Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

VATICAN CITY, Vatican

Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa (UN), Askofu Mkuu Mhashamu Gabriele Caccia ameakisi malengo ya kipaumbele ya ufadhili wa maendeleo, akisema kwamba kufutwa kwa deni ni muhimu ili kuhakikisha utu na ukuaji kwa Mataifa dhaifu zaidi unakuwepo.
Askofu Mkuu Caccia aliyasema hayo katika kikao cha Kamati ya maandalizi ya Mkutano IV wa Kimataifa juu ya Ufadhali wa Maendeleo, uliofanyika hivi karibuni huko New York Marekani.
Akitoa hotuba yake katika kikao hicho, alisema kwamba Uwakilishi wake unapenda kutoa shukrani zake kwa Ureno na Burundi kwa uongozi wao kama Wenyeviti Wenza wa mchakato huo muhimu, na kwa Hispania kwa ukarimu wake wa kujitolea kuwa mwenyeji wa Mkutano ujao wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FfD4), huko Seville.
“Zaidi ya hayo, shukrani zinatokana na Wawezeshaji Washirika, yaani Nepal, Norway, Mexico, na Zambia, kwa juhudi zao katika kuandaa Waraka wa Mambo, ambao unatoa msingi thabiti wa kazi kuelekea hati ya matokeo yenye matarajio na matokeo. Ni jambo la kupongezwa kwamba Hati ya Vipengele kwamba inatambua changamoto kuu zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa,” alisema Askofu Mkuu Caccia.
Aliongeza pia kuwa juhudi za ufadhili wa maendeleo katika muongo mmoja uliopita zimeshindwa kushughulikia ipasavyo kukosekana kwa usawa na udhaifu unaoendelea, ambao unazidishwa na migogoro inayoingiliana.
Aidha, alibainisha kwamba hiyo imechelewesha malengo ya Maendeleo Endelevu, na hivyo kufikia maendeleo muhimu ya binadamu, akiongeza kuwa Dira Kabambe ya Maendeleo Endelevu, lazima iendane na hatua madhubuti.
Sambamba na hayo, alisema kuwa njia za utekelezaji ni muhimu kufikia malengo ya pamoja, na kwamba ujumbe wa Vatican unakaribisha kuwa Waraka huo unatambua maeneo kadhaa muhimu, ikiwa ni pamoja na mambo mengine, ikiwemo uharaka wa kuweka kipaumbele kwa mahitaji ya nchi zilizo katika hali maalum, ambazo ni Nchi Chini zisizoendelea, Nchi zinazoendelea zisizo na Bandari, na Nchi za Visiwa Vidogo Vidogo zinazoendelea.
Alibainisha pia kwamba Nchi hizo ziko mstari wa mbele katika changamoto za Kimataifa, na kusema kuwa lazima ziwe katikati ya juhudi zao za pamoja za ufadhili.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Caccia, Vatican inakaribisha kwamba hati hiyo inasisitiza kuoanisha msaada na vipaumbele vya kitaifa kuwa ni muhimu ili kuhakikisha masuluhisho endelevu na mahususi ya muktadha, yanatambua hitaji la kuongezeka kwa ufadhili wa hali ya Tabianchi.
Akifafanua kuhusu suala la deni, Askofu Mkuu Caccia alieleza kuwa Vatican inaunga mkono mwito ulio kwenye Waraka wa Mambo kwa ajili ya ahadi thabiti zaidi kuhusu usimamizi, uendelevu na urekebishaji wa madeni.
Hata hivyo, alisema kuwa ili kukidhi mahitaji ya maendeleo na hali halisi ya wote, Ujumbe wake unaamini kuwa matarajio makubwa ni muhimu, na yanaweza kufikiwa.
Aliongeza kwamba Baba Mtakatifu Fransisko ameyataka Mataifa tajiri kuchukua hatua ya kijasiri ya mshikamano, ili kusaidia kufuta madeni ya Nchi zinazoendelea ambazo hazitaweza kuyalipa.
Alisema kwamba wanapokaribia Mkutano ujao wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FfD4), huko Seville, Vatican inasisitiza umuhimu wa kutanguliza uondoaji wa umaskini kama lengo kuu la juhudi zote za ufadhili.
Alibainisha kwamba umaskini si changamoto ya kiuchumi tu, bali pia ni ukiukwaji mkubwa wa utu wa mwanadamu aliopewa na Mungu, na ni kikwazo kikuu cha maendeleo endelevu, na hivyo mijadala yao lazima itambue ipasavyo kwamba umaskini unasalia kuwa changamoto kubwa zaidi duniani.
Kwa mujibu wa Askofu Mkuu Caccia, ili kutokomeza umaskini kama lengo kuu la juhudi zao, watahakikisha kwamba matokeo ya Mkutano huo yatashughulikia mahitaji ya dharura, zaidi ya yote.

