Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *
Captcha *
Reload Captcha

MOROGORO

Na Angela Kibwana

Katika nyumba moja huko Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, Lucy Patrick (siyo jina lake halisi), mfanyakazi wa majumbani, anajikuta akifanya kazi kwa saa 18 kila siku, bila kupumzika.
Hajawahi kulipwa mshahara wake wa miezi mitatu, sasa, ambapo malengo yake ya awali ilikuwa ni kujiongezea kipato kusaidia familia yake na mara nyingi anakula mabaki ya chakula cha familia.
Kwa muda mrefu, sauti yake haikusikika, lakini sasa, juhudi za Chama cha Wafanyakazi Wakatoliki (CWW) zimeanza kuleta matumaini kwake baada ya kutoa mafunzo ya kuboresha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi.”
Wafanyakazi wa majumbani wanakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo kutolipwa mishahara inayoendana na kazi zao, kunyimwa chakula, kupigwa, na kudhulumiwa haki zao za msingi.
Aidha, wengi wao hawana mikataba ya ajira, jambo linalowafanya kukosa ulinzi wa kisheria, hivyo wanajikuta wakifanya kazi kwa mazingira magumu bila msaada wowote wa kisheria au kijamii.
Victor Mackyao, mwanasheria na mwezeshaji wa mafunzo yaliyoandaliwa na (Chama cha Wafanyakazi Majumbani: CWM), anasema kuwa wafanyakazi wa majumbani, mara nyingi hawajui sheria za ajira, wala haki zao za msingi.
Wafanyakazi wa majumbani wengi wao ukiwauliza wanasema wanakumbana na vipigo, wananyanyapaliwa, wanatengwa,wanateswa maeneo wanayoishi siyo rafiki, wanakosa fursa ya matibabu wanapougua, wengine kukosa chombo maalum cha kuwasemea” alisema Mackyao.
Alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwaelimisha wafanyakazi hao wa majumbani ili kujua nini maana ya haki, lakini pia waajiri watambue wajibu wao ni upi kwa wafanyakazi hao ili kujenga usawa katika makundi yote mawili.
Alifafanua kuwa moja ya changamoto zinazochangia wafanyakazi hao wa majumbani kukosa hali zao msingi ni kutokana na vyombo au mamlaka mbalimbali ambazo zina dhamana ya kuwasimamia haki zao, kutowafikia kwa wakati kwa sababu wafanyakazi hao wanatoka kwa waajiri tofauti na maeneo tofauti.
Alisema kuwa tangu Cwm ilipoanza kutoa mafunzo hayo wamebaini kwamba baadhi ya wafanyakazi wa majumbani wanapohojiwa, ambao wanakaa kwao nje ya mwajiri wake, baada ya kuulizwa, wamedai kwamba wanalipwa kiasi cha shilingi elfu 30 au 50, wakati sheria inamtaka alipwe kuanzia 120,000/=.
“Wafanyakazi ambao wanakaa kwa waajiri wao sheria inawataka walipwe shilingi elfu 60, lakini hawalipwi kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo changamoto hizo ndizo zilizotufanya tuweze kupita na kutoa elimu kwa jamii lakini tutoe rai na tuviombe vyombo vyenye mamlaka ya kushughulikia masuala ya wafanyakazi wa majumbani, waweze kutumia mbinu kama tunazotumia sisi, ili waweze kuwafikia kujua changamoto zao na kazitatua wasikae tu mijini.”
Alisema kwamba kazi za majumbani si rahisi, na sheria inakataza ajira ya watoto katika kazi hizi kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, Sura ya 13, Hata hivyo, bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,
Kwa kutambua changamoto hizi, CWM jimbo la Morogoro limeanza kutoa mafunzo kwa waajiri na wafanyakazi wa majumbani katika Dekania ya Kilosa.
Kwa mujibu wa CWM, kati ya wafanyakazi 161 waliopata mafunzo, asilimia 70 hawakuwa wanajua haki zao za msingi, na wala hawajui lolote kuhusu haki yao ya kuwa na mikataba ya kazi, ili kulinda haki zao.
