Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Wakili wa Kujitegemea Dk. Aloys Rugazia amesema eneo la jinai la kubambikiwa kesi ni eneo linalosumbua watu wengi katika jamii.
Amesema kuwa Wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba hiyo ni changamoto wanayokutana nayo katika maisha yao.
Dk Rugazia (pichani) alisema hayo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kibasila jijini Dar es Salaam wakati wa maandalizi ya kutoa elimu ya sheria bure na kuandaa nyaraka katika kuadhimisha wiki ya sheria kwa lengo la kuwafikia wananchi ambao hawana fedha za kupata huduma za sheria.
“Tunapokutana na wananchi wanatueleza changamoto nyingi katika eneo la jinai kwamba kuna kubambikiwa kesi kuna kuonewa ndiyo maana tunawataka waje hapa tuwape elimu ya kutosha wajue haki zao ni zipi na watakiwa kufanya nini,” alisema Dk. Rugazia
Aidha, alisema changamoto nyingine ambayo wananchi wanapata ni eneo la ardhi na mirathi wajane, wazee na watoto yatima wanapata shida kupata haki zao za msingi kwa wakati.
“Ardhi ni maisha ni moja kati ya mali muhimu katika mustakabali wa watu mara nyingi ardhi imekuwa ikileta msuguano waliyonacho na wasio nacho, mara nyingi wanajikuta katika hali ngumu ndiyo maana kwa wiki hii tunatoa msaada bure watu waje,” alisema Dk. Rugazia.
Aliongeza kwamba wapo kwenye wiki ya sheria ambayo ilizinduliwa Januari 25, 2025 kwa kawaida wanaadhimisha kwa kujaribu kuifikia jamii kuhakikisha inapata haki kwa sababu sio kila mtu anauwezo wa kulipia gharama za kupata huduma za kisheria.
Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alianzisha mpango maalumu wa kusaidia wananchi wa Mama Samia Legal Aid, mkakati wa kutoa msaada wa kisheria kwa watu wanaishi kwenye jamii wenye kiu ya kudai haki ambao hawawezi kuipata.

Kisarawe

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Viwanda Dk. Selemani Jaffo ameiagiza Mamlaka ya Maji Vijijini (Ruwasa) kuchimba Kisima kirefu Kata ya Bwama iliyopo Wilayani Kisarawe, Mkoani Pwani.
Dk. Jaffo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kisarawe alitoa agizo hilo alipofika Bwama kwenye kuzindua Zahanati ya Bwama iliyogharimu Shilingi milioni 77/- hadi kukamilika kwake tangu ujenzi ulipoanza mwaka 2010.