DAR ES SALAAM

Na Paskazia Nestory

Jamii ya siasa kwa hivi tuna mambo mengi yanayotuzunguka, mathalan harakati nyingi, mipango mingi shughuli nyingi na zinatufanya tukose muda wa kuongea na Mungu hasa katika sala kusoma Neno la Mungu, na kutafakari.
Hali hii inapelekea kuwa na mikwamo kila mahali kwenye familia, jumuiya, vikundi vya sala Kanisa na Taifa.
Kiongozi yeyote anahitaji kuombewa ili aweze kuongoza vyema sehemu anayokuwa amesimamia.
Madhara yanaweza kujitokeza kwa kukosa kuwaombea viongozi. Biblia inahitaji sehemu mbalimbali kuhusu maombi kwa ajili ya viongozi,  Esta, 4:16 Esta anakubali ushauri wa mjomba wake Modekai anaamua kufunga kusali na kuomba kwa ajili ya (Wayahudi) Taifa la Israeli, na kumwomba Mungu ampe kibali cha kuingia kwa mfalme.
1.Tuanzie kwenye familia:
Kiongozi wa nyumba (baba na mama) akiyumba, nyumba yote inafarakana. Malezi ya watoto yanakuwa hafifu na matarajio ya familia yanapotokea.
2. Kanisa Kiongozi wa Kiroho akiyumba, Kanisa lote linakosa msimamo. Waamini  wanakosa imani na Kanisa lao na kiongozi wao, na kondoo wengi wanatangatanga, Efeso, 6:18 Mtume Paulo anakazia jambo hilo kwani ni himizo kwa kila Mkristo kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho Mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea Watakatifu wote.
Kwa mambo mengi tuliyonayo sisi, tumewachosha viongozi wetu wa Kanisa. Tunawapelekea mizigo mizito ili waitatue, lakini wao wanashindwa kutatua migogoro yetu, hatuwaombei, nao hawana nafasi ya kutosha kujiombea wenyewe.Tunapowachosha huduma zao zikaenda ndivyo sivyo, tunawanyooshea vidole.
Kama wewe ni Mkristu Mkatoliki, nakuomba usifanye hivyo kama kiongozi wako wa kiroho akikengeuka. Kitu cha kwanza mwombee bila kuongea chochote, maana ukifanya hivyo, Mungu yupo tayari kusamehe. Lakini kama unaona kuongea kama watu wengine wa mataifa kama biblia inavyotaja, kutakusaidia utajidanganya na utabeba dhambi yake na yako. Tukumbuke hawa ni wapakwa mafuta (makuhani) yatakupata yaliyompata. Aroni na dada yake Miriam, Mwenyezi Mungu anatafuta mtu mmoja tu kujenga mahali palipobomoka Ezek, 22:30.
Hawa ni ndugu zetu, watoto wetu, kaka zetu na jamaa zetu. Tunawapenda na kuwathamini ili huduma yao iwe nyepesi.
Viongozi wa Nchi:
Tusipowaombea Viongozi wa nchi jua kazi kubwa iko kwetu. Tusisubiri kwenye ibada za Jumapili, shetani muda wote yuko kazini.
Uongozi ni mzigo na kama ujawahi kuwa kiongozi mahali popote hata kuwa kaka au dada wa darasa, huwezi kufahamu jambo hili.
Ukimwona mjumbe wa mtaa anaboronga, usipambane nae mwombee tu, Mungu wetu si mwanadamu anashughulika naye. Vile vile Muheshimu amebeba dhamana kubwa.
Viongozi wakubwa, wanakutana na mambo makubwa wanapambanishwa na mambo mengi. Hata wa Dini wakipata madaraka makubwa, kiburi kunaweza kuinuka ndani yao na kuanza kutoa amri kama wanavyotaka wao, bila kufuata sheria kanuni, na miongozo husika. Upinzani unaanza machafuko na mafarakano yanaanza kati ya kiongozi na waongozwa.
Tuombe neema ya kutubu:
Ee Bwana kumbuka yaliyotupata, utazame na kuona aibu yetu, urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni wa nyumba zetu kuwa mali za makafiri Maomb, 1:5,1-2 Kiongozi wa nchi akifanya yasiyompendeza Mungu, Taifa lote linaingia hatarini, haijalishi maskini, tajiri wala mwenye cheo, Tuombeane ili Mungu atusaidie katika madhaifu tuliyonayo.
Kama hawa Viongozi tunawapelekea shida zetu ili wazitatue, je, shida zao wao wanazipeleka kwa nani?
Sisi ndio tunapaswa kupeleka chngamoto kwa Mwenyezi Mungu ili awape nguvu ya kutenda kazi yake.

Na Remigius Mmavele

Sehemu ya Pili

ILIPOISHIA
Uhamisho wake kwenda Loketo ulikuwa wa kuvutia sana kwa sababu rafiki yake Awilo Longomba alitaka ajiunge na kundi la Papa Wemba, Viva la Muzika.
ENDELEA...

