Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Klabu ya soka ya Simba imesema kuwa kinachoendelea hivi sasa katika sajili zao za wachezaji wa Kitanzania, ni sehemu ya hujuma za kuwachafua ili waonekane hawajui wanachokifanya.
Hivi karibuni Klabu za Coastal Union ya Tanga, Geita Gold ya Geita, na KMC ya Kinondoni, kwa nyakati tofauti zilikuja juu zikipinga sajili za wachezaji wake waliosajiliwa na wekundu hao kwamba hazikuwa halali kwa sababu wachezaji bado wana mikataba nao.
Simba ilimtangaza beki Lameck Lawi kutoka Coastal Union kwamba imemsajili, kisha Valentino Mashaka wa Geita Gold, pamoja na Awesu Awesu wa KMC, lakini hadi sasa imeonekana kukwama kwa Lawi, huku wengine ikiwanasa kwa tabu.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa wekundu hao wa Msimbazi, Ahmed Ally alisema kuwa wanahisi kuna jambo linaendelea, kwa sababu haiwezekani usajili wa wachezaji wa ndani uonekane una makosa, halafu wa wachezaji wa nje uonekane hauna dosari.
“Simba hatujawahi kukosea katika eneo la usajili, na ndiyo maana hata siku moja huwezi kusikia mchezaji katupeleka FIFA kisa anatudai. Tunafanya mambo yetu kwa weledi mkubwa. Leo hii haiwezekani tusajili wachezaji kutoka nje ya Tanzania bila malalamiko halafu ikitokea tunasajili mchezaji kutoka Geita au Kinondoni tu hapo, ikaja kuonekana hatukufuata utaratibu. Hizi ni namna za kutuchafua,” alisema.
Alisema kuwa wamesajili wachezaji wapatao nane wa Kimataifa, lakini hakuna klabu yoyote kutoka nje iliyoibuka kuzungumzia makosa ya usajili kwa wachezaji hao.
Simba imefanya usajili wa wachezaji 13 hadi sasa, ambao ni Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Joshua Mutale kutoka Power Dynamos, Steven Dese Mukwala kutoka Asante Kotoko, Jean Charles Ahoua kutoka Stella Club d’Adjamé na Abdulrazack Mohamed Hamza kutoka Super Sport United.
Wengine ni Valentino Mashaka kutoka Geita Gold FC, Augustine Okejepha Kutoka Rivers United, Debora Fernandes Mavambo Kutoka Mutondo Stars, Omary Omary Kutoka Mashujaa FC, Karaboue Chamou Kutoka Racing Club d’Abidjan, Valentin Nouma kutoka St. Eloi Lupopo, Yusuph Kagoma kutoka Singida Black Stars FC na Kelvin Kijili kutoka Singida Fountain Gate.
Dirisha la usajili kwa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Ligi ya Championship, First League na Ligi Kuu ya Wanawake msimu wa 2024/25 ambalo lilifunguliwa Juni 15, litafungwa Agosti 15 mwaka huu, ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini chini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (Tanzania Episcopal Conference: TEC), wanmekutana katika Mkutano wao Mkuu, huku changamoto za kichungaji, ikiwemo kumomonyoka kwa maadili, zikichukua mjadala mkubwa.
Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, amesema kuwa ni vyema kutafakari vema, kama yote yanayoigwa katika Ulimwengu, yanastahili kuigwa ili kuenenda Kiibada na Kiliturujia.
Kardinali Rugambwa alisema hayo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Maaskofu, uliojadili mambo mbalimbali yanayolihusu Kanisa, Mada kuu ikiwa ni ‘Kuchagiza Hatima ya Waamini Wakatoliki: Changamoto ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Lumen Gentium (Mwanga wa Mataifa), uliofanyika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Kurasini jijini Dar es Salaam.
“Ukitazama baadhi ya mambo yanayoendelea katika Ulimwengu huu, utaona kuwa ni mengi sana. Kwa hiyo tutafakari kwamba, je, yote yanayoigwa katika ulimwengu huu, yanastahili kuigwa ili kuenenda Kiibada na Kiliturujia?
Binadamu wahama misingi ya Imani:
Akizungumzia juu ya mada hiyo kuhusu Changamoto ya Kichungaji katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Lumen Gentium (Mwanga wa Mataifa), Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Mhashamu Isaac Amani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kurugenzi ya Kichungaji, alisema kuwa binadamu wengi wamehama katika misingi ya kiimani, jambo linalosababisha machafuko na ukosefu wa hali ya amani.
Askofu Amani alisema kwamba uwepo wa Watakatifu, ni mwaliko mama, ambao kila mmoja anatakiwa kuufuata ili kuleta tunu ya kiulimwengu.
Wazazi chanzo kubomoka maadili:
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, akichangia mada kuhusu changamoto hizo, alisema kuwa wazazi wanachangia kwa namna fulani watoto kutokuwa na maadili, kwani hawana muda wa kutosha kukaa nao na kujua tabia zao.
“Wazazi wengi hawana muda wa kukaa na kufuatilia mwenendo na tabia za watoto wao, kwa sababu utaona wazazi wanatoka alfajiri kwenda kazini kabla watoto hawajaamka, halafu wanarudi usiku sana, muda ambao watoto wameshalala,” alisema Askofu Mchamungu.
Usafirishaji haramu Binadamu mwiba:
Naye Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi aliwataka wananchi wanaokwenda kufanya kazi katika Mataifa ya mbali kuwa makini, kwani wengi huambulia manyanyaso wanapofika katika Mataifa hayo.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alitoa rai hiyo wakati akichangia mada kuhusu nini kifanyike, katika kupunguza changamoto zinazowakumba watu mbalimbali, hasa suala la biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu.
“Mwezi uliopita nilisafiri kwenda Adis Ababa, Ethiopia, nilipofika kwenye ndege, nikakutana na wanawake ambao nao walikuwa wanasafiri, nikawauliza ‘mnakwenda wapi?’ wakajibu ‘Muscat’, walisema kwamba wametafutiwa kazi huko wanakwenda kufanya;
“Mimi nikawaambia ‘kuweni makini na hizo kazi mlizoitiwa huko, na mkifika huko msikubali kumpa mtu yeyote Passports zenu, kwa sababu mkiwapa watu Passports zenu, mkifanyiwa jambo baya hamtaweza hata kutoroka,” alisema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.
Kwa upande wake Sista Digna Chuwa -CPS, Mratibu wa Mradi wa Taasisi ya TCAS, aliyetoa mada ya usafirishaji wa binadamu, alisema kuwa ipo haja ya kushirikiana na jamii kuzuia biashara haramu ya usafirishaji binadamu, kwani hali hiyo huanzia katika familia.
Vyombo vya Kanisa kunasua mtanziko:
Akichangia kuhusu nini kifanyike, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba alisema kuwa vyombo vya habari vya Kanisa, ni vyema vikatumika ipasavyo, kuandaa vipindi vitakavyosaidia kutoa mafundisho ya imani.
Askofu Kilaini agusia Mtaguso:
Kwa upande wake Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Method Kilaini alisema kuwa lengo la kuwepo na Mtaguso ni kwenda na wakati, na kuweka vizuri Kanisa kuwa na usawa.
Aliongeza kuwa miongoni mwa malengo hayo, ni pamoja na kutengeneza umoja na kuunganisha urika wa Kanisa zima, mambo ambayo yalichagizwa na Baba Mtakatifu kwa ajili ya kuleta amani ndani ya Kanisa.
Akitoa neno la kufunga Mkutano huo wa Maaskofu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,aliyemaliza muda wake, Mhashamu Gervas Nyaisonga, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, aliwashukuru wote walioshiriki mkutano huo, akisema kwamba anaamini kwamba yote yaliyojadiliwa, yatakuwa msaada katika suala zima la Kichungaji.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakatoliki wametakiwa kumtangaza Bwana Yesu Kristo mahali popote, bila uwoga sehemu yoyote na bila kujali jambo lolote na kuacha tabia ya kusaka miujiza.
Wito huo ulitolewa hivi karibuni na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Ambrosi IPTL, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Paul Sabuni katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyofanyika katika Parokia Teule ya Utatu Mtakatifu Skaska, IPTL –Salasala jimboni humo.
“Mkristo yeyote inampasa kumtangaza Kristo popote pale anapokuwepo bila uwoga, kwani hiyo ni njia bora zaidi katika maisha yenu ya kila siku,”alisema Padri Sabuni.
Alisema pia kuwa Waamini wa Parokia hiyo Teule wanatakiwa kuwa na Imani thabiti, isiyo suasua hasa katika kuitangaza Injili.
Aliendelea kusema kwamba watu wengi sasa wamekuwa waoga kuzungumza habari za Yesu Kristo, hata kufundisha habari njema.
“Msije mkatetereka kwa kumwogopa mtu yeyote, kwani mkifanya hivyo mtakuwa mmetenda dhambi kubwa ya makusudi kabisa, kutokana na uwoga ndani mwenu wa kumtangaza Kristo,”alisema Padri Sabuni.
Awakanya wasaka miujiza:
Aidha Padri Sabuni, alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakitangatanga, kutafuta miujiza na kujikuta wakiingia katika sehemu zisizofaa.
Alibainisha kwamba watu wanaopenda miujiza ni watu wenye imani ndogo, akiwasihi Wakatoliki kuishika imani yao.
“Yesu Kristo alisema kwamba katika siku za mbeleni watakuja manabii wengi wa uwongo,basi inawapasa mtambue  kwamba ndio hao wanaowatangazia miujiza kwa sasa,”alisema.
“Inawapasa kushika Imani moja ya Kanisa Katoliki, ambalo lina miujiza, imani kamilifu na muachane na kutangatanga katika madhehebu tofauti, mkifanya hivyo, wewe kama Mkatoliki unamkata Yesu Kristu,”alisema Padri Sabuni.
Padri sabuni pia aliwaomba Waamini wa Parokia hiyo kuchangia Tumaini Media ambayo ina vyombo vitatu navyo ni televisheni Tumaini Radio Tumaini pamoja na gazeti la Tumaini Letu ili Kituo hicho kiweze kupanua wigo wake katika Uinjilishaji.