Lengo ni kujenga mahusiano bora kati ya waajiri na wafanyakazi wa majumbani, kwa kuhakikisha haki na wajibu vinazingatiwa pande zote mbili.
Mratibu wa CWM, Edson Yeyeye, alisema kuwa mafunzo haya yalianza mwishoni mwa mwaka 2024 katika Dekania za Kihonda, Morogoro mjini, na sasa yamefikia Kilosa. Tayari wafanyakazi 161 na waajiri 62 wamepatiwa mafunzo hayo, huku Viongozi wa Dini na serikali 27 wakiungwa mkono katika juhudi hizi.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mfanyakazi wa majumbani anapata elimu ya haki zake na waajiri wanajua wajibu wao,” alisema Yeyeye.
Bahati Ramadhani, mmoja wa waajiri walioshiriki mafunzo hayo, alisema, “Ni muhimu elimu hii kufika vijijini kwa sababu huko ndiko wafanyakazi wengi wa majumbani wanatoka, Wengi wanapokuja mjini, wanakosa haki zao kwa sababu hawana mikataba wala hawajui sheria”.
Maria Chalalika, mshiriki mwingine, aliongeza kuwa kunahitajika kuundwa vyombo maalum vya kushughulikia haki za wafanyakazi wa majumbani, hasa kwa wale wanaopelekwa nje ya nchi, bila kujua wanachokwenda kukifanya
Kwa upande wake, Hosea Nikodemas Mgunda, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlimani Boma, aliwapongeza CWM kwa juhudi zao za kutoa elimu hiyo kwa jamii, ili haki za wafanyakazi wa nyumbani ziweze kulindwa na kuthaminiwa.
“Wafanyakazi wa majumbani wanapitia madhila mengi, hivyo tunahitaji kuwa na chama chao maalum ili kuwatetea na kuhakikisha wanapata haki zao.ili kupunguza vitendo vya ukatili miongoni mwao
Hata hivyo, Mgunda aliahidi kutumia mikutano yake ya kijamii kutoa elimu kuhusu haki za wafanyakazi wa majumbani ambavyo anatarajia kufanya kuanzia tarehe mosi Februari mwaka huu 2025.
Mafunzo haya yameongeza uelewa miongoni mwa wafanyakazi na waajiri, ambapo wengi wao sasa wanatambua umuhimu wa mikataba ya ajira, haki ya likizo, na mishahara inayotambulika kisheria.
Hata hivyo, changamoto bado zipo, hasa katika kuwafikia wafanyakazi walioko maeneo ya vijijini, na wale wanaofanyiwa ukatili wa kimya kimya.
Washiriki wa mafunzo hayo walipendekeza kuundwa kwa vyombo maalum vya kushughulikia haki za wafanyakazi wa majumbani, Kuongeza uhamasishaji kuhusu sheria za kazi vijijini na mijini, Kuwapatia wafanyakazi wa majumbani elimu ya malezi na maadili, kwani mara nyingi wao ndio walezi wa karibu wa watoto katika familia nyingi
Mratibu wa CWM, Edson Yeyeye, alisisitiza kuwa jitihada hizi zitaendelea hadi sauti za wafanyakazi wa majumbani zisikike na kuheshimiwa kikamilifu.
 “Ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha haki na heshima kwa kila mfanyakazi wa majumbani, kwani mchango wao katika familia na jamii hauwezi kupuuzwa,” alisema Yeyeye.
Sasa ni wakati wa jamii kushirikiana ili kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi wa majumbani anapata heshima anayostahili, na mahusiano ya kazi yanajengwa kwa misingi ya haki na usawa.
Nashauri wafanyakazi wa majumbani wapewe elimu ya malezi na maadili mara kwa mara, kwa sababu katika nyumba nyingi za mijini na hata vijijini, sauti ya mfanyakazi wa majumbani ndiyo inayopokelewa kwanza asubuhi, ikiongoza familia katika maandalizi ya siku.
