UZINDUZI MWEZI MOYO MTAKATIFU WA YESU
Maasi yaibua mjadala
- Askofu: Dunia ingekuwa basi, abiria wote wangeshuka
DAR ES SALAAM
Na Mathayo Kijazi
Imeelezwa kuwa Dunia ingekuwa ni basi ama daladala, abiria wote wangeshuka na kuondoka zao, hasa kutokana na maasi yaliyokithiri, ikiwemo vitendo vya ushoga na usagaji vinavyozidi kushamiri nchini na dunia kwa ujumla.
Aidha waamini wamatakiwa kuchangia na kuitegemeza Tumaini Media, kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwekeza mbinguni, kwani kazi kubwa ya chombo hicho ni uinjilishaji.
Hayo yalisemwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu wakati wa homilia yake katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Uzinduzi wa Kampeni ya Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa mwaka 2024, iliyoadhimishwa katika Parokia ya Kristo Mfalme – Tabata, jimbioni humo.
“Kwa maasi haya ya sasa, dunia ingekuwa ni basi, abiria wote wangeshuka na kuondoka zao,”alisema Askofu Mchamungu.
Aidha, Askofu Mchamungu, aliwakumbusha Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu kuiga mfano wa Yesu Kristo juu ya kuwapenda na kuwasaidia wengine, kwani Kristo alikubali kutoa uhai wake kwa ajili ya wanadamu.
“Alitupenda mpaka kufa msalabani. Na sisi tunajua waziwazi kwamba moyo unaashiria upendo, lakini pia moyo unaashiria huruma. Kristo alitupenda upendo usiokuwa na mwisho. Kwa hiyo, na sisi Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu tunapaswa kumuiga Kristo ambaye alitupenda mpaka kumwaga damu yake.
“Pengine si rahisi kufikia kile kiwango chake kwamba tuko tayari kutoa uhai wetu kwa ajili ya wengine. Mbona hata katika familia wakati mwingine mwanandoa mmoja anaweza akamuacha mwenzake, kisa ‘ame-paralyse’, kwa sababu ameshaona kwamba mwenzake hajiwezi tena, hivyo anaona atapata shida sana. Kwa hiyo pamoja na hayo, tutambue kwamba tunapaswa kupendana,” alisema Askofu Mchamungu.
Wakati huo huo, Askofu huyo aliwataka Wanamoyo kuongeza nguvu katika kusal ili maovu yapungue, kwani baadhi ya mambo yanayoendelea ulimwunguni, si ya kuridhisha.
Aliwapongeza pia kwa jinsi wanavyojitahidi katika masuala ya imani, huku akiwasihi kuongeza jitihada hizo ili zionekane katika matendo juu ya kuichukia dhambi.
Askofu alibainisha kuwa miongoni mwa mambo makubwa wanayotakiwa kuyazingatia Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu, ni pamoja na kuichukia dhambi, kwani haipendezi kumuona mwanachama huyo kushabikia dhambi katika maisha yake.
Aliwaonya pia kuepuka kufanya vitendo vya mauaji, wala kuhusika katika tukio lolote la kuangamiza uhai wa mtu mwingine, kama vile kibaka, kwani lengo la chama hicho ni kuiga upendo na huruma ya Mungu katika maisha yao.
“Ikitokea, kwa mfano, kuna kibaka huko ameiba akakamatwa, watu wakaanza kumzunguka wanataka kumuadhibu kwa kumchoma moto, itakuwa ni kitu cha kushangaza sana kuona kwamba kati ya hao wanaotaka kufanya kitendo hicho, yupo mtu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, kitakuwa kitu cha ajabu sana, yaani haiingii akilini…
“Katika tukio hilo, unamkuta mtu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu ndiye anaenda kutafuta kibiriti au mafuta ya taa kwa ajili ya kumchoma kibaka, hiyo haiji kabisa, haviendani na vile Kristo alivyotutaka, na kwamba mtu anajiunga kwenye Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu, ili kuiga ule upendo na huruma ya Mungu,” alisema Askofu Mchamungu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Padri Chesco Msaga, ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Tumaini Media, aliwaomba Waamini kuendelea kuvichangia vyombo hivyo, kwani kwa kufanya hivyo, watakuwa wameshiriki katika kazi ya uinjilishaji.
Naye Mkurugenzi wa Tumaini Media, Padri Joseph Massenge alimshukuru Askofu Mkuu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi kwa kukubali mwezi Juni uwe ni maalumu kwa ajili ya kukichangia chombo hicho, ili kiendelee vyema katika kazi yake ya uinjilishaji.
Padri Massenge aliwashukuru Maaskofu Wasaidizi wa Jimbo hilo, Mhashamu Henry Mchamungu na Mhashamu Stephano Musomba kwa kuendelea kuhamasisha pamoja na kuvilea vyombo hivyo vya Tumaini Media, vinavyohusisha televishen, radio, pamoja na gazeti.
Sambamba na hayo, Mkurugenzi huyo alimshukuru Askofu Mchamungu kwa kuadhimisha Misa hiyo Takatifu, huku akiwashukuru pia Mapadri wenzake wote walioungana naye kwa ajili ya Adhimisho hilo.
Padri Cornelius Mashare, Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme - Tabata, alikipongeza chombo hicho kwa kazi yake kubwa ya uijilishaji, huku akiwaomba Waamini kuendelea kukiwezesha, kukitangaza, pamoja na kukisaidia chombo hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Masoko wa Tumaini Media, Arnord Kimanganu Mtui aliwashukuru Waamini kwa majitoleo yao, huku akisema kuwa kutokana na mwitikio mkubwa ambao ulionekana mwaka jana 2023, mwaka huu wameanza vyema kwa kujiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha Shilingi milioni 550, wakiwa na imani kwamba kama zitafanyika juhudi kama za mwaka jana, watafikia malengo hayo.
Kimanganu aliongeza kuwa mpaka sasa tayari gharama za upanuzi wa masafa kwenda Mahenge Shilingi milioni 30 zimeshafanyika, hivyo kinachosubiriwa kwa sasa ni kwenda tu kuwasha mitambo hiyo, na kuongeza kuwa sababu iliyochelewesha ni kutokana na ubovu wa miundombini ya barabara ya kwenda Mahenge.
Naye Mhandisi John Ndazi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam alisema kuwa Tumaini Media ni chombo cha wote, hivyo ni wajibu wao kujitolea kukichangia chombo hicho.
Akizungumza katika Adhimisho hilo, Mwenyekiti wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Godon Rwenyagira, alimwahidi Mkurugenzi pamoja na wafanyakazi wa Tumaini Media kuwa wao kama Wanamoyo, wamejipanga kuhakikisha kwamba bahasha zote zilizotolewa kwa ajili ya michango hiyo, zitarudishwa kama ilivyokusudiwa, kwani wamelibeba jukumu hilo kwa upendo mkubwa.