DAR ES SALAAM

Na Salehe Said

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (United Nations: UN), Amina Mohamed ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa mkakati wa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia na utafutaji madini nchini.
Amina alitoa pongezi hizo hivi karibuni wakati wa mkutano wa pembeni wa Mkutano wa Nishati, alipokutana na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waandishi wa Habari wametakiwa kutumia vyema kalamu zao kuandika habari zenye ukweli, na si zenye kuwachafua wengine, kwani wana jukumu la kueneza ujumbe wa matumaini, upendo na amani.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Joseph Massenge, katika homilia yake wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa Wanamawasiliano wa Jimbo hilo, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Bikira Maria, Mama wa Fatima, Msimbazi.
“Wanahabari tumieni vyema kalamu zenu kuandika habari zenye ukweli, epukeni kuandika habari zenye kuwachafua wengine. Mnatakiwa kueneza ujumbe wa matumaini, upendo na amani,” alisema Padri Massenge.
Padri Massenge ambaye pia ni Mkurugenzi wa Tumaini Media, na Paroko wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu - Makongo Juu, alitoa wito huo kwa wanahabari kuhakikisha Injili inafika kwa kila kiumbe.
Ageukia utunzaji mazingira:
Aliwasihi kupitia kazi zao wanahabari hao wahamasishe pia kuhusu  utunzaji wa mazingira, kwani kwa kutunza mazingira, watakuwa wamepeleka Injili kwa kila kiumbe.
“Hakikisheni Injili inafika kwa kila kiumbe, siyo kwa kila binadamu tu, ni kwa kila kiumbe. Kupitia kazi zenu hizo, nendeni mkahamasishe pia kuhusu utunzaji wa mazingira…Tunzeni mazingira ili yawatunze, mkifanya hivyo mtakuwa mmetangaza habari njema kwa kila kiumbe,” alisema Padri Massenge.
Aidha, aliwasisitizia wanahabari hao kuepuka kuwa waandishi wenye kuandika habari zenye maslahi ya papo kwa papo, bali wafanye kazi zao wakizingatia maadili ya uandishi wa habari.
Padri Massenge aliwasihi wanamawasiliano hao kuwaombea waandishi wote waliotangulia mbele za haki kutokana na kazi zao, akiwataka kuendelea kusimamia ukweli katika uwajibikaji wao.
Padri Mujuni awafunda Waandishi:
Kwa upande wake, Padri Audiphace Mujuni, Padri wa Jimbo Katoliki la Bunda, anayechukua masomo yake katika fani ya Uandishi wa Habari katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT), Tawi la Msimbazi, jijini Dar es Salaam, alisema kwamba vyombo vya habari vina haja ya kuchangia kuleta upendo na mshikamano katika jamii.
Aidha, Padri Mujuni aliongeza kuwa waandishi wa habari ni vyombo vya matumaini katika ulimwengu, hivyo ni wajibu wao kufanya kazi kwa kufuata misingi inayowaongoza.
“Waandishi wa habari, tambueni kwamba ninyi ni vyombo vya matumaini katika ulimwengu. Kwa hiyo, ni wajibu wenu kufanya kazi kwa kufuata misingi na taratibu zinazowaongoza. Mnapaswa kuwa watumishi wa kweli, mkifahamu kwamba kila neno linaweza kuleta athari katika jamii,” alisema Padri Mujuni.
Aliwasisitiza wanamawasiliano kufanya kazi zao, huku wakimtanguliza Mungu, wakitambua kwamba uandishi wao usiwe sababu ya kuikosa mbingu.

DAR ES SALAAM

Na Laura Chrispin

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba, amewasihi Watawa kutambua kwamba wito ni zawadi ya thamani kutoka kwa Mungu, hivyo wasifanye mzaha.
Alisema hayo hivi karibuni  wakati wa Adhimisho la Misa Takatifu ya Kupandishwa hadhi ya Utawa kwa Wapostulanti kuwa Wanovisi, iliyofanyika katika Kituo cha Kiroho -Mbagala, jimboni humo.
“Wito ni zawadi ambayo usipoitambua, utaipoteza, na baadaye utajutia, kwani utakuwa umepoteza tunu ya thamani zaidi kwa sababu ya kufuata mikumbo katika jumuiya, kwa kusikiliza maneno ya wengine na kusahau ulichoitiwa na Mungu, kwa sababu ya tamaa ya ulimwengu na uwongo wa watu wa nje,” alisema Askofu Musomba.
Aidha, alisema kuwa kuongoka ni kutoka katika fikra zisizo njema, na kuanza kufikiria mambo yanayofaa na kumpendeza Mungu, kwani hata Mtume Paulo aliyekuwa akiitwa Sauli, alikuwa ni mtu aliyewachukia Wakristo, na aliwatesa.
Na hata wakati mwingine alidiriki kuyabomoa makanisa, na hata alipokuwa njiani akielekea Damaskasi nchini Syria kuwatafuta Wakristo, ajabu alisikia sauti ikimwita ‘Sauli Sauli, mbona unanitesa’ na yeye hakutambua ni nani, na sauti imetokea wapi.
Aliendelea kusema kuwa ile sauti ilimjibu na kumwambia, Mimi ni Yesu; na baada ya kuingia Damaskasi, alibatizwa na kupewa maelekezo ya kulijenga Kanisa na kubadilishwa jina na kuitwa Paulo, badala ya Sauli.
Askofu Musomba aliwasihi Watawa wote kupenda kujitoa zaidi kwa kuwatumikia wengine kwa unyenyekevu mkubwa, bila kujibakiza wala kujali chochote au kusema wanaonewa na wengine au kuteswa, badala yake wanatakiwa kutambua wapo kwa ajili ya kutumwa, kwani waiitwa na wakaitika.
Askofu Musomba alisema umoja na upendo unaweza kuharibika kwa sababu ya udanganyifu na hisia, na kuwasihi kuwakemea Watawa wengine ambao watakuwa wanaenda tofauti na mapenzi ya Mungu, na kuwataka watambue wakifanya hivyo itawafanya waishi vizuri zaidi.
Aliendelea kusema kuwa Mungu hapendi kuona jumuiya yenye magomvi na masimango, wala kuona jumuiya ya watu wenye roho mbaya, badala yake wanatakiwa kutengeneza jumuiya yenye upendo na upatanisho.
Askofu Musomba aliwapongeza Wapostulanti watano kwa kuvuka hatua na kuwa Wanovisi, na kuwataka wawe ni watu wenye unyenyekevu na furaha kama ya wakati ule walipoandika barua ya kuomba kujiunga katika shirika, na kusikia wamekubaliwa ombi lao.
Askofu Musomba alisema kwamba ukiona mwenzako anafanya vibaya, alafu unampongeza na kufurahia ujue hiyo ni tabia mbaya, na kuwaasa wasidanganyike katika safari yao ya Utume bali wazidi kumwomba Mungu ili wazidi kukua kiimani.