Wakati huo huo, Aurlus Mabele aliyekuwa kaka mkubwa jirani na pia binamu yangu, Lucien Bokilo na Jean Baron(marehemu), walimfuata na kumwambia kuwa aende akajiunge na kundi la Loketo.
Hiyo ilikuwa mwaka 1988, ndipo Bokilo alijiunga na kundi hilo akiwa mwenye umri mdogo kuliko wanamuziki wenzake wote.
Miaka michache baadaye, kulitokea kutokuelewana katika bendi kati ya Diblo Dibala na wenzake, jambo ambalo lilifanya bendi isimame kufanya kazi kwa miezi michache.
Kipindi hicho ndipo mwimbaji Ballou Canta alimwomba ajiunge na kundi la Soukous Stars, naye bila hiyana, akakubali kujiunga na kundi hilo, na wakatoa album yao ‘Soukouss Stars in Hollywood (1993)’, ambayo alitunga Wimbo ‘Robin Pretty’.
Kuna wakati Bokilo aliwahi kulitumikia kundi la Nouvelle Generation (Zipompa Pompa), ambalo lilikuwa chini ya Luciana Litemo Demingongo, kundi ambalo lilianzishwa Oktoba 13 mwaka 1992. Alilitumikia kundi hilo kwa kipindi kifupi sana.
Lucien Bokilo alikuwa na urafiki wa muda mrefu na Awilo Longomba ambaye walikuwa marafiki wakiwa mtaani, na baadae walikuja kufanya kazi pamoja wakiwa katika kundi la Loketo. Wakati huo, Awilo Longomba alikuwa mpiga ngoma,akiwa hajaanza kuimba.
Bokilo ndiye aliyemshawishi Awilo aanze kuimba, kwa kuwa aliamini kuwa ana uwezo wa kuimba. Lucien Bokilo alipotoa albamu yake ya kwanza ‘Le Jeu Est Fin,’ Awilo alifanya naye kazi pamoja akiwa mpiga ngoma katika nyimbo saba zilizo kwenye albamu hiyo.
Lucien Bokilo na Jean Baron ni mtu na binamu yake, ingawa Bokilo akiwa bado kijana mwenye umri wa miaka 6 au 7, Jean Baron alihamia jiji tofauti na alipokuwa anaishi Lucien Bokilo. Hivyo, ikapita miaka mingi bila kuonana na walipoteza kabisa mawasiliano.
Baada ya kupita miaka mingi, walikuja kukutana tena Jijini Paris nchini Ufaransa, wakafanya kazi pamoja katika bendi ya Loketo.
Mwaka 1991, Lucien Bokilo alitoa albamu yake ya kwanza inayoitwa ‘Le Jeu Est Fin’ ambayo ina jumla ya nyimbo saba ambazo ni La Vie La Vie, La S.A.P.E, Adidja, Le Magnifique, Leonore, Le Jeu Est Fin, na Tchao Je Me Casse.
Waimbaji katika albamu hiyo walikuwa Lucien Bokilo, Joe Fataki na Ballou Canta. Wapiga gita walikuwa Rigo Star (Solo & Rythm), Dally Kimoko (Solo), Remy Salomon (Bass). Ngoma zimepigwa na Awilo Longomba.
Mwaka 1995 Bokilo alitoa albamu ya Pili inayoitwa ‘One Way’ ambayo waimbaji walikuwa Lucien Bokilo na Ballou Canta, huku wapiga gita wakiwa Alain Makaba, Rigo Star, Nene Tchakou (Solo), Ngouma Lokito (Bass), Lokassa ya Mbongo , Rigo Star (Rhythm) na Rapa alikuwa Lucien Bokilo na Awilo Longomba.
Albamu hiyo ina nyimbo nane ambazo ni One Way, Missete, Djoukende, Accro De Toi, Aziza, Retourne Toi, Mwasi, Ngoma.
Lucien Bokilo alitoa albamu yake ya tatu yenye nyimbo kumi na mbili mwaka 1998 ambayo inaitwa ‘Africation’ ambayo waimbaji ni Ballou Canta, Lucien Bokilo, Nyboma Mwandido, Shimita El Diego. Wapiga gitaa Caien Madoka , Dally Kimoko, Freddy Fumunani (Solo), Caien Madoka , Lokassa ya Mbongo (Rhythm), Ngouma Lokito ( Bass).
Baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu akifanya maonyesho katika nchi mbalimbali barani Afrika na Ulaya, Lucien Bokilo alitoa wimbo mmoja mwaka 2020 ambao unaitwa ‘Welcome to Colombia.’
Katika kazi zake za muziki, Bokilo amewahi kushirikiana na Kanda Bongoman katika baadhi ya maonyesho ya Kanda Bongoman. Pia alikuwa mmoja wa wanamuziki walioshiriki kwenye albamu ‘Mariana’ iliyotoka mwaka 1995 ambayo ilishirikisha wanamuziki wengi maarufu ambao ni Aurlus Mabele, Lucien Bokilo, Tchico Tchicaya, Soule Ngofoman, Chantal Fernand, Andre Marcellin, Eitel Meva’a, Hugues Exillie, Marika Fostin.