Wakati mwingine, wao ndio waangalizi wa karibu wa watoto; wanahakikisha wanakula, wanavaa, na mara nyingi hata wanasaidia katika kujenga maadili ya msingi kwa watoto hao, ikiwa ni pamoja na kuwafundisha kusoma au kuandika. Hata hivyo, mchango huu wa kipekee mara nyingi unapuuzwa, ukifichwa na mwanga wa jukumu lao la kazi za nyumbani.

MELBOURNE, Australia
Alexander Zverev amekerwa na shabiki kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia wakati wa hafla ya kupokea tuzo ya Australian Open.
Mchezaji huyo namba mbili wa Ujerumani, alishindwa kwa seti moja kwa moja kutoka kwa nambari moja duniani, Jannik Sinner huko Melbourne.
Alipopiga hatua kupokea kombe lake la washindi wa pili, shabiki mmoja alipaza sauti: “Australia inaamini katika Olya na Brenda.”
Mchezaji huyo alishitakiwa kwa kumnyanyasa mpenzi wake wa zamani Olya Sharypova mnamo mwaka 2020, na unyanyasaji wa nyumbani mnamo 2023 aliyofanya kwa Brenda Patea, ambaye alizaa nae mtoto mmoja.
Zverev mara kwa mara amekuwa akikanusha kesi zote mbili za madai, na kesi ya mahakama ya Berlin iliyoletwa na Patea ilikomeshwa mwaka jana.
Mnamo Oktoba 2020, mpenzi wa zamani Sharypova, alimshtaki Zverev kwa vurugu na unyanyasaji wa kihemko wakati wa uhusiano wao. Zverev alikanusha madai hayo na kusema, “hayana msingi”.
Sharypova hakufungua mashtaka, na uchunguzi wa miezi 15 wa ATP Tour ya wanaume uligundua kuwa hakuna “ushahidi wa kutosha” kuthibitisha madai yaliyotolewa na Sharypova, na hivyo Zverev hakukabiliwa na hatua za kinidhamu.

LEICESTER, Uingereza
Baraza la majaji limestaafu kuanza mashauri yake katika uchunguzi wa vifo vya watu watano waliofariki katika ajali ya helikopta nje ya Uwanja wa King Power wa Leicester City.
Mwenyekiti wa Foxes, Vichai Srivaddhanaprabha alifariki pamoja na abiria wenzake Kaveporn Punpare, Nusara Suknamai, rubani Eric Swaffer na mshirika wake Izabela Roza Lechowicz, Oktoba 27 mwaka 2018.
Siku ya Jumatatu, mchunguzi wa maiti Catherine Mason, alihutubia baraza la majaji, huku uchunguzi ukiingia wiki ya tatu katika Ukumbi wa Jiji la Leicester.
Prof Mason aliita ajali hiyo “msiba mbaya”, huku akiagiza baraza la mahakama kwamba hitimisho la bahati mbaya tu, lingeweza kufikiwa.
Aliwaambia majaji 11 kwamba watajibu maswali manne. Kila mtu aliyekufa alikuwa nani? Walikufa lini? Walifia wapi? Na, walikujaje na kifo chao?
“Hilo lisijumuishe mambo kama mifumo, taratibu, na tahadhari ambazo zingeweza kusababisha helikopta na kubeba kubuniwa kwa njia tofauti,” aliongeza.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Tenisi ni mchezo unaofurahiwa na washiriki wa rika zote na viwango vyote. Mchezo huo umekuwa ukivutia watazamaji na wachezaji tangu mwanzoni mwa karne ya 12.
Hapa kuna ukweli na maendeleo ya kupendeza ambayo yametokea tangu historia ya mapema ya tenisi.
RAKETI:
Raketi ni kifaa cha kuchezea mchezo wa tenisi, ambacho kazi yake ni kupigia mpira huo.