DAR ES SALAAM

Na Rosemary Daniel

Imeelezwa kuwa Wakristo wengi wamekuwa na tabia ya kumiliki Bibilia nyingi kama fasheni, pasipo na faida yoyote katika maisha yao hasa kwa kuisoma, kuielewa na kupata ujumbe wa Mungu.
Hayo yalielezwa na Dekano wa Dekania ya Ubungo, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padri Gallen Mvungi wakati akitoa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu aliyoadhimisha katika Parokia ya Maria Mtakatifu, Kimara.
Padre Mvungi ambaye pia ni Paroko wa Parokia ya Utatu Mtakatifu, Changanyikeni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, alisema,
“Kuwa na Bibilia nyingi bila kusoma, siyo tija kama hatujitaabishi na kijibidiisha kuisoma, kuelewa na kupata ujumbe wa Mungu. Unakuta Mkristo ana Bibilia nyumbani, kwenye gari, kwenye mkoba na hata ofisini kwake, ila imekaa kama pambo tu bila kusomwa.”
Padri Mvungi (pichani) alisema kuwa Wakristo wengi hawampatii Mungu nafasi ya kwanza katika maisha yao, bali wanamweka Mungu kama pambo la kuthibitisha kile wanachokifikiri.
“Pale tunaposoma na kuyaelewa Maandiko Matakatifu, huwa yanapenya ndani kabisa na kuichoma mioyo yetu na kuinua Imani yetu, ndipo tunapopokea majibu ya maombi yetu, njia zetu za kiimani zinafunguka na kuleta amani na uzima tele,”alisema Padri Mvungi.
Alisema kuwa Maadiko Matakatifu pia yanafundisha, kuonya, kurekebisha na kuasa wanadamu waliokengeuka kwa namna ya kipekee kulingana na karama na vipawa vyao, na jinsi walivyoguswa na maandiko hayo.
“Ndani ya Maandiko Matakatifu, jumbe tofauti ambazo zinamgusa Mkristo mmoja mmoja kulingana na kipawa na karama yake kwa jinsi Mungu alivyomjalia, kama vile kila kiungo kilivyo na kazi yake katika mwili wa binadamu,”aliongeza kusema Padri Mvungi.
Alisema kwamba endapo Wakristo hao watakapoyaelewa na kuyashika Maandiko Matakatifu ya Mungu,hakika hawawezi kudanganyika, na wala Ulimwengu hautawahadaa kwa kutafuta mambo ya kidunia, kukimbilia makanisa mengine kutafuta miujiza.

