KIBAHA
Na Mathayo Kijazi
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amewataka Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), na waamini wote kutambua kwamba wanapomsifu Mtakatifu Agustino, wanapaswa pia kumshukuru Mama yake mzazi Mtakatifu Monica.
Askofu Ruwa’ichi aliyasema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) Kijimbo, katika Kumbukumbu ya Mtakatifu Monica, iliyofanyika katika Seminari Ndogo ya Mtakatifu Maria, Visiga, jimboni humo.
“Tunaadhimisha mambo kadhaa, kwanza kabisa tunawamkumbuka WAWATA, na hususan Mtakatifu Monica, mama yake Mtakatifu Agustino. Huyu ni mama wa mfano, mama aliyetukuka, mama wa kuigwa. Mama huyu alizaliwa mwaka 331 katika Bara la Afrika, huko Afrika ya Kaskazini,” alisema Askofu Mkuu, na kuongeza,
“Alizaliwa na kulelewa vizuri katika familia ya Kikristo, akajenga na kustawisha fadhila zilizo njema; fadhila ya Imani; fadhila ya mapendo; fadhila ya huruma na fadhila za kimama. Tumtukuze Mungu kwa zawadi ya Mama huyu kutoka Bara la Afrika,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Askofu Ruwa’ichi aliwapongeza WAWATA kwa kuendelea kusimama imara na kwa kujitolea kwao katika shughuli mbalimbali za Kanisa, huku akiwasihi kufahamu kwamba wao ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa na Ulimwengu.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimshukuru Mungu kwa utume unaofanywa na akinamama hao, hasa kuwalea Vijana wa Seminari ya Visiga, akimwomba Mungu awazidishie neema na baraka zake, ili utume wao uendelee kustawi, na kuutukuza ukuu wa Mungu.
Askofu Ruwa’ichi aliwasihi WAWATA kutafakari kwamba wao ni baraka kutoka kwa Mungu, kwa uwepo wao wa Miaka 50 sasa, kwani Utume wa Wanaume Wakatoliki (UWAKA), hata miaka 30 bado hawajafikisha, huku akiwasihi akinamama hao kumshukuru Mungu kwa mema yote anayowajalia.
Aidha, aliwaasa WAWATA kuendelea kubaki kuwa Wakristo Wakatoliki wazuri, hata katika Kanisa la nyumbani, kwa kusimama imara na kuwa mama bora, hata katika familia zao.
Kwa upande wao, Maaskofu Wasaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu na Mhashamu Stephano Musomba, waliwapongeza WAWATA kwa kuadhimisha Jubilei yao ya Miaka 50, na kwa kazi nzuri ya utume wanaoendelea nao kuufanya jimboni humo.
Naye, Mwenyekiti wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Stella Rwegasira aliwashukuru waamini wote walioshiriki Adhimisho hilo.
Aidha, Catherine Mwingira, Katibu wa WAWATA Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alisema kuwa wanamshukuru Mungu kwa kufikisha Miaka 50 tangu chama hicho cha Kitume kuanzishwe na waasisi wao, huku akisema kuwa yamefanyika mengi mazuri tangu kuanzishwa kwa chama hicho hadi sasa.
Chama cha Kitume cha Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), kilianzishwa rasmi mwaka 1972.