Katika safu hii ya Chimba Chimba Historia ya Kanisa wiki iliyopita, tuliwaletea historia ya Uinjilishaji katika nchi za Afrika ya Kati na Camroon. Leo tunaanza kuwaletea historia ya Uinjilishaji ulivyoingia katika nchi ya Afrika Kusini. Sasa endelea…
Nchi ya Afrika ya Kusini kabla ya Wazungu kufika huko, ilikaliwa na Wasan au Wahentoti kama Wazungu walivyowaita pamoja na Wabantu wakiwemo Wazulu, Waxhosa na wengine.
Ingawa Wareno walipita Afrika ya Kusini wakienda India, hawakuacha misioni yo yote kule. Vile vile hawakufanya koloni za kudumu huko. Wakoloni wa kudumu walifika mwaka 1650 wengi waliokosa makazi kwao wengi wao wakltoka Uholanzi, na wachache Ujerumani na Ufaransa.
Wote hao waliunganishwa na imani moja walikuwa Waprotestanti Wakalvinisti wenye siasa kali. Katika imani yao walijiona siyo kama watu weusi bali wao walikuwa wateule wa Bwana na matendo yao yalidhihirisha hilo.
Kwa uhakika walijua kwamba walikuwa wameokoka, walitumia Biblia (Mwa, 9) hasa simulizi juu ya Ham mtoto wa Noa, kuonyesha kwamba watu weusi walikuwa watoto wa Ham waliolaaniwa.
Hii ilikuwa dhana ya Wazungu wengi, isipokuwa dhamira na mtazamo wa uhusiano na namna ya kusaidia, ilikuwa tofauti. Comboni Mmisionari mkubwa Mkatoliki huko Sudan aliongelea juu ya kuwaombea ‘watoto maskini wa Ham,’ akitaka kuona kama nao wanaweza kukombolewa, ingawa ni vigumu.
Wakalvinisti waliongelea juu ya ‘watoto wa Ham waliolaaniwa’ na hivyo hakuna la kufanya kuwasaidia. Bahati mbaya vile vile wale Wakalvinisti wa Kanisa la Mageuzi la Uholanzi hawakuwa na sera ya Uinjilishaji kwa Waafrika kwa sababu kwao waliokoka wale tu waliopangiwa na Mungu, ambao walionyesha ishara za nje za wokovu.
Kwa Waafrika, ishara za nje, ikiwemo kuwa na wake wengi, ilionyesha kwamba hawakuchaguliwa na Mungu, na hilo mtu huwezi kuligeuza.
Nchi ya Afrika ya Kusini ilipotekwa na Waingereza miaka ya 1806-36, utumwa ulipigwa marufuku, lakini Waafrika walibaki kuwa watumishi na manamba kwa manufaa ya Wazungu. Wakalvinisti walibuni mafundisho ya dini (teolojia) ya ubaguzi mkali kwamba Mungu aliumba mtu mweusi amtumikie mzungu.
Madhehebu mengine ya Kikristu pamoja na serikali ya Uingereza walipopinga sera na mafundisho hayo ya dini, Wazungu wengine zaidi ya 6,000 wenye siasa kali walihamia kaskazini hadi Rhodesia (sasa Zimbabwe).
Huko walitaka wawe na nchi yao, ili wawe na uhuru wa kuwatumikisha Waafrika bila kubughudhiwa. Wao walijiona kama Waisraeli wa zamani, taifa teule ambalo Mungu amewatoa katika nchi ya mateso, na anawapeleka katika nchi ya agano atakayowapa.
Kuingia kwa Wamisionari Waprotestnti Afrika Kusini:
Wamisionari wa kweli wa kwanza walikuwa wa dhehebu la Moraviani kutoka Ujerumani waliofika Afrika Kusini mwaka 1792. Baadaye yalikuja mashirika mengine ambayo yalikuwa na mafanikio makubwa zaidi kama Shirika la Kimisionari la London (London Missionery Society: LMS), ambao ni Waanglikana Wainjilisti waliofika huko mwaka 1799.
Wamisionari hawa walifanya kazi kubwa sana kupigania haki za watu weusi. Kwa namna ya pekee, Dk. Yohannes van der Kemp aliyepigana sana dhidi ya ukatili wa Makaburu. Wakati huo Makanisa ya Wakaburu yalisisitiza ndani ya Kanisa kuwatenga kati ya Wazungu na Wachotara (mchanganyiko wa wazazi Wazungu na Waafrika) na kuwajengea Waafrika makanisa yao. Zaidi soma Tumaini Letu...