DAR ES SALAAM

Na Mathayo Kijazi

Waamini wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeey – Tegeta ‘A’, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wameadhimisha siku ya Somo wa Parokia hiyo, huku wakitakiwa kupendana katika kila hali walizo nazo, kwani hakuna aliyeumbwa kuwa mtumwa kwa wengine.
Hayo yalisemwa na Padri Prosper Kessy, Gombera wa Kituo cha Hija cha Mtakatifu Padri Pio, San Damiano – Msimbazi, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Somo wa Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeey – Tegeta ‘A’, jimboni humo.
“Kwa hiyo ndugu, tupendane katika hali zozote tulizo nazo, kwa sababu hakuna aliyeumbwa kwa ajili ya kuwa mtumwa kwa watu wengine, yaani hata ukijiona una pesa kiasi kwamba ukaamua kutafuta wafanyakazi wa nyumbani kwako, lakini tambua kwamba wale hawakuumbwa kwa ajili ya kuja kuwa watumwa wako,” alisema Padri Kessy.
Aidha, Padri huyo aliwasihi Waamini kufahamu kwamba Neno la Mungu ni tofauti na maneno mengine, kwani Neno hilo huwabadilisha hata majambazi na kuamua kuishi maisha yanayofaa katika jamii.
Padri huyo aliwasisitiza Wakristu kuliruhusu Neno la Mungu lifanye kazi katika maisha yao ili liwabadilishe, na kuwa watu wema.
Alitoa wito kwa Waamini kuliruhusu Neno hilo lifanye kazi katika biashara zao, akiwataka kuepuka udanganyifu katika biashara hizo, ikiwemo kujipangia viwango vya bei za bidhaa, tofauti na bei halali za bidhaa hizo.
“Liruhusuni Neno la Mungu liingie katika biashara zenu, ili liwasaidie kuwa waaminifu. Wapo wafanyabiashara ambao ukifika wanakudanganya kwamba ‘nguo hii imetokea Uturuki,’ ili akuuzie kwa bei ya juu zaidi, huku ukiamini kwamba kwa sababu imetoka Uturuki, basi itakuwa ni nzuri na imara zaidi…
“Yaani mtu anaamua kuuza bidhaa kwa bei mara tatu zaidi ya aliyonunulia, huo ni udanganyifu wa juu sana katika biashara. Halafu baadaye anatoka mbele za watu anasema, ‘Mungu amenitendea mambo makuu sana katika biashara yangu,’ huyo aliyekutendea siyo Mungu, bali ni shetani kupitia udanganyifu wako,” alisema Padri Kessy.
Padri Kessy alitoa wito kwa wazazi kuwapa watoto wao malezi yaliyo bora, na si ya kuwanyenyekea, kwani wakiwadekeza kupitiliza, watawatengenezea mazingira magumu pale watakapokuwa wakubwa.
Aidha, aliwashukuru Waamini wa Tegeta ‘A’ kwa kumwalika kusali naye katika Adhimisho hilo la Misa Takatifu ya Somo wa Parokia, akiwaasa kuendelea kushikamana na kuwa wamoja ili waweze kupiga hatua kimaendeleo parokiani hapo.
Kwa upande wake Paroko wa Parokia hiyo, Padri Urbanus Riziki alimshukuru Padri Kessy kwa kukubali mwaliko wa kwenda kuungana na Waamini wa Tegeta ‘A’, akimshukuru pia kwa kuongoza Misa hiyo Takatifu.
Padri Riziki aliwaasa Waamini parokiani hapo kuongeza nguvu katika kuchangia ujenzi wa kanisa jipya linaloendelea kujengwa, ili waweze kuukamilisha kwa haraka ujenzi huo.
Kwa mujibu wa Katibu wa Parokia hiyo, Prisila Clemence, Parokia ya Mtakatifu Yohane Maria Muzeey - Tegeta ‘A’ ilianzishwa kama Kigango cha Mtakatifu Yohane Maria Muzeey, Julai 6 mwaka 2007.
Kigango hicho kilianzishwa kutoka Parokia ya Bikira Maria Mama wa Huruma - Mbezi Beach (BMMH) iliyokuwa chini ya Paroko wa Mbezi Beach wa wakati huo, Padri Romuald Mukandara.
Baadaye Kigango hicho kilihamishiwa Parokia ya Bikira Maria Consolatha – Makabe, chini ya Mapadri wa Missionaries of Mary Immaculate (MMI), baadaye tena kikahamishwa na kuwa chini ya Parokia ya Benedicta wa Msalaba – Msumi.
Julai 7 mwaka 2018, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kwa wakati huo,  alikipandisha hadhi kuwa  Parokia Teule.
Julai 7 mwaka 2020, Mtakatifu Yohane Maria Muzeey - Tegeta ‘A’  ilitangazwa rasmi kuwa Parokia Kamili na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, na kuwekwa chini ya Mapadri wa Jimbo hilo, ambapo Padri Urbanus Riziki Ngowi alitangazwa kuwa Paroko wa Parokia hiyo.

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi wetu

Baba Mtakatifu Fransisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka shughuli za kichungaji za Jimbo Katoliki la Iringa, lililowasilishwa na Askofu wa Jimbo  hilo, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, akimteua Padri Romanus Elamu Mihali kuwa Askofu mpya wa jimbo hilo.
Askofu Mteule Mihali ameteuliwa baada ya Askofu Ngalalekumtwa aliyekuwa akiongoza jimbo hilo, kufikisha umri wa kustaafu.
Kabla ya uteuzi huo, Askofu mteule Mihali alikuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga, na Paroko wa Parokia ya Ujewa, jimboni humo.
Askofu Mteule Mihali alizaliwa Juni 10, mwaka 1969 katika Kijiji cha  Itulituli, Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa.
Baada ya majiundo yake ya Falasafa na Taalimungu katika Seminari Kuu ya Songea, alipewa Daraja  Takatifu la  Upadri Julai 13 mwaka 2000 kwa ajili ya Jimbo la Iringa.
Askofu Mteule Mihali katika utume wake, alishika nyadhifa mbalimbali na kuendelea na masomo zaidi, ambapo mwaka 2000 hadi 2003, alikuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Paulo Mtume huko Ilula, jimboni Iringa.
Mwaka 2003 hadi mwaka 2005 alikuwa Mlezi na Mkufunzi wa Seminari Ndogo ya Mtakatifu Kizito, Jimbo Katoliki la Mafinga.
Aidha, mwaka 2005, hadi 2011, aliendelea na masomo yake ya Uzamili wa Sayansi katika Sayansi ya fani ya wanyama, na kupata  Shahada yake  katika Chuo Kikuu cha Kerala nchini India.
Mwaka 2012 hadi 2015 alifanya utume kama Paroko Msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria wa Fatima huko Usomaki, jimboni Iringa.
Mwaka 2015 hadi 2024, alikuwa akifanya utume kama Paroko wa Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa, Ujewa,  Iringa.
Baada ya kuundwa kwa Jimbo Katoliki la Mafinga  mwaka  2024, na  kupatikana Askofu mpya wa Jimbo hilo, Padri Romanus aliteuliwa kuwa Makamu Askofu wa Jimbo hilo, na Paroko wa Parokia ya  Bikira Maria Mpalizwa (Mafinga), hadi uteuzi wake.
Askofu Mstaafu Tarcisius Ngalalekumtwa ataendelea kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Iringa hadi Askofu   Mteule Mihali atakapowekwa wakfu wa Kiaskofu kwa ajili ya Jimbo hilo hilo.