Kabla ya wachezaji wa tenisi kutumia raketi, watu walianza kutumia kiganja cha mikono yao kupiga mpira na kuurudisha juu ya wavu.
Watu katika karne ya 12 waliteseka kutokana na kuvimba mikono  katika mchezo wa jamii ya tenisi ulioitwa ”jeu de paume” unaomaanisha “mchezo wa mitende.”
Hali hiyo haikuchukua muda mrefu, kwani ilikwenda hadi karne ya 16 ambapo ‘racquets’ zilitumiwa ingawa kabla ya raketi walitumia matawi ya mnazi yaliyosukwa kupigia mpira.
RANGI ZA MIPIRA:
Kabla ya mipira ya tenisi yenye rangi ya njano kuletwa mchezoni, kulikuwa na mipira myeupe.
Mipira myeupe ilitumika tangu mchezo huo unatambulishwa duniani, hadi pale iipoanzishwa michuano ya Wimbledon mnamo mwaka 1986, wakati mipira ya tenisi ya njano ilipotumiwa.
Maafisa waliamini kuwa mpira wa njano ungekuwa rahisi kwa watazamaji kutazama kwenye TV, na hiyo ndiyo ikawa sababu ya kutumia mipira ya rangi hiyo.
MAILI TATU:
Wakati wa mechi ya tenisi, mchezaji kwa wastani hukimbia maili 3.
Kwa sababu ya udogo wa uwanja wa tenisi, hiyo ni maili 3 ngumu zaidi ya mchezaji kwenda mbele na kurudi nyuma mara zote.
MKANGANYIKO WA RAKETI:
Raketi ya tahajia ndiyo njia ya kawaida ya kutamka kifaa kinachotumika katika michezo ya wavu, kama vile tenisi.
Kwa Kiingereza, kuna maneno mawili yanatofautiana kwenye kuandika, lakini yanafanana kimatamshi. Racket na racquet hutofautiana kwenye matumizi, ambapo Racket ni kifaa ambacho hutumika kwa kuchezea tenisi, na Racquet hutumika kuchezea michezo mingine, kama vile skwashi.
Ingawa tovuti nyingi zitakuambia kuwa raketi ni tahajia sahihi, USTA mara kwa mara hutumia raketi ya tahajia.
DADA WA FAMILIA MOJA:
Venus na Serena Williams walikuwa seti ya kwanza ya kina dada kushinda medali za dhahabu za Olimpiki katika historia ya tenisi.
Akina dada hao walishinda medali yao ya kwanza ya dhahabu ya Olimpiki katika Michezo ya Olimpiki ya Sydney mwaka 2000.
Sasa wana medali mbili za ziada za dhahabu kutoka Beijing 2008 na London 2012.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Mtibwa Sugar ya Morogoro imesema kwa ubora inayouonyesha kwenye Ligi ya Chamionship kwa sasa, ni kama vile walitoka Ligi Kuu mara moja na kwenda kutalii, ili kuona hali ya hewa ya huko.
Mtibwa imekuwa ikionyesha kiwango bora tangu msimu wa Championship uanze, Ligi ambayo zamani ilifahamika kama Daraja la Kwanza, ambayo huzipokea timu zinazoshuka daraja kutoka Ligi Kuu.
Mtibwa ambayo ipo kileleni mwa Ligi hiyo, endapo itaendelea kukaza uzi, itafanikiwa kurejea tena Ligi Kuu, ambapo msimu uliopita ilishuka daraja baada ya kuwa na matokeo mabovu.
Afisa Habari wa ‘Wakata miwa’ hao. Thobias Kifaru alisema kwamba ushiriki wao wa Championship ni kama wanafanya utalii, ili kujua mandhari yake, na kisha kurudi Ligi Kuu kuwasimulia wengine maisha ya huko.
“Huku ni kama tumekuja kutalii na kujionea maisha ya Chamionship yalivyo, halafu tutarejea zetu Ligi Kuu tukiwa tuna taarifa zote za kinachoendelea huko kwa sababu kwa sasa hatukamatiki na tunajihisi hatuna mpinzani wa kutusumbua,”alisema Kifaru.