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI), limesema kuanzishwa kwa ada ya kuendeleza viwanda kwa bidhaa zinazotoka nje kwenye Bajeti Kuu ya Serikali, kutasaidia kulinda viwanda vya ndani, kuchochea uwekezaji, na kuongeza mauzo ya nje.
Mkurugenzi wa Shirikisho hilo, Leodegar Tenga alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maoni ya wenye viwanda waliojadili bajeti hiyo.
Alisema kuwa hatua ya serikali kupunguza ada na tozo zinazotolewa na wakala wa udhibiti ili kupunguza gharama za uzalishaji, kupunguza ushuru wa forodha wa malighafi za viwandani na pembejeo za uzalishaji, kutaongeza ushindani wa viwanda vya ndani.
Tenga alisema kwamba kuondoa kodi ya ongezeko la thamani kwa bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa pamba inayolimwa nchini kutachochea uwekezaji katika tasnia ya nguo nchini.
“Hatua za kodi zilizopendekezwa hapo juu zinalenga kusaidia viwanda vya ndani katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhimiza matumizi ya nyenzo za ndani, kuongeza ushindani, na kukuza ukuaji wa uchumi,” alisema Tenga.
Tenga alipongeza bajeti kuu ya Serikali kwa kuweka mambo muhimu ambayo yatachochea ukuaji wa viwanda nchini.
Alibainisha kuwa Serikali imekuwa sikivu kwa wenye viwanda na kila wanapokuwa na jambo, wamekuwa wakifunguliwa milango ya majadiliano, na kwamba hakuna jambo la wenye viwanda ambalo linakwama.
Tenga aliendelea kusema wenye viwanda wamefurahia sana bajeti ya serikali kwa kuzingatia uendelezaji wa miradi ya kimkakati kama reli ya kisasa (Standard Gauge Railway: SGR) ambayo alisema itasiadia kwa kiwango kikubwa kukuza viwanda vya ndani katika kuzalisha kwa wingi bidhaa.
Azungumzia mradi SGR
Tenga alisema kwamba miradi kama SGR inasaidia kukuza uchumi, kwani viwanda vitazalisha kwa wingi na bidhaa kusafirishwa kwa urahisi kwa haraka tofauti na sasa ambapo usafirishaji umekuwa ukisababisha bei kupanda.
“Nchi ambayo iko makini, inaendeleza miradi mikubwa kama ya ujenzi wa reli, barabara, miradi ya maji kama kuendeleza miradi ya kimkakati ya barabara maji, bandari kwa sabbau huwezi kuendeleza viwanda kama huna umeme au una matatizo ya usafirishaji,” alisema Tenga.
Tenga alifahamisha kwamba bajeti ya mwaka huu inakusudia kuhamasisha mapato ya ndani zaidi ikilinganishwa na bajeti ya 2023/24.
Kwa mujibu wa Tenga, jambo muhimu katika bajeti ya mwaka huu ni Serikali kufanya mageuzi mbalimbali ya muundo wa kodi, ada, tozo na marekebisho ya sheria na kanuni ili kuboresha mazingira ya biashara.
Alisema pia kuwa marekebisho ambayo yamependekezwa kuhusiana na sekta ya viwanda ni katika ongezeko la thamani VAT, ushuru wa bidhaa, ada na tozo za wakala, pamoja na ushuru wa forodha.
Tenga amesema kuwa baadhi ya hatua chanya, ni pamoja na kuanzishwa kwa tozo ya maendeleo ya viwanda kwa bidhaa zinazotoka nje, yenye lengo la kulinda viwanda vya ndani, kuchochea uwekezaji na kuongeza mauzo ya nje; kupunguza ada na tozo zinazotolewa na vyombo vya udhibiti, ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Amesema pia kuwa wamefurahishwa na kupunguzwa kwa ushuru wa forodha kwenye malighafi za viwandani na pembejeo za uzalishaji, ili kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani na kutozwa ushuru wa VAT kwenye bidhaa za nguo zinazotengenezwa kwa pamba inayolimwa hapa nchini ili kuchochea uwekezaji katika viwanda vya nguo vya ndani.
Alisema hatua za kodi zilizopendekezwa hapo juu zinalenga kusaidia viwanda vya ndani katika kupunguza gharama za uzalishaji, kuhimiza matumizi ya vifaa vya ndani, kuongeza ushindani, na kukuza ukuaji wa uchumi.