Wapiga gita Alain Makaba, Blandin Wabacha , Dally Kimoko (Solo), Aladji Toure, Ngouma Lokito (Bass), Blandin Wabacha, Dominique Gengoul, Lokassa ya Mbongo, Yves N’Djock, na ngoma zimepigwa na Awilo Longomba.
Mwaka 1996 waimbaji wengine wawili wakubwa wa Kongo, Pierre Belkos na Ballou Canta walijiunga naye kuunda B3 (trio) Mapapou. Kundi hilo lilipata mafanikio ya haraka na kufanikiwa kutoa albamu yao “Samedi ... Ca ma dit,” yenye nyimbo kumi na moja, na alifuatana na Bokilo katika ziara ya dunia ya mwaka 1997, ikiwa ni pamoja na nchi kama Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Saudi Arabia, Japan, Ureno, na Afrika nzima.
Nyimbo kumi na moja zilizomo katika albamu “Samedi ... Ca ma dit,” ni Yo! (Ballou Canta), “Samedi ... Ca ma dit,”(B3 Mapapou), Au fond de toi (Lucien Bokilo), Kongossa (Ya Pas defi) (Pierre Belkos), Decollage (Ballou Canta), Kissalu (Lucien Bokilo), Bellede Loango (Ballou Canta), Party(Fete)(Lucien Bokilo), Beleza (Classe Tendresse)(Pierre Belkos), Mukento (Pierre Belkos),na Ata Ozali (Franklin Boukaka).
Waimbaji vinara katika albamu hii ni Pierre Belkos, Lucien Bokilo, Ballou Canta. Wengine ambao sio waimbaji vinara ni Valerie Tribord na Marie Paule Tribord.
Wapiga magitaa Alain Makaba, Caien Madoka , Nene Tchakou (Solo), Caien Madoka (Rhythm), Ngouma Lokito, Miguel Yamba, Guy N’sangue (Bass) na Rapa ni Jean Didier Loko (JDL).
Katika wimbo wake ‘Welcome to Colombia’ uliotoka mwaka 2020, Bokilo anasema alishawishika kutunga wimbo huo baada ya kuguswa na ukaribisho alioupata alipotembelea nchi hiyo. Wimbo huo Solo gitaa limepigwa na Diblo Dibala, Besi limepigwa na Ngouma Lokito, Rhytm gitaa limepigwa na Lokasa ya Mbongo, ikiwa ndiyo kazi yake ya mwisho kufanya na Bokilo, kabla hajafariki.
Waimbaji wengine walikuwa kutoka nchini Colombia pamoja na Patchy Langi na Wawali Bonane.                                           

Na Arone Mpanduka

Katika miaka ya 1990 na kurudi nyuma, bendi nyingi nchini zilikuwa na ushindani mkubwa wa kimuziki, kulingana na mazingira halisi waliyokuwa nayo katika miaka hiyo, tofauti na sasa.
Sasa hivi muziki wa dansi Tanzania, pamoja na wanamuziki wake, umekuwa ukichechemea kufuatia mabadiliko makubwa ya teknolojia ambayo yameegemeza zaidi katika miziki ya kizazi kipya.
Upekuzi na udadisi wangu umebaini mambo kadhaa kuhusiana na muziki wa zamani, namna ulivyokuwa unaandaliwa, na wanamuziki wenyewe walivyokuwa wanajinoa kabla wimbo haujafika kwa wasikilizaji.
Yapo mambo kama 6 hivi ambayo yalikuwa yakifanyika, na hatimaye wimbo pendwa unakwenda sokoni ukiwa umekamilika na watu wakaufurahia.
UTUNZI WA WIMBO
Katika miaka ya zamani, bendi nyingi za muziki zilikuwa zikihusisha wanamuziki wengi ambao walikuwa wanaimba pamoja kwenye kumbi za starehe, na hata studio walikuwa wanakwenda pamoja kurekodi.Hii iliwarahisishia watunzi kutunga nyimbo zao kwa kushirikiana na kundi zima.
Mtunzi alikuwa anaweza kutunga wimbo wake, kisha akaufanyia uhakiki yeye mwenyewe ili kujiridhisha kama unafaa kuwapelekea wenzake, ama la.
Tungo ya muziki inaweza ikawa inazungumzia siasa, mapenzi, ama masuala yoyote yanayohusu maendeleo ya nchi, na mara nyingi walikuwa wakitunga kulingana na matukio halisi wanayoyashuhudia, na kisha kujazia na vionjo vingine vya kubuni ili kuleta ladha.