Alisema kwamba imani yao ni kuona wanarejea kwenye Ligi Kuu msimu ujao na kujiwekea mipango ya kuhakikisha hawashuki tena daraja kwa sababu chanzo wameshakijua, na wamejifunza.
Hivi karibuni Mtibwa ilicheza mechi ya kirafiki na Azam FC na kuiadabisha kwa kuichapa bao 1-0 kwenye mchezo uiopigwa Manungu Complex mjini Morogoro.

DAR ES SALAAM

Na Arone Mpanduka

Siku chache baada ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara kupaa hadi nafasi ya nne kwa ubora barani Afrika, timu shiriki za Ligi hiyo zimeshauriwa kuongeza ushindani ili kuondoa mazoea ya timu zile zile kupokezana ubingwa.
Hayo yamesemwa na beki wa zamani wa Taifa Stars Bakari Malima wakati akitoa mtazamo wake kuhusiana na ubora wa Ligi hiyo ikilinganishwa na ilivyokuwa katika miaka ya zamani.
Alisema kuwa bado kumekuwa na kasumba ya Ligi hiyo kuwa na ushindani wa timu tatu ama nne zinazowania ubingwa kila msimu, huku timu zingine zikiwa zinashiriki kuwania kutoshuka daraja.
“Ligi Kuu ni bora, lakini kila msimu kumekuwa na ushindani wa timu tatu ama nne pekee, ambazo zinawania ubingwa.Sasa kwenye hilo, kunahitaji uboreshaji hasa kwa timu zenyewe kuongeza ushindani ili kuleta uimara,”alisema Malima.
Alisema pia kuwa ifike wakati bingwa wa Ligi Kuu asitabirike kirahisi, kwa maana ya kwamba ikitokea Yanga ameyumba, basi Simba anapewa nafasi, au ikitokea Simba kayumba kwenye msimu, Yanga anapewa nafasi ya ubingwa katika wakati ambao hata msimu haujafika katikati.
Malima alisema kwamba hata mechi zinazohusisha Simba, Yanga na Azam FC dhidi ya timu zingine, bado imekuwa ni rahisi sana kutabiri nani atashinda, tofauti na ilivyo katika Ligi zingine.
Alitolea mfano Ligi Kuu ya Uingereza, ambayo kila msimu imekuwa ni ngumu kumtabiri bingwa pamoja na mechi moja moja zinazochezwa ambazo mshindi amekuwa haeleweki, na hivyo kuwapa shida watu wanaobashiri mechi hizo.
Katika hatua nyingine, Malima alisema kuwa uongozi bora na ubora wa miundombinu, ndiyo silaha kubwa ya kupanda viwango kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Alisema kwamba katika miaka ya zamani ambayo yeye alicheza soka, Chama cha Soka nchini FAT (Football Association of Tanzania) kwa wakati ule, kilitawaliwa na migogoro ya mara kwa mara, huku viwanja vingi vya kuchezea vikiwa chakavu.
“Ninakumbuka zamani uwanja mzuri ambao wachezaji tulikuwa tunapenda kuuchezea ni wa CCM Kirumba uliopo jijini Mwanza lakini zaidi ya huo, hakukuwepo na uwanja mwingine mzuri. Hata wa Uhuru haukuwa sawa kwenye eneo la kuchezea,”alisema Malima.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi, akisalimiana na Calistre Camilius Lekule wa Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu  - Makongo Juu, wakati wa kumshika mkono Askofu kwenye Adhimisho la Misa Takatifu ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, iliyoadhimishwa parokiani hapo sanjari na uzinduzi wa Shule mpya ya Awali na Msingi ya Mary of The Rosary Pre & Primary School-Makongo.

Dar es Salaam

Na Pd. Richard Mjigwa- C.PP.S

Mwenyeheri Giovanni Merlini ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda, amini wa Injili na mshauri mwenye busara.