DAR ES SALAAM

Na Celina Matuja

Madaktari na Wauguzi Wakatoliki nchini wametakiwa kuzingatia mambo muhimu ili waweze kutoa huduma kadri ya mwelekeo wa Bwana Yesu Kristo.
Madaktari na wauguzi hao wameaswa pia kutumia muda wao kusali ili  kuomba mwongozo wa Mungu katika huduma zao kwa wagonjwa.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katopliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu ametoa maagizo hayo katika salamu kwenye Semina ya Madaktari na Wauguzi Wakatoliki, iliyoandaliwa na Jimbo hilo, iliyofanyika katika Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata.
Semina hiyo ilikwenda sanjari na Adhimisho la Misa Takatifu, ambapo katika homilia yake aliwataka madaktari hao, kufuata mfano wa Mtakatifu Paulo aliyewaua na kuwatesa Wakristo, lakini aliongoka, hivyo wao nao wahakikishe wanaleta uponyaji kwa wagonjwa  na kuihubiri Injili.
“Kutokana na Ufunuo wa Kristo mwenyewe, Mtakatrifu Paulo alifanya kazi kubwa na nyingi kufundisha habari njema za Yesu Kristo, baada ya kuongoka. Sisi pia tuongoke kama Paulo, hivyo nawapatia ‘take home’ ili mpate kuzingatia katika kazi yenu,” alisema Askofu Mchamungu.
Askofu awapa Madaktari ‘vitendea kazi’:
Moja ya mambo ambayo walitakiwa kuzingatia wanataaluma hao ni kusali na kuomba maongozi ya Mungu, kwa sababu kazi yao inagusa moja kwa moja uumbaji na uhai.
Kuwahi kazini na kuwajibika kwa wagonjwa kwa moyo wa upendo na furaha, kuwasikiliza wagonjwa kwa umakini ili kuelewa shida zao kiafya ili kutoa matibabu sahihi.
Kuepuka uzembe kazini na kuwa makini, kwa kufanya kazi kwa kujiamini ili kumpa mgonjwa tumaini la kupona ama kupata ahueni, kupenda kazi na kuitenda kwa furaha kwa kuwa ni wito wao.
Kutoa huduma bila kudai chochote kwa mgonjwa, na kutumia lugha nzuri, ikiwemo kutunza siri za mgonjwa.
Kutokuwa na mahusiano ya kimapenzi na wagonjwa wao,  kuwahudumia kwa karibu wagonjwa wanaohitaji uangalizi makini, kama wanaoongezewa damu, maji mwilini, na hasa nyakati za usiku.
Aidha, Askofu Mchamungu aliwataka kusoma na kujiendeleza zaidi ili kuwa na ujuzi mkubwa kwa kusoma vitabu mbalimbili vinavyohusu taaluma yao.
Padri Mosha: Fanyeni kazi bila kinyongo:
Kwa upande wake, Padri Dakta Joseph Mosha, Paroko wa Parokia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alikemea baadhi ya tabia za Wauguzi na Madaktari kutotoa huduma kwa moyo na ari kwa wagonjwa.
Aliwataka kutambua kwamba wao ni washirikishwa wa kazi ya utendaji wa Mwanadamu kutoka kwa Mungu, na kutokuondoa nafasi ya Mungu katika maisha ya Mwanadamu.
Padri Mosha alisema kuwa Maandiko, kitabu cha mwanzo 1:26 akinaeleza kwamba “Sisi Binadamu tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu,”, akiwataka Wanataaluma hao kutambua kwamba kila wanapomwona mgonjwa, watambue kuwa ni sura na mfano wa Mungu.
Alisema kwamba maisha huanza kwenye familia, hivyo hawana budi kutenda kwa misingi ya Mwenyezi Mungu pasipo kufuata ile siasa ya uhuru wa kufanya lolote, ambao una upotofu.
Padri Kessy: Tendeni kazi kwa upendo:
Naye Padri Prosper Kessy Gombera wa Kituo cha Hija cha San Damiano Msimbazi, aliwakumbusha  Madaktari na Wauguzi hao, kutenda kazi zao kuzingatia huruma na upendo.
Aidha, aliongeza kuwa itamsaidia sana mgonjwa iwapo atapokea huruma na upendo, bila kusahau kumhudumia kwa hadhi njema, na hisia ya utu.
Kwamba kuna baadhi ya watu wamepoteza hisia, wanaona kila jambo ni sawa, wamezoea kifo, hata wakimwona mgonjwa yu mahututi wanaona kama ni mfu, wasikubali iwatawale, kwani Mungu amempa kila mtu hisia na huruma.
Jambo lingine la kuzingatia ni kuigeuza kazi kuwa sala,kwa maana ya kusali kabla ya kuwahudumia wagonjwa na kuifanya kazi hiyo kwa  umakini, ndipo inapogeuka kuwa injili na sala.
Aliwataka pia kuvumilia kutokana na matukano mbali mbali, ila kusimama na msimamo wa kuutafuta utakatifu na uaminifu kwa kuheshimu uhai mwanzo mpaka mwisho, kwa kukemea maovu mamlaka waliyopewa wasikubali kushiriki katika  dhambi.
Akinukuu Maandiko Matakatifu Matayo 28:16 – 20: Nimepewa mamlaka yote Duniani na Mbinguni enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.

