DODOMA
Na Ndahani Lugunya
Wakristo nchini wametakiwa kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo, kuchangia Pato la Taifa, na kutatua changamoto katika maeneo yao.
Hayo yalielezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene, wakati akizunguma katika sherehe ya kumweka wakfu Askofu wa tatu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto, iliyofanyika Jijini Dodoma, baada ya aliyekuwa Askofu wa Kanisa hilo, Askofu Donald Mtetemela kustaafu.
Simbachawene alisema kuwa changamoto nyingi za kiuchumi katika jamii zitatatuliwa endapo wananchi watajituma kufanya kazi na kuwa wabunifu kwa kuanzisha miradi mbalimbali, kama ambavyo Maandiko Matakatifu yanavyoagiza watu kufanya kazi.
“Lazima Wakristo wa sasa tufanye kazi, lazima tutatue changamoto kwenye maeneo yetu kwa sababu imeandikwa katika Biblia, ‘asiyefanya kazi na asile’, kwa hiyo kufanya kazi ndio uhai wako, heshima yako na ukizalisha, utaweza kuendesha maisha yako binafsi,” alisema Simbachawene.
Aliongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za Dini, kwani zimekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo, kusimamia maadili na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu wasio na hofu ya Mungu.
Aidha, alibainisha kwamba Serikali inaendelea kuchukua hatua za kisheria kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa, ufisadi, utovu wa nidhamu kwa watumishi wa umma, pamoja na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dk. Maimbo Mndolwa, aliipongeza Serikali kwa kuwa mstari wa mbele kuziunga mkono Taasisi za Dini katika nyanja zote, huku akimtaka Askofu Chiteto kufanya kazi kwa kumtegemea Mungu, hatimaye kufikia malengo ya Kanisa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule aliwataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa ya Serikali kushusha bei ya mbolea kwa kujikita katika kilimo.