Hayo yamo katika Waraka wake wa Kitume wa Baba Mtakatifu Fransisko wa kumtangaza Mwenyeheri huyo, ambaye Sikukuu yake itaadhimishwa kila mwaka Januari 12.
Mwenyeheri Giovanni (pichani) yeye alikuwa ni mhubiri mahiri; Mshauri mwenye busara na mjumbe wa matumaini na amani katika Kristo Yesu.
Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu anajifunua, kwa watu wake waliokuwa wamepokea Ubatizo wa toba na maondoleo ya dhambi.
Hii ni siku ya Ufunuo wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. “Huyu ni mwanangu, mpendwa wangu ninayependezwa naye” (Mt, 3:13-17, Mk, 1:9-11, Lk, 3:21-22). Ni tukio linalotakatifuza maji yote ya Ubatizo, na umuhimu wa maisha ya sala. Rej Lk, 3:21 na katika kusali, Kristo Yesu anawafundisha Wafuasi wake kusali. Rej KKK 2607.
Huu ni mwaliko kwa Waamini kutafakri ufunuo wa Sura na Sauti ya Mungu. Ubatizo wa Bwana unahitimisha maadhimisho ya Kipindi cha Noeli, Mwanzo wa: maisha na Utume wa Kristo na ni siku maalum ya Ubatizo kwa watoto wachanga, changamoto na mwaliko kwa wazazi na walezi kuwarithisha watoto wao zawadi ya imani.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Fransisko, Dominika Januari 12, 2025 amemtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini, kuwa ni Mwenyeheri na ambaye alizaliwa tarehe 28 Agosti, 1795 huko Spoleto, Perugia nchini Italia.
Akapewa daraja Takatifu la Upadri Desemba 19, 1818. Agosti 15, 1820 akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, lililokuwa limeanzishwa na Mtakatifu Gaspari del Bufalo Agosti 15, 1815. Alijiunga na Shirika baada ya kuvutiwa sana na mahubiri yaliyotolewa na Mtakatifu Gaspari, kuhusu Fumbo la Ukombozi chemchemi ya upendo wa kimisionari.
Kumbe, Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ndiyo msingi wa ukombozi wa mwanadamu, na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote.
Tasaufi hii ina msingi wake katika, na Neno la Mungu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, ambalo ndilo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa, na maisha ya Mkristo kwa jumla.
Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa Imani ya Kikristo, na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. Rej KKK 1324 na 1327. Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, Agano Jipya na la Milele, ikawa ni msingi wa maisha na sadaka, kwa bidii ya kutafakari na shauku ya kitume “cum ardore contemplativo et passione apostolica.”
Mwenyeheri Giovanni Merlini aliishi nyakati za Mapinduzi ya Napoleone, wakati wa mchakato wa mafundisho tanzu ya Kanisa. Papa Pio IX Desemba 8, 1854 akatangaza rasmi kwamba, Mwenyeheri kabisa Bikira Maria, tangu nukta ya kutungwa kwake mimba, kwa neema na upendeleo wa pekee wa Mwenyezi Mungu, kwa kutazamia mastahili ya Kristo Yesu, Mwokozi wa wanadamu wote, alikingiwa na kila doa la dhambi ya asili.
Mwenyeheri Giovanni Merlini akatangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika maisha ya kila siku kwa kutambua mbegu za Ufalme wa Mungu, na hivyo akajipambanua kuwa ni chombo cha huruma ya Mungu na amani; na shuhuda wa matumaini yasiyotahalisha. “Spes non confundit.”
Kati ya Mwaka 1847 hadi 1873 aliteuliwa kuwa ni Mkuu wa tatu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu. Kama kiongozi, akaonesha utakatifu wa maisha, udugu, ari na mwamko wa kimisionari; ukaribu na majadiliano katika ukweli na uwazi; kupima mang’amuzi ya maisha na utume wa Kimisionari mbele ya Msalaba. Ni katika wakati wa uongozi wake, Shirika likapanuka na kuenea nje ya mipaka ya Italia hadi Kaskazini mwa Ulaya na nchini Marekani.
