DAR ES SALAAM
Na Angela Msele
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amewausia Waamini na watoto kuacha dhambi ya wivu, kwani itawasababishia kupata ukoma wa kiroho.
Amewakumbusha Waamini kufahamu kwamba Agosti 8 kila mwaka, ni siku ya kumuenzi Mtakatifu Dominiko aliyeishi karne ya 13, ambaye ndiye mwanzilishi wa Shirika la Dominiko.
Askofu Mkuu Ruwa’ichi aliyasema hayo hivi karibuni wakati akihubiri katika Adhimisho la Misa Takatifu ya Shukrani kwa Mungu kwa safari za Kitume za Watoto wa Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam walizozifanya katika Jimbo Katoliki la Kondoa mkoani Dodoma na Utete mkoani Pwani, iliyofanyika Parokia ya Bikira Maria wa Fatima – Msimbazi, jimboni Dar es Salaam.
“Tunakuwa wakoma wa kiroho pale tunapochukiana na kuoneana wivu, na tunapofanya mambo mabaya yanayowaumiza wenzetu,”alisema Askofu Rua’ichi na kuongeza;
“Yesu anatufundisha Neno la Mungu, yeye ambaye ni Neno wa Mungu, kwa upendo wake alifufua wafu, aliwaponya wagonjwa na kulisha wenye njaa…daima tunatakiwa kuwa watu wa sala, kwa sababu hata Yesu ambaye ni mwana wa Mungu, alisali.”
Askofu Mkuu Ruwa’ichi alibainisha kuwa sala ni mahusiano kati ya binadamu na Mungu, inayowaunganisha wanadamu na Mwenyezi.
Naye aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Taifa (PMS), Padri Jivitus Kaijage, alimshukuru Mungu kwa kumaliza salama muda wake wa utume katika nafasi hiyo, akimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa ushirikiano wake katika kipindi chote cha miaka 12 ya kuwa Mkurugenzi wa mashirika hayo.
Kwa upande wake Padri Alfred Gwene, Mkurugenzi mpya wa PMS,Taifa, aliwataka walezi kuwafundisha sala watoto hao na kuwafanya washiriki shughuli zote za kimisionari.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Walezi wa Utoto Mtakatifu Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Cletus Majani, alimshukuru Askofu Mkuu Ruwa’ichi kwa kuwapa ruhusa ya kushiriki Makongamano yote yaliyofanyika katika Majimbo hayo.
Aliongeza kuwa Kongamano la Utoto Mtakatifu lililofanyika Utete mkoani Pwani, lilizaa matunda kwa kupata kijana wa Kidato cha Pili kutoka Dini nyingine, ambaye aliomba kubatizwa ili awe Mkatoliki, ambaye tayari ameanza mafundisho, kwa ruhusa ya wazazi wake.
Katika misa hiyo parokia 10 bora zilizotoa idadi kubwa ya watoto katika Makongamano hayo, zilipoongezwa na kuzawadiwa vyeti.