MOROGORO

Na Mwandishi wetu

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Business Reguratory and Licesing Authority: BRELA), umetaja siri ya mafanikio yake yanayosaidia kufanya kazi zake bila kusabababisha usumbufu.
Mkurugenzi wa Leseni BRELA, Andrew Mkapa,alisema hayo wakati akitoa mada kuhusu utoaji wa leseni za biashara Kundi A.

MAFIA

Na Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, kwa kufanikiwa kuongeza vyanzo vya mapato na kupata hati safi.
Kunenge alisema hayo katika kikao cha kujadili hoja za CAG kilichofanyika wilayani Mafia, Mkoa wa Pwani.

DODOMA

Na Mwandishi wetu

Katibu Tawala Mkoa wa Kilimanjaro, Tixon Nzunda (pichani) amefariki dunia katika ajali ambayo imetokea eneo la Njia panda ya KIA, Wilaya ya Hai, akiwa kwenye ziara mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kwamba ajali hiyo imetokea muda wa saa 8 kuelekea saa 9 mchana Juni 18, 2024.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu, amewaasa Wasimamizi wa vijana wa Sakramenti ya Kipaimara kuhakikisha wanawalea vijana wao kwa kuwaimarisha kiimani.
Askofu Mchamungu alitoa wito huo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara, iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara_Magole, jijini Dar es Salaam.
Askofu Mchamungu alisema kwamba wasimamizi wengi hawajui majukumu yao, japokuwa wanasimamia watoto na kuacha kutimiza wajibu wao.
“Wakifanya sherehe na kula pilau basi hawana muda tena na huyo kijana aliyemsimamia, ndugu zangu wasimamizi mnaosimamia iwe Ubatizo, Kipaimara,  na waomba sana majukumu yenu mhakikishe mnayatimiza,”alisema Askofu Mchamungu.
Aidha, aliwasihi vijana hao kutoacha kwenda kanisani, kwani kufanya hivyo, watayumbishwa kiimani.
“Msiache kuja kusali, muwe watu wa sala kila muda… lakini pia ndugu zangu waamini, nanyi msije mkadanganywa na manabii wasio na Imani Takatifu Simameni imara siku zote,”aliongeza kusema Askofu Mchamungu.
 Askofu Mchamungu aliwaomba watu wenye ndoa kuhakikisha wanaiishi Sakramenti yao vizuri, bila kuwa na vikwazo vya mivurugano katika ndoa zao.
Askofu Mchamungu aliwapongeza Waamini kwa kupanda hadhi na kuwa Parokia kamili, akiwasihi kuungana ili Parokia yao isonge mbele.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Singano, alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuwapatia vijana Sakramenti ya Kipaimara.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Bonaventura - Kinyerezi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Francis Hiza, amewataka Waamini kutoshabikia unafiki, kwani hauna faida yoyote maishani.
Padri Hiza (pichani) alisema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Dominika, iliyoadhimishwa parokiani hapo.
“Tujitahidi sana katika maisha yetu, tusiupe nafasi unafiki, kwa sababu hauna faida yoyote katika maisha ya Mkristo, na pia hauna faida ndani ya Kanisa;
“Wewe kama Mkristo, usikate tamaa katika maisha yako, kwa sababu licha ya changamoto unazozipitia, Mungu yuko pamoja nawe,” alisema Padri Hiza.
Padri Hiza aliwatada Waamini kutojiingiza katika dhambi ya ushoga, akisema kuwa dhambi hiyo ni kubwa sana, na anayejiingiza humo, hawezi kusamehewa na Mungu.
Padri huyo aliwasisitiza Waamini kulijenga Kanisa la ndani, yaani mioyo yao, kabla ya kulijenga Kanisa la nje, yaani Kanisa jengo.
Aidha, aliwakumbusha kujenga tabia ya kuwapenda zaidi wengine, badala ya wao kusubiri tu kupendwa, kwani upendo huo una nguvu kulingana na Maandiko Matakatifu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tumaini Media aliwashukuru Waamini wa Kinyerezi kwa majitoleo yao ya kuitegemeza Tumaini Media, huku akiwaomba kuendelea kukitegemeza chombo hicho.
Padri Massenge ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu,  Makongo Juu, alitumia nafasi hiyo kuwaomba waamini hao, kuendelea kuvitumia vyombo vya habari vya Tumaini Media.
Alisema pia kuwa hata pale watoto wao wanapotaka kutazama Televisheni, wajitahidi kuwawekea chaneli ya Tumaini Tv.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mstaafu wa  Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amesema kuwa watu wanaolitangaza jina la Mungu katika mazingira yoyote, hueleweka.
Kardinali Pengo alisema hayo wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Clara wa Asizi - Chamazi, jijini Dar es Salaam.
“Watoto wa Kipaimara, jitahidini sana kulitangaza jina la Mwenyezi Mungu katika maisha yenu. Watu wanaolitangaza jina la Mungu katika mazingira yoyote yale, watu hao hueleweka,” alisema Kardinali Pengo.
Aidha, Kardinali Pengo aliwasisitiza vijana waliopokea Sakramenti hiyo kutambua kwamba, lengo kuu la kupokea Sakramenti kuja kulitangaza Neno la Mungu.
Aliongeza kuwa siku watakaposahau kwamba lengo lao kuu ni kulitangaza Neno hilo, basi watajikuta wanaingia katika vurugu.
Wakati huo huo Kardinali Pengo, aliwaasa Waimarishwa hao kuepuka kuwa waoga, badala yake watambue kwamba wanasimama kwa niaba ya kundi lililoamini kuwa Kristo alifufuka katika wafu.
Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo aliwapongeza waamini wa Parokia hiyo, kwa kuwa na kanisa kubwa na la kisasa, akiwasihi kuongeza nguvu ili kukamilisha maboresho yaliyobaki kwa sasa.