Katika maisha na utume wake alibahatika kuwa ni kiongozi wa maisha ya kiroho kwa Mtakatifu Maria De Mattias, utume alioutekeleza kwa kipindi cha miaka arobaini na miwili.
Akasaidia kujenga na kuwaimarisha Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, ASC. Katika mashauri yake alikazia: majadiliano katika utu, heshima na ukuaji wa maisha ya kiroho, daima wakitafuta mapenzi ya Mungu.
Mwenyeheri Giovanni Merlini, alisaidiana na Mtakatifu Gaspari del Bufalo kupyaisha maisha ya Waamini na Makleri kwa namna ya pekee kama yaliyoasisiwa na Papa Pio VII (1800-1823: wa 251) na Pio 1X kwa njia ya mahubiri, mafungo, na hata wakati mwingine akahatarisha maisha yake kwa kutangaza Injili miongoni mwa majangili, kielelezo cha mtume wa msamaha unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo.
Fumbo la Pasaka ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba Waraka wa Kitume wa “Amantissimus human” wa Mwaka 1862 ulionesha umuhimu wa Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo, na kunako mwaka 1849 katika Waraka wa Kitume wa “Redempti sumus,” Sikukuu ya Damu Azizi ya Yesu, ikatangazwa kuwa ni Sikukuu kwa Kanisa zima. Mwenyeheri Giovanni Merlini akaitupa mkono dunia tarehe 12 Januari 1873 kwa ajali.
Tarehe 10 Mei 1973, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, likamtangaza kuwa ni Mtumishi wa Mungu. Tarehe 23 Mei 2024 Baba Mtakatifu Fransisko akaruhusu atangazwe kuwa ni Mwenyeheri. Katika Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, Dominika tarehe 12 Januari 2025 akatangazwa kuwa ni Mwenyeheri.
Jumamosi tarehe 11 Januari 2025, kukafanyika Ibada ya mkesha wa nguvu ukiongozwa na AskofuVincenzo Viva wa Jimbo Katoliki Albano, nchini Italia. Misa ya shukrani imeadhimishwa Jumatatu, tarehe 13 Januari 2025 kwa kuongozwa na Askofu Mkuu Renato Boccardo wa Jimbo Kuu la Spoleto, Italia.
Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa Kitume wa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Giovanni Merlini kuwa ni Mwenyeheri, anasema, kwa hakika alikuwa ni Mtume mwenye ari na mwamko wa Fumbo la Pasaka ya Kristo linaloleta wokovu, shuhuda amini wa Injili na mshauri mwenye busara.
Sikukuu yake itakuwa inaadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Januari. Baba Mtakatifu Fransisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana alisema, Giovanni Merlini, Padri Mmisionari wa Shirika la Damu Azizi, alijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya utume kwa watu wa Mungu, akawa mshauri mwenye busara kwa roho nyingi, na mjumbe wa amani.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Stephano Musomba - OSA (mwenye fimbo ya kichungaji), akiwa katika picha ya pamoja na Mapadri na Viongozi wa Kamati Tendaji wa Parokia ya Mtakatifu Pio wa Pietrelcina - Ulongoni ‘B’, baada ya Adhimisho la Misa Takatifu ya Sherehe ya Miaka 10 ya Parokia hiyo. Kushoto kwa Askofu ni Paroko wa Parokia hiyo, Padri Leonard Amadori - OFMCap (Picha na Mathayo Kijazi)

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Sana Jude Thaddaeus Ruwa’ichi akiwa katika picha ya pamoja na Mapadri, Viongozi wa Kamati Tendaji na Kamati ya Ujenzi wa Shule mpya ya Awali na Msingi ya Mary of The Rosary Pre & Primary School ya Parokia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu - Makongo Juu.