VATICAN CITY, Vatican

Baba Mtakatifu Fransisko amekutana na Maaskofu, Marais wa Tume za Mawasiliano za Mabaraza ya Maaskofu na Wakurugenzi wa Ofisi za Mawasiliano za Mabaraza ya Maaskofu.
Katika hotuba yake Baba Mtakatifu aliwashukuru kwa kushiriki nao, akiwakaribisha wote ambao katika Makanisa mahalia wanafanya huduma ya kuwajibika katika nyanja ya mawasiliano.
“Inapendeza kuwaona hapa, Maaskofu, Mapadri, Watawa wa kike na kiume na walei, walioitwa kuwasilisha maisha ya Kanisa na mtazamo wa Kikristo wa ulimwengu. Kuwasiliana na maono haya ya Kikristo ni kuzuri,” alisema Papa Fransisko.
Aidha, Papa aliongeza kwa kusema, “Tunakutana leo, baada ya kuadhimisha Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano, kufanya mapitio na pia uchunguzi wa dhamiri pamoja. Hebu tutulie ili kutafakari zaidi juu ya njia halisi tunayowasiliana nayo, inayohuishwa na imani ambayo, kama ilivyoandikwa katika Waraka kwa Waebrania, ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyoonekana…
Baba Mtakatifu Fransisko alifafanua kuwa hiyo ambayo kwao ni huduma ya kitaasisi, pia ni wito wa kila Mkristo, wa kila mtu aliyebatizwa, na kwamba kila Mkristo anaitwa kuona na kusimulia historia za mema ambayo uandishi wa habari mbaya hujaribu kufuta, na kutoa nafasi ya uovu tu.
Alibainisha pia kwamba uovu upo, hivyo haupaswi kufichwa, lakini lazima ukoroge, uzae maswali na majibu, na kusema kwamba kwa sababu hiyo,  kazi yao ni kubwa na inawahitaji wajitoe wenyewe kufanya kazi ya pamoja ili ya kuwashirikisha kila mtu, kuwathamini wazee, vijana, wanawake na wanaume kwa kila lugha, kwa maneno, sanaa, muziki, uchoraji, na picha.
Aliwataka Waamini kufahamu kwamba wote wameitwa ili kuthibitisha jinsi gani wanawasiliana naye, hivyo wanahitaji kuwasiliana kwa kila linalotokea.
Alisisitiza kuwa changamoto ni kubwa, huku akihimiza kuimarisha harambee kati yao, katika ngazi ya bara na ya ulimwengu mzima ili kujenga mtindo tofauti wa mawasiliano, tofauti katika roho, katika ubunifu, katika nguvu ya kishairi inayotoka katika Injili na isiyokwisha.
Aidha, Baba Mtakatifu alikiri jambo moja kwao kuwa anajali zaidi akili ya asili kuliko akili mnemba, akisema kuwa akili ya asili ndiyo ambayo wanapaswa tuikuze, na kwamba wanapohisi kuwa wameanguka kwenye shimo, watazame zaidi ndani yao wenyewe.