KUSHIRIKISHA WANAMUZIKI WENGINE
Baada ya kujiridhisha na tungo yake, mtunzi alikuwa anachukua andiko lake na kwenda nalo mazoezini na kuwashirikisha wenzake. Na hapo kila mmoja alikuwa makini kuangalia nini cha kuongeza, ili wimbo uwe mzuri kusikilizwa na kuchezwa na watu ukumbini.Na kama ikitokea wimbo haufai kabisa, labda kwa kukosa maadili, mtunzi hulazimika kurudia upya kuandika tungo zake, na kisha kuurudisha tena kwa wenzake.
Hapo mtunzi hulazimika kutafuta ‘tone’ ya kuimba mbele ya wenzake, huku wapiga gita, kinanda na ngoma wakiwa makini kusikiliza ili kuona vyombo vyao wanavipiga kwenye maeneo gani ya mistari hiyo.
KUUJARIBU WIMBO HADHARANI
Baada ya hapo, wanamuziki wote wa bendi hukubaliana kuujaribu wimbo huo mbele ya mashabiki zao, hasa pale wanapokwenda kutumbuiza nyimbo zao ambazo zimeshaingia sokoni. Kwa mfano, wanaweza kwenda kutumbuiza ukumbi wa DDC Kariakoo, na hatimaye huchomekea wimbo mpya na kisha kusikilizia hisia za mashabiki juu ya wimbo huo.
Wakati hayo yanafanyika, kunakuwa na kiongozi wa jukwaa ambaye kazi yake ni kuangalia muunganiko kati ya mashabiki na kile kinachotolewa na wanamuziki kupitia sauti zao, na mchanganyiko wa vyombo vyao.
MASAHIHISHO
Kama ikitokea mashabiki wamepoa wakati wimbo mpya unapigwa, basi kiongozi huyo wa jukwaa huamuru wimbo urudiwe mara kwa mara, na hali ikibaki hivyo, wakirudi kambini wanashirikiana kutafuta wapi walipokosea ili warekebishe.Hapo wanaweza kubadilisha hata staili ya kinanda, ama baadhi ya waimbaji. Na baada ya hapo, huujaribu tena kwenye onyesho lingine. Ikitokea mashabiki wameupokea wimbo kwa furaha, basi hukubaliana kwamba urekodiwe studio.
KUHAKIKIWA STUDIO
Kama wimbo umependwa na mashabiki, hupelekwa studio haraka kwa ajili ya kujadiliwa na kuhakikiwa ili itoke ruhusa ya kurekodiwa. Studio zenyewe kwa wakati huo zilikuwa ni za Redio Tanzania Dar es salaam (RTD), sasa hivi zikifahamika kama Tanzania Broadcasting Corporation (TBC).
Hapo wimbo unachujwa tena na kuboreshwa na wataalamu waliosomea muziki na lugha ya Kiswahili.Hiyo ilikuwa ni Kamati Maalum ambayo kazi yake ilikuwa ni kupitia nyimbo zilizoandikwa kwenye karatasi, na kisha huruhusu bendi kwenda kurekodi.
KUREKODI
Baada ya wataalam kuhakiki, walikuwa wakitoa ruhusa ya kurekodi wimbo ambapo kwa mujibu wa teknolojia kwa wakati huo, walitumia ‘Two track recording,’ mfumo ambao ulilazimisha mwanamuziki yeyote arekodi bila kukosea, akiwemo mwimbaji, mpiga ngoma, gita n.k. Na kama ikitokea mmoja amekosea, kazi huanza upya. Muda wao ulikuwa kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 kasoro, jioni.
Mfumo huo ulikuwa shirikishi, kwani ulilazimisha wanamuziki wa bendi nzima kuingia studio na kufunga vifaa vyao vya muziki, na kisha kurekodi.
Hizo ndizo njia 6 ambazo wanamuziki wa zamani walizitumia katika kuandaa wimbo hadi kuwafikia wasikilizaji.
Katika miaka ya sasa hali imebadilika kwani msanii anaweza kurekodi kwa kurudiarudia, kisha producer anakata vipande vilivyokosewa na kuacha vilivyo sahihi, na pia miaka ya sasa, msanii anaweza kutuma sauti yake kwa njia ya Whatsapp na kisha huchanganywa na za wengine, ili kukamilisha wimbo.

Canberra, Australia
Bingwa wa Olimpiki wa discus Roje Stona na mchezaji wa kimataifa wa Rugby wa Australia Jordan Petaia, watakuwa miongoni mwa kundi la hivi punde la wanariadha watakaoshiriki katika Njia ya Wachezaji wa Kimataifa ya NFL.
Tangu programu ya IPP ianzishwe mwaka wa 2017, wachezaji 41 wa kimataifa wamejiunga na timu za NFL, huku 23 wakiwa na timu kwa sasa, na sita wameingia kwenye orodha inayotumika ya timu.
Mpango wa IPP hutambua vipaji vya kimataifa, na huwapa wanariadha fursa ya kukuza ujuzi wao wa soka wa Marekani, na uwezekano wa kupata nafasi kwenye orodha ya NFL.
Mnamo Januari, wanariadha 14 wataenda kwenye kambi ya mafunzo ya wiki 10 huko Florida, inayojumuisha vipindi vya uwanjani na darasani, kabla ya kuonyesha ujuzi wao kwa maskauti wa NFL kabla ya rasimu ya NFL ya mwaka ujao.
Stona, 25, alifanya mazoezi na timu mbili za NFL majira ya kuchipua mwaka jana, kabla ya kushinda medali ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki ya Jamaica katika mchezo wa kutupa tufe huko Paris 2024.
Petaia, 24, alikuwa tayari amehusishwa na kuhama chama cha raga na atalenga kumwiga Mwaustralia mwenzake Jordan Mailata.

NEW YORK, Marekani
Juan Soto anatazamiwa kusaini mkataba ambao unadaiwa kuwa mkubwa zaidi katika historia ya michezo baada ya kukubali mkataba wa $765m (£600m) kwa miaka 15 na New York Mets ya Ligi Kuu ya Baseball.
Vyanzo vingi vya habari nchini Marekani vimefichua maelezo ya mpango huo, ingawa Mets bado hawajathibitisha hilo kwa sababu raia huyo wa Dominican mwenye umri wa miaka 26 anahitaji kukamilisha uchunguzi wa kimatibabu.
Soto aliwekwa kuwa wakala wa bure anayetafutwa zaidi na MLB katika msimu huu wa nje baada ya kuwa na msimu bora wa maisha yake akiwa na Yankees ya New York, tena akionyesha uwezo wake wa hali ya juu wa kupata msingi.
Ana asilimia kubwa zaidi ya kazi kwenye msingi kati ya wachezaji wanaocheza (0.421), ni mchezaji mwenzake wa Yankees Aaron Judge ndiye aliyekuwa na OBP bora zaidi mnamo 2024 na ni wachezaji watatu pekee waliopiga mbio zaidi za nyumbani.
Tovuti ya MLB ilisema, Soto nje ya mshahara wake lakini atapata bonasi ya kusaini ya $75m, bila pesa iliyoahirishwa, katika mkataba ambao unaweza kuwa na thamani ya hadi $800m (£627m).
Thamani ya jumla ya mkataba huo inapita mkataba wa miaka 10 wa $700m (£558m) ambao Shohei Ohtani alisaini na Los Angeles Dodgers mwaka jana, huku nyota huyo wa Japan akikubali kuahirisha $680m (£541m) ya kiasi hicho.
Baadhi ya wachezaji wengine wakubwa ni pamoja na beki wa Dallas Cowboys Dak Prescott kuwa mchezaji anayelipwa pesa nyingi zaidi katika historia ya NFL mnamo Septemba kwa kukubali kuongezwa kwa mkataba wa miaka minne wenye thamani ya $240m (£183m).

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Visiwani Zanzibar nako wana michezo yao inayopendwa zaidi kama Tanzania Bara ilivyo na michezo yake ikiwemo ya asili.
Ni michezo ambayo huchezwa kwa kuhusisha rika la watu tofauti, na hufanyika haswa wakati wa mapumziko ikiwemo jioni baada ya watu kumaliza shughuli zao za kujitafutia kipato.
MAKACHU
Makachu ni mchezo wa asili ya Kizanzibari unaochezwa zaidi na vijana wenye ujuzi wa kujitupa majini kutoka umbali mrefu wa nchi kavu, na kisha kuogelea.
Zamani, mchezo huo ulikuwa kama wa kujifurahisha lakini sasa hivi unatumika kuwaingizia pesa vijana ambao hufanya matangazo kwa kubeba mabango yenye maandishi ama bendera, na kisha kukimbia nayo kwenye usawa wa bahari, na kujitupa majini. Tukio hilo husindikizwa na kamera ili kunogesha tangazo.
Hata watalii wanapokwenda Visiwani humo huwalipa pesa vijana na kisha huandika majina yao kwenye bango, mfano “Welcome Mr John,” na kukimbia na hilo bango baharini na kujitupa nalo kwenye maji.
NGWARE
Ngware ni mchezo wa kupiga mtu mtama.Kwa ujumla, ni mchezo unaotumia miguu na mikono katika uchezaji wake.
Mchezo huu unaweza kusema hauna tofauti na mieleka kutokana na uchezaji, ukamataji wake, hata watu kuangushana kwao hadi kupatikana mshindi.
Katika kisiwa cha Pemba Wilaya ya Micheweni, ndiko mchezo huo unakochezwa tangu miaka 30 iliyopita. Katika Bara la Afrika ni mchezo mkubwa sana, na zaidi huchezwa Senegal. Kidunia huchezwa Japan, na hutumiwa na wachezaji wanene.
Kwa sasa, mchezo wa ngware haumo tena kwenye mashindano ya Olympiki, mara ya mwisho mchezo huo uliondolewa mwaka 2020.
Ulingo wake unatakiwa ujengwe juu kidogo kama wa ‘boxing’, ili kuwafanya watu weweze kuona pande zote.
Mchezo hushirikisha timu mbili A na B, kila timu inatoa mchezaji mmoja, ambapo watakuwa katikati, na mwamuzi mmoja wa kuamua mshindi wa mchezo huo.
Anasema wachezaji hukamatana mikono kwa ukakamavu wa hali ya juu, hapo tena ndipo wanapopigana Ngware (mtama), ili mmojawapo amwangushe mwenzake chini na hivyo kuwa mshindi.
NAGE
Nage ni mchezo mwingine unaochezwa sana Zanzibar.Zamani watoto waliucheza sana vijijini lakini sasa hivi hata watu wazima wanaocheza, hasa wanawake.
Mchezo huu unafanana na rede, lakini unashirikisha wanawake wanne na kuendelea, na ukaaji wao ni tofauti, kwa kuwa wachezaji hujipanga pande nne, na mchezeshaji mmoja hukaa katikati, ili apate mpira ambao walio nje ya duara, wanarushiana. Akifaulu kuudaka, hujiunga na wachezaji walio katika duara, na aliyeurusha anaingia katikati badala yake.
BAO
Ni mchezo ambao hupendwa sana Visiwani humo, ambapo wanaume huucheza sana hasa wanapomaliza shughuli zao za uvuvi na biashara za pweza na samaki.
Kiutamaduni wengi hucheza wakiwa wamevaa misuli, huku wakisimuliana mambo mbalimbali.
Ikumbukwe zamani Hayati Abeid Aman Karume alikuwa anapenda sana kucheza mchezo huo, na hata tukio la kupigwa risasi na kusababisha kifo chake, lilitokea wakati akiwa anacheza mchezo huo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wapinzani wa Yanga katika kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Hilal ya Sudan, wameliandikia barua Shirikisho la Soka Afrika CAF kuomba mechi zao za kimataifa zichezwe nchini Libya.
Al Hilal kwa sasa wanatumia nchi ya Maurtania kama nyumbani katika mechi za kimataifa ambapo hivi karibuni ilimualika TP Mazembe na kumnyuka 2-1.
Kwa mujibu wa mtandao wa michezo wa Libya Observer, Al Hilal imeandika barua kisirisiri kwenda CAF ikitaka kutumia uwanja wa Benghazi.
Kama endapo CAF watakubali ombi la Al Hilal, mechi ijayo ya hatua ya makundi kati yao na Yanga itachezwa nchini Libya katika dimba la Benghazi.
Mechi ya marudiano ya makundi kati ya Al Hilal na Yanga imepangwa kuchezwa Januari 10 mwakani 2025.
Yanga bado ina kisasi kikubwa na Al Hilal baada ya kufungwa mara mbili na timu hiyo, ambapo mwaka juzi ilikwama kule nchini Sudan katika mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa ya kuwania nafasi ya kuingia hatua ya makundi kwa kufungwa 1-0.
Safari hii Yanga alifungwa tena katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi kwa kupokea kichapo cha 2-0 nyumbani kwenye dimba la Benjanim Mkapa, huku kocha akiwa yule yule Florent Ibenge.
Msisitizo walionao Yanga kwa sasa ni kuhakikisha wanashinda mechi zilizo karibu yao kwa mujibu wa ratiba, na kisha waanze kuipigia hesabu Al Hilal ambayo imekuwa mfupa mgumu msimu huu.
“Tupo kwenye kipindi kigumu, lakini hatupaswi kuangalia yaliyopita, sisi kazi yetu ni kusonga mbele kama kaulimbiu yetu inavyosema, ya ‘Daima Mbele, Nyuma Mwiko’. Tunaomba mashabiki wetu waendelee kuwa nasi. Malengo yetu bado ni yaleyale ya kufika mbali katika mashindano ya kimataifa,”alisema Alex Ngai, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Yanga.
Yanga hadi sasa imepoteza mechi mbili za Ligi Kuu na mbili za kimataifa ndani ya muda mfupi.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewataka Waamini kuuishi Ukristo wao, huku wakilishika Neno la Mungu.
Kardinali aliyasema hayo hivi kalibuni wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti Takatifu ya Kipaimara kwa Vijana 112 katika Parokia Teule ya Mtakatifu Stephano wa Hungaria – Makurunge, jimboni humo.
“Sakramenti hii ya Kipaimara ni muhimu sana kwa Mkristo kuipokea, kwa sababu inakupatia uwezo mkubwa wa kumtangaza Kristo mahali,popote pale bila hofu. Pia, inakupatia nguzo kubwa ya kuwa askari hodari wa imani ya Kristo,” alisema Kardinali.
Alisema pia kuwa Waamini wengi hawasikilizi sauti ya Kristo, na hawafuati maneno yake, akiwasisitiza kuepuka kupotoshwa kwa maneno ya uongo, bali wafahamu kwamba sauti ya Mungu ndiyo inatakiwa kufuatwa.
“Sijui wamepotoshwa na kitu gani kibaya, bali utakuta wanafuata sauti za watu waongo ambao hawawezi kuwafikisha safari ya kuelekea kwa Baba Mungu. Ndugu zangu Waamini, nawaomba sana fuateni sauti ya Kristo, ambayo itawasaidia katika safari yenu ya kumtangaza Yesu Kristo ili baadaye muwe watu wema machoni mwake.
“Pia, tutambue kwamba Mungu ametuambia tusikilize sauti ya mwanaye. Huyu ndiye mwanangu niliyependezwa, naye msikieni, Mungu alikuwa na maana kubwa sana kutamka maneno haya. Tuwe watu wa kupendana, kuheshimiana, na kusaidiana kila wakati,” alisema Kardinali.
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Watakatifu Wote – Kiluvya, Padri Danipaso Bitegeko, ambaye pia ni Msimamizi wa Parokia hiyo Teule, alimshukuru Kardinali Pengo kwa kufika parokiani hapo, na kuwapatia Vijana Sakramenti hiyo ya Kipaimara.
Naye, Mwenyekiti wa Parokia Teule, Gabriel Mwalo alisema kuwa kwa sasa wapo katika ujenzi wa nyumba mpya ya Mapadri, ili Padri aweze kukaa hapo hapo, kwani kwa sasa Waamini wanazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa, hivyo wanahitaji huduma ya kiroho kwa karibu.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ametoa wito kwa Vijana wanaopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara, kumweka Mungu maanani siku zote za maisha yao.
Kardinali aliyasema hayo wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu iliyoambatana na Sakramenti hiyo katika Parokia ya Mtakatifu Yakobo Mkuu Mtume – Kijitonyama, jimboni humo.
“Wanakipaimara tambueni kwamba katika maisha yenu ni lazima mumuweke Mungu Mwenyezi maanani. Na ndilo Neno lililotukusanya leo hapa, mlipotualika tuje kuadhimisha, kushuhudia adhimisho lenu la Sakramenti ya Kipaimara, ni ninyi mmetualika. Huwa hamumwoni Askofu anakuja hapa kanisani, lakini ni kwa sababu yenu ninyi mnaopokea Sakramenti ya Kipaimara, mimi niko hapa…
“… na hawa wote waliopo hadi Wanakwaya, huwa wanakuwepo sawa, lakini kwa leo ni kwa sababu yenu kuonyesha kwamba tunaweka maanani tendo mnalolifanya siku hii ya leo. Ni tendo kubwa lenye manufaa, siyo kwenu tu, ni tendo kubwa ambalo mnalifanya kwa niaba ya Kanisa zima. Kwa hiyo tunawaombea kwa Mungu Mwenyezi atekeleze maombi yanayokuwa ndani ya moyo wa kila mmoja wenu,” alisema Kardinali Pengo.
Aliongeza kwamba hakuna mwanadamu anayeweza kufanya kitu na kufanikiwa bila kumtanguliza Mungu, akisisitiza kuwa kila mmoja ahakikishe anamtanguliza Mungu katika mipango yake.
Sambamba na hayo, Kardinali alitoa mfano wa watu waliotaka kujenga mnara mrefu ili wakamwone Mungu mbinguni, na kwamba Mungu hakuona wivu juu ya maamuzi hayo, bali lengo ni kuwaonyesha kuwa hakuna kitu kinachofanywa na mwanadamu bila kumweka Mungu maanani.
“Waliotaka kujenga mnara ili uwe kumbukumbu yao hata kama hawapo, Mungu Mwenyezi alipogundua kwamba hawa watu wanataka kujenga kitu cha namna hii, akaamua kuwachanganya kwa lugha, hawakuweza kuelewana tena; mmoja akitumwa na mwenzake lete jiwe, yeye analeta maji; naomba mchanga, yeye analeta maji, kwa hiyo hawakuweza kuendelea kwa sababu hawaelewani tena…
“Si kwamba Mungu Mwenyezi aliwaonea wivu kwamba watafanya kitu kikubwa hivyo, lakini Mwenyezi alitaka kumwonyesha mwanadamu kwamba ‘ukitaka kufanya kitu chochote bila kuniweka mimi Mungu maanani, haiwezekani, hutafanikiwa,” alisema Kardinali Pengo.
Vile vile, alitoa wito kwa Vijana waliopokea Sakramenti Takatifu ya Kipaimara katika Adhimisho hilo, pengine wana mipango mikubwa iliyopo katika maisha yao, bali watambue kwamba hawataweza kufanikiwa bila kumweka Mungu mbele.
Aliwasisitiza kufahamu kuwa hakuna anayeweza kuwazuia kupanga mipango, hasa ya kimaendeleo maishani mwao, bali wakumbuke kwamba bila kumweka Mungu maanani, hakuna kitakachofanikiwa.
Wakati huo huo, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliwakumbusha Vijana hao kuendelea kuishi maisha yanayompendeza Mungu, kwani hayo ndiyo yatakayowasaidia kupokea baraka katika kila wanaloliomba kwake.