
Aidha, licha ya kuwapongeza wazazi hao kutokana na jitihada katika malezi, Askofu Mchamungu alisema kuwa bado wanalo jukumu la kuendelea kuwalea, kwani bado ni watoto na wanaendelea kukua.
Alisisitiza kuwa watoto hao bado ni wadogo huku wakiwa hawana uwezo wa kufanya maamuzi binafsi, hivyo ni vema wazazi wakaendelea kuwasimamia ili wakue katika misingi na imani thabiti.
“Bado ni watoto ambao hawawezi kufanya maamuzi binafsi, kwa sababu bado wako pungufu ya miaka 18. Aliye na miaka 18 au zaidi, tunasema ni mtu mzima, anajifanyia maamuzi yake, lakini hawa ambao leo hii wataimarishwa, bado ni watoto, na bado wanahitaji uangalizi wa wazazi,” alisema Askofu Mchamungu.
Wakati huo huo pia aliwasisitiza Waimarishwa kuzidi kuisimamia imani yao, huku akiwasihi kwamba wasije wakafika mahali wakaiacha imani yao, na kushikilia imani dhaifu katika maisha yao.
Aliongeza pia kwamba zipo jitihada kubwa zilizofanywa na Makatekista kwa watoto hao tangu walipopokea Kumunyo ya Kwanza, na kisha kuwaandaa kwa ajili ya kupokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, hivyo utume wao ni wa kipekee na wenye thamani kubwa.
Askofu Mchamungu aliwakumbusha kuwa kazi ya Roho Mtakatifu ni kumwimarisha Mwamini, hivyo akawataka Waimarishwa kumpokea Roho huyo, ili awafanye kuwa Askari hodari wa Kristo katika maisha yao.
Pia, aliwasisitiza Waimarishwa hao kuwa wakakamavu kama walivyo askari wengine, akisema, “Kwa kawaida mtu anayeitwa askari, ni mkakamavu, hakuna askari ambaye yuko ‘slow slow’ tu, amelegealegea kama konokono, hapana, askari yuko mkakamavu.”
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Efrem Msigala alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuadhimisha Misa hiyo.
Parokia ya Mtakatifu Nicholaus wa Tolentino ilianza kama Kigango cha Parokia ya Mtakatifu Augustino, Temboni, na ilitangazwa rasmi kuwa Parokia Julai 7 mwaka 